Mwanadada Luizer Mbutu, mmoja wa waimbaji mahiri wa muziki wa dansi, sasa anatarajiwa kuongoza onyesho kubwa la Twanga Pepeta la kusherehekea miaka yake 16 mfululizo ya kuitumikia bendi hiyo, Jumamosi ya Januari 31.
Hii ni baada ya onyesho hilo kuahirishwa mara kadhaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo vya wasanii waliotarajiwa kushiriki tukio hilo la kihistoria. Mara ya mwisho onyesho hilo lilipangwa kufanyika Disemba 20.
Kama ilivyopangwa hapo awali, katika onyesho hilo litakalofanyika Mango Garden, Luizer anatarajiwa kuwakusanya nyota wengi wa Twanga Pepeta ambao kwa sasa wako na bendi zingine.
Saluti5 imefahamishwa kuwa nyota kadhaa waliowahi kufanya kazi na Luizer Twanga Pepeta, katika vipindi tofauti ndani ya hiyo miaka 16, watakwea jukwaa la Mango Garden kumpa tafu mwimbaji huyo bora wa kike Tanzania kupitia Kili Music Awards.
Meneja wa Aset, Hassan Rehani ameifahamisha Saluti5 kuwa miongoni mwa vitu vitakavyofanywa na Twanga Pepeta siku hiyo, ni kupiga nyimbo zote kali alizoshiriki kuimba Luizer ili kutoa nafasi kwa mwanadada huyo ya kujipambanua mbele ya mashabiki wake juu ya kile alichokizalisha Twanga ndani ya hiyo miaka 16.
Comments
Post a Comment