KAGERA SUGAR FC: SIMBA SC WATANG’OA VITI TENA TAIFA IJUMAA


KAGERA SUGAR FC: SIMBA SC WATANG'OA VITI TENA TAIFA IJUMAA

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Wakatamiwa wa Kagera, Kagera Sugar FC wameitishia nyau Simba SC wakitamba kuibuka na ushindi katika mechi yao inayofuata na kukumbushia ung'oaji viti kwenye Uwanja wa Taifa uliofanywa na baadhi ya mashabiki wa Simba SC msimu uliopita.

Licha ya Simba kusajili wachezaji nyota kutoka Uganda, Kagera Sugar FC wametamba kuivuruga tena kwa kuipa kichapo katika mechi yao ya keshokutwa.
mr
Kikosi cha Mzambia Patrick Phiri cha Simba, kilichokimbilia kambini Visiwani Zanzibar tangu Jumapili, kitakuwa na kibarua kigumu mbele ya wakatamiwa hao wa Kagera katika mechi hiyo ya raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mrage Kabange, kocha msaidizi wa Kagera Sugar, amesema jijini Dar es Salaam leo kuwa kikosi chao kiko vizuri na hawatishwi na majina ya nyota wa Simba SC.

"Kila mwaka Simba SC na Yanga SC zinapambana na kupigana vikumbo kusajili wachezaji wapya, lakini tunazifunga tu. Kilichowatokea Yanga mjini Bukoba (Kagera) msimu huu, ndicho kitakachowatokea Simba Ijumaa.

"Tumejiandaa vyema kwa ajili ya ligi, wala hatutishiki kuona Simba ina wachezaji wapya wenye majina," amesema Kabange akikumbushia kichapo cha bao 1–0 ambacho wameipa Yanga FC ya Mbrazil Marcio Maximo Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera msimu huu.

Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Hamis Madachi amesema leo kuwa kikosi chao kimo jijini hapa tangu jana tayari kwa mechi hiyo dhidi ya timu iliyoimarika ya Simba SC.

Kagera Sugar inayonolewa na Mganda Jackson Mayanja, haijasajili hata mchezaji mmoja dirisha dogo wakati Simba imesajili nyota watatu kutoka Uganda akiwamo mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu huu, Dan Sserunkuma na mdogo wake Simon Sserunkuma sanjari na Mganda mwenzao beki Juuko Murshid.

Simba, iliyoko nafasi ya saba katika msimamo wa VPL ikiwa na pointi tisa, moja nyuma ya Kagera walioko nafasi ya tano, itaingia kwenye Uwanja wa Taifa kesho ikisaka kisasi cha kulipishwa faini ya mamilioni ya shilingi kutokana na mashabiki wake kuanzisha vurugu na kung'oa viti vua uwanja huo baada ya wapinzani wao hao kusawazisha dakika ya mwisho katika mechi yao ya sare ya bao moja msimu uliopita.



Comments