KMKM, POLISI ZENJ ZAPEWA MTIHANI MICHUANO YA CAF


KMKM, POLISI ZENJ ZAPEWA MTIHANI MICHUANO YA CAF

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Zanzibar, KMKM wamepangwa na Klabu ya Hilal ya Sudan katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika huku Polisi Zanzibar wakipangwa na CF Mounana ya Gabon katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani mwakani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye mtandao rasmi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) leo, droo ya michuano ya 19 ya Klabu Bingwa Afrika mwakani na michuano ya 12 ya Kombe la Shirikisho barani imechezeshwa kwenye makao makuu ya CAF jijini Cairo, Misri leo asubuhi, klabu 58 zikichuana katika Klabu Bingwa na 56 katika Kombe la Shirikisho.
km
Michuano yote miwili ya bara itaanzia katika mechi ya awali zitakazochezwa kati ya Februari 13, 14 na 15 na kurudiana kati ya Februari 27, 28 na Machi Mosi mwakani.

Mechi za hatua ya kwanza kuwania kuingia 16 bora zitachezwa kati ya Machi 13, 14 na 15 na kurudiana kati ya Aprili 03, 04 na 05 na hatua ya 8-bora kuamua nani anaingia hatua ya makundi zimepangwa kuchezwa kati Aprili 17, 18 na 19 kwa mechi za kwanza kurudiana kati ya Mei 01, 02 na 03.

Kwa michuano ya Kombe la Shirikisho, mechi za kwanza kusaka timu zitakazoingia hatua ya nane bora zitachezwa kati ya Mei 15, 16 na 17 na kurudiana kati ya Juni 05, 06 na 07.

Katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, mabingwa watetezi ES Setif hawajapangwa katika hatua ya awali pamoja na timu za Coton Sport, AC Leopards, Al Ahly, TP Mazembe na timu mbili za Tunisia, CSS na EST.

Timu ambazo hazijapangwa katika hatua ya awali ya mtoano katika michuano ya Kombe la Shirikisho, ni Asec Mimoas, Zamalek, Djoliba, na wanafainali wa Klabu Bingwa mwaka huu AS Vita, Orlando Pirates, Ahli Shendi na Club Africain ya Tunisia.

Mshindi kati ya Hilal na KMKM baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini, atakutana na mshindi kati ya Fomboni Club de Mobeli dhidi ya Big Bullets ya Mali katika hatua ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika wakati mshindi kati ya Polisi Zanzibar na CF Mounana atakipiga dhidi ya mshindi kati ya Khartoum ya Sudan vs Power Dynamos ya Zambia katika hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho barani.



Comments