Ili wimbo uweze kukamilika huwa unakuwa na vipengele kadhaa ndani yake. Kuna maneno au mashahiri, au kwa lugha ya siku hizi 'mistari' na kwa kiingereza Lyrics. Mistari huhitaji kupewa sauti ya kuimbia, Melody. Baada ya hapo hutengenezwa arrangement , au mpangilio wa muziki huo, nini kinakuja wapi, waimbaji waimbe vipi na kujumlisha kazi zote hizi unapata wimbo mmoja. Kwa uzoefu wa bendi zetu, mara nyingi, Lyrics huletwa na mtu mmoja, anaweza akaleta mistari yenye melody au akaleta mistari peke yake na kutaka msaada wa wanamuziki wenzie watafute melody. Kazi inafuata ya arrangement pia hufanywa kwa ushirikiano na hatimae kukapatikana wimbo ambao kwa utamaduni wetu huwa tunatangaza kuwa mtunzi ni yule aliyekuja na mistari.
Si kila mtu ana kipaji cha kutunga, japo hiyo ndio imani ya wengi kuwa kila anaejua kuimba hujua kutunga. Waimbaji wengi maarufu duniani waliimba nyimbo zilizotungwa na wengine, na halikadhalika si kila anaetunga anajua kuimba, watunzi hata wa mashahiri huwaachia watu wengine waghani mashahiri yao, mtunzi akilazimisha kuimba wakati hana kipaji hicho matokeo ni madudu tu na hali kadhalika muimbaji asiye na kipaji cha kutunga aking'ang'ania kutunga kipawa chake cha kuimba kinaweza kisionekane kutokana na utunzi kuwa hafifu.
Na hali kadhalika si kila mtu ni arranger, tatizo ni pale asiekuwa na kipaji anaamua kufanya hiyo kazi, kinachotoka hakieleweki kama kinakwenda au kinarudi.
Kama nilivyosema awali katika bendi arrangement huwa ni mchango wa mawazo, lakini ukifanya utafiti kidogo utagundua hata katika kazi inayoonekana ni kikundi kuna mtu au watu ndio wanaoongoza nini kipigwe wapi. Katika bendi nilizopitia kama vile Orchestra Mambo Bado, Orchestra Makassy au Vijana Jazz enzi hizo kulikuwa na mtu ana sauti ya mwisho kuhusu arrangement, enzi za Mambo Bado Assossa ndie aliyekuwa na maamuzi ya mwisho kuhusu kipengele katika wimbo, wakati nikiwa Makassy , Mzee Aimala Mbutu ndie aliyekuwa mwongozaji katika kufanya arrangement, enzi za Maneti yeye ndie aliyekuwa akikubali au kukataa kitu katika tungo, japo kwa bahati awamu baada ya Maneti ilikusanya arrangers kama Beno Villa, Jerry Nashon na Shaaban Wanted ambao kwa pamoja matokeo ndio vibao kama VIP, Shoga, Thereza na kadhalika. Kupendwa kwa wimbo ni mkusanyiko wa haya niliyoyataja hapo juu. Nyimbo nyingi zinazopendwa sasa hazitachukua muda kusahaulika kutokana na kuwa na arrangement hafifu sana. Mfumo wa sasa wa waimbaji kujaza wimbo wote bila kuweko na hata nafasi ya vyombo kutamba ni aina moja ya arrangement lakini kwa mtazamo wangu nyimbo hizi zitasahaulika katika kipindi kifupi.
Katika mfumo wa uajiri au utafutaji wa wanamuziki katika bendi zetu, umuhimu hutolewa kwa wapiga vyombo na waimbaji, nadra kusikia mtunzi anatafutwa na nadra zaidi kusikia anatafutwa arranger, hivyo huwa bahati tu akatokea arranger mzuri au mtunzi mzuri katika bendi na si kutokana na mipangilio, na nina wajua arrangers wengi ambao hata wao hawajui kuwa ni arrangers, hivyo 'majembe' kama hayo yakifukuzwa au kuhama bendi, basi bendi inaanza kudorora, na si mara moja nimekuta hata bendi zenyewe hazijui kwanini ghafala kuna ukame wa tungo nzuri, pengine yule msanii aliyeitwa mzigo, kwa kuwa hakuwa muimbaji mzuri alikuwa ndie arranger bora wa bendi hiyo!!!
Mara nyingi siku hizi huwa naingia katika bendi na kukuta wakitangaza wimbo mpya, ukipigwa unagundua kuwa wimbo huo kimsingi ni mzuri lakini arrangement yake hafifu mno, na unaweza kukuta bendi ina wanamuziki vigogo lakini tungo zao hazitikisi wasikilizaji, tatizo ni aidha tungo zina melody hafifu au melody ni nzuri lakini arrangement ziro.
Labda niseme kwa kifupi, arrangement ndio ule mpangilio wa kuamua nini kipigwe na kipigwe wapi. Muziki unasheria za msingi kama vile hesabu.2+2=4, si nne na nusu wala na robo, arranger anakuwa na kipaji cha kupanga nini na anaweza kukueleza kwa nini pale kipigwe kinanda na gitaa liwe kimya au pale vipigwe vyote na kwanini iwe hivyo.
Muziki wetu wa Bongoflava, umetawaliwa na waimbaji kwani swala la utunzi wa muziki na arrangement (kunakotambuliwa kama kutengeneza beat), huachiwa 'producer'. Ni wazi ukisikiliza mfululizo wa nyimbo zinazotoka kila siku ni wazi kuwa maproducer wachache sana wanakipaji cha kuarrange, utasikia vyombo vinalia katika wimbo bila kuwa na mpangilio wala sababu ya kuwepo, hapa utasikia filimbi, mara saksafon, mara rimba, mara gitaa , hivyo wapenzi wengi wa muziki wanaweza sana kukuimbia wimbo fulani lakini hawakumbuki na vyombo gani vilivyopigwa na vilipigwa vipi. Na mara nyingi wimbo usiokuwa na kumbukumbu hivyo hupotea mawazoni mapema sana.
Kutokana kutokuelewa maana halisi ya majina ya mapigo, watu huunganisha staili na kundi au muimbaji, hata wanamuziki wenyewe unaweza kusikia mi naimba zouk, au mimi naimba reggae au mi sipigi rumba napiga Taarb, lakini kwa mfano nyimbo nyingi za vikundi vya Taarab zinapigwa katika midundo ya rumba, na hata nyingi za Bongoflava na hasa zinazofuata mipigo ya 'Kinaijeria' ni mipigo ya rumba. Karibuni muimbaji mahiri Isha Mashauzi amerekodi kibao kizuri sana katika mipigo ya rumba lakini wengi huuita wimbo huo ni wa Taarab
Kwa sababu rumba, charanga, chacha, reggae na kadhalika ni midundo itokanayo na aina ya ngoma, vyombo vyote vinavyopigwa katika arrangement ya muziki huo hulazimika kufwata mapigo hayo. Hapo ndipo umahiri wa kupanga vyombo hivyo humtenganisha arranger mahiri na mbabaishaji
Comments
Post a Comment