TIMU ya magolikipa inayoongozwa na mlinda mlango Ivo Mapunda wa Simba, Shaaban Kado wa Coastal Union na Salehe Malande wa Ndanda juzi waliiongoza timu yao ya Chama Cha Magolikipa Tanzania (TAGA FC) kuiadhibu ile ya waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa FC) magoli 3-0 kwenye mchezo maalum wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini Dar es salaam.
Awali mchezo huo ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa Karume kabla ya kuahamishiwa uwanja wa bora kutokana na ?Mizengwe? ya dakika za mwisho ya wamiliki wa uwanja huo.
Timu zote zilianza mchezo huo kwa kasi na kukosa nafasi kadhaa za wazi. TAGA ndio ilikuwa ya kwanza kulifikia lango la Taswa FC ambayo ilizindua jezi zake kwa mara ya kwanza zilizotolewa na Benki ya Posta Tanzania (TPB), hata hivyo shuti la mshambuliaji, Ivo Mapunda likatoka nje.
Makipa walikuwa katika nafasi nzuri ya kufunga tena katika dakika ya sita ya mchezo, hata hivyo penati ya Shaaban Kado ikipanguliwa na kipa wa Taswa, Ahmed Famau.
Taswa FC iliibuka katika dakika ya nane ya mchezo na Zahoro Mlanzi alikosa bao la wazi akiwa na kipa wa TAGA FC, Fatuma Omari ambaye pia alifanya kazi ya ziada kuokoa mipira miwili ya kona iliyopigwa na Majuto Omary ambayo ilielekea golini.
Licha ya kutofanya mazoezi kila siku kulinganisha na timu ya makipa, wachezaji wa Taswa, Ali Mkongwe, Martin, Majuto, Ibrahim Masoud, Zahoro Mlanzi, Shafii Dauda, Wilbert Molandi, Sweetbert Lukonge, Muhidini Sufiani, Salum Jaba, Juma Ramadhani na Julius Kihampa walionyesha uwezo mkubwa katika mchezo huo .
Mapunda aliipatia TAGA goli la kuongoza dakika ya 14 kufuatia krosi safi ya Saleh Malande aliecheza vizuri na Juma Kaseja na Ali Mustapha (Barthez)
Bao la pili la makipa lilifungwa na Shaaban Kado baada ya kazi nzuri ya Deogratius Munishi 'Dida' na Malande kuhitimisha ushindi wa TAGA dakika ya 86.
Rais wa makipa hao, Alex Ndembeka alisema kuwa wamefarijika sana mchezo huo ambao umetumika rasmi kuzindua chama chao ambacho lengo lake kubwa ni kuendeleza fani hiyo kwa kuvumbua vipaji na kuondoa fikra za kuwa ?magolikipa? hawapendani.
"Tunawapongeza waandishi kwa kukubali wito wetu na kufanikisha kuzindua chama hiki, nadhani umeona jinsi ilivyo kwa makipa wetu kucheza pamoja, kufurahi na kuondoa mtazamo hasi wa kuwa makipa hawapendani", alisema Ndembeka.
Comments
Post a Comment