Mshambuliaji nyota wa Mbeya City Fc Paul Nonga amesema mvua kubwa iliyonyesha masaa mawili kabla ya mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara baina ya timu yake na Ndanda Fc uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya imesababisha kukosekana kwa ushindi wa idadi kubwa ya mabao waliokuwa wamepanga kuupata.
Akizungumza mapema leo Nonga aliyefanikiwa kupachika mabao 6 kwenye ligi msimu uliopita alisema kuwa yeye na wachezaji wenzake walikuwa wamejiandaa kushinda mchezo huo kwa idadi kubwa ya magoli lakini mvua iliyonyesha iliwafanya kushindwa kucheza vizuri kufuatia utelezi uliokuwepo uwanjani hapo.
"Mchezo ulikuwa mzuri, lakini mvua imetufanya kushindwa kupata mabao mengi kutokana na kuwepo utelezi mwingi uwanjani, tulijiandaa kushinda kwa idadi kubwa lakini pia tunashukuru kwa ushindi tuliopta kwasababu tumeongeza poiti tatu muhimu tulizokuwa tunazihitaji zaidi" alisema Nonga
Katika mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Mbeya City ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Deus Kaseke katika dakika ya 5 ya mchezo.
Fredy Cosmas wa Mbeya City Fc (kulia) akipiga mpira mbele ya Zabron Raymond wa Ndanda Fc ya Mtwara.
Comments
Post a Comment