Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi limesita kutoa taarifa juu ya uwapo wa taarifa za ubadhirifu wa fedha kiasi cha Sh. bilioni mbili katika Klabu ya Yanga ya jijini hapa.
Taarifa za ubadhirifu huo zimeitikisa Yanga huku baadhi ya waliokuwa watendaji wa klabu hiyo kufikishwa kwenye vyombo vya usalama kwa tuhuma za kutafuna kifisadi kiasi hicho cha fedha hizo.
Katibu Mkuu mpya wa Yanga, DK. Jonas Tiboroha amethibitisha kubainika kwa ubadhilifu wa fedha ingawa hakuwa tayari kutaja kiasi kamili kilichobainika kuchotwa kijanja na baadhi ya wafanyakazi wanaodaiwa kuwa ni wale waliomaliza muda wao katika klabu hiyo hivi karibuni.
Baadhi ya wafanyakazi wa zamani wakiongozwa na aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Beno Njovu na aliyekuwa mhasibu Rose Msamila, wamedaiwa kufikishwa kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Polisi (Central) mjini hapa jana kuhojiwa kuhusu ubadhirifu huo.
"Ni kweli kuna suala hilo, lakini siwezi kuliongelea zaidi ni kina nani hasa wanahusika na kiasi cha fedha kinachotajwa kwa sababu tayari suala hilo liko chini ya Jeshi la Polisi. Watakapomaliza uchunguzi wao, watatujuza na sisi (Yanga SC) tutaliweka wazi," amesema Tiboroha.
POLISI WASITA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo baada ya kutafutwa na mtandao huu mjini hapa leo akisema: "Muulize RPC Ilala."
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mary Nzuki amedai hana taarifa za kuhojiwa na Polisi kwa waliokuwa watendaji wa Yanga SC.
"Mimi nimefuatilia kwenye vituo vyetu mbalimbali lakini sijapewa taarifa kuhusu kuhojiwa kwa watu wa Yanga. Pengine suala hilo limefanywa na kitengo cha upelelezi, ngoja niwasiliane nao kupata ufafanuzi," amesema kamanda huyo.
RPC huyo pia amekiri kuona picha mitandaoni zikiwaonesha baadhi ya waliokuwa viongozi wa Yanga SC wakiwa na Polisi.
"Waandishi wa habari wananiuliza sana kuhusu suala hilo, nimeona pia baadhi ya picha mitandaoni zikiwaonesha watendaji wa Yanga wakiwa na polisi lakini zijapata taarifa rasmi juu ya suala hilo," amesema zaidi.
Baadaye jioni hii RPC huyo amesemaL "Tumeangalia kwenye mafaili yetu hatuna suala hilo Mkoa wa Ilala, labda kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (Ofisi ya Kova)."
Inadaiwa kuwa fedha zilitafunwa kijanja kupitia malipo ya kambi mjini Antalya, Uturuki, nauli za usafiri wa ndege wa baadhi ya nyota wa kigeni.
Mwishoni mwa wiki, Yanga ilimtangaza Tiboroha kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo akichukua nafasi ya Njovu. Mtangazaji wa zamani wa televisheni za ITV na TBC, Jerry Muro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Habari na Mawasiliano, Omari Kaya aliteuliwa kuwa mkuu wa Idara ya Sheria ya klabu hiyo wakati Baraka Deusdetit aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Fedha.
Muda mfupi baada ya uteuzi huo kumegundulika kulikuwa na kile kinacoelezwa kama ubadhirifu miongoni mwa watangulizi katika utendaji wa klabu hiyo ya Jangwani.
Comments
Post a Comment