MKWASA : YANGA SC SASA KICHEKO TU


MKWASA : YANGA SC SASA KICHEKO TU

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Kocha msaidizi wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa amewataka mashabiki wao kutembea kifua mbele kwa kuwa mafanikio yanakuja Jangwani.

Mkwasa amerejea tena Yanga SC kama Kocha Msaidizi baada ya uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani, Dar es Salaam kumfungshia virago aliyekuwa kocha mkuu Mbrazil Marcio Maximo na msaidizi wake Leonardo Neiva wiki iliyopita.

mk
Katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya Yanga SC zilizopo makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam leo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, Jerry Muro amesema Mkwasa amemhakikisha kikosi chao kiko vizuri kambini mjini Bagamoyo, Pwani kujiandaa kwa mechi inayofuata dhidi ya Azam FC.

"Tumewasiliana na kocha msaidizi (Mkwasa) leo asubuhi. Ametuambia kikosi kiko vizuri na hakina mchezaji hata mmoja aliye majeruhi. Amewataka wanayanga sasa kutembea kifua mbele maana mambo mazuri yanakuja," amesema Muro.

Yanga SC itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Azam FC katika mechi ya raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu kutokana na historia kati ya timu hizo mbili.

Licha ya kuifunga Azam FC mabao 3-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii msimu huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga SC haikuifunga timu hiyo ya wanalambalamba katika mechi mbili za msimu uliopita wakipoteza 3-2 katika mechi ya mzunguko wa kwanza kabla ya kutoka sare ya 1-1 katika mechi ya mzunguko wa pili.

Azam FC iliyokuwa imeweka kambi ya siku 10 jijini Kampala, Uganda kujiandaa kwa mwendelezo wa VPL msimu huu, iko nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 13 sawa na Yanga SC, pointi mbili nyuma ya vinara Mtibwa Sugar.

Timu hiyo ya kocha Mcameroon Joseph Omog — Azam FC, inabebwa na faida ya herufi katika nafasi ya pili baada ya kufanana kwa kila kitu na yanga SC.



Comments