MECHI YA WATANI SHINYANGA DESEMBA 24



MECHI YA WATANI SHINYANGA DESEMBA 24

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Timu za Stand United na Mwadui FC za Shinyanga zitakutana katika mechi maalum ya kirafiki kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani humo iliyoandaliwa kwa ajili ya kumaliza uhasama baina ya timu hizo.
st
Kumekuwa na uhasama mkubwa katika ya timu hizo baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuinyima kibabe Mwadui FC nafasi ya kupanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) licha ya kufuzu msimu uliopita wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na kuipandisha kwa upendeleo Stand United.

Kutokana na uhasama huo, Mkurugenzi wa Ufundi wa Stand United, Muhibu Kanu amesema kuwa viongozi wa pande zote mbili wamekutana na kuamua kuumaliza uhasama huo na timu zao zitachuana katika mechi hiyo ya kirafiki siku moja kabla ya Sikukuu ya Krismasi.

Stand United inayonolewa na Emmanuel Masawe iko nafasi ya 10 katika msimamo wa VPL ikwa na pointi tisa wakati Mwadui FC inayofundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio' inakamata nafasi ya kwanza katika msimamo wa Kundi B la FDL ikiwa na pointi 22 sawa na Toto Africans ya Mwanza.

Wakati huo huo kikosi cha Mwadui FC kimeishika kwa sare ya mabao 2-2 timu ya Ruvu Shooting Stars katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani leo.

Mshambuliaji mpya wa Ruvu Shooting Betram Mwombeki aliyeichezea Simba SC msimu uliopita ameng'ara katika mechi hiyo baada ya kukifungia kikosi cha Mkenya Tom Olaba kabla Mwadui FC hawajacharuka na kurudisha mabao yote.



Comments