JOHN STEPHEN AKHWARI :NGULI MCHEZO WA RIADHA ALIYEWEKA HISTORI YA KIMATAIFA

JOHN Stephen Akhwari ni miongoni mwa wanariadha wenye historia kubwa

hapa nchini kutokana na umahiri wake katika mchezo huo.

Akhwari anakumbukwa sana katika Michezo ya Olimpiki kutokana na kauli
yake ya kizalendo aliyoitoa wakati aliposhiriki mbio za marathoni
katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika huko Mexico mwaka 1968


JOHN Stephen Akhwari akiwa na baadhi ya medalii zake alizozipata katika mashindono ya riadha


Kwanini ANAKUMBUKWA?:
Wengi wamajiuliza mkongwe huyo wa riadha kwanini anaendelea hadi leo
kuwemo katika vitabu vya historia ya michezo ya Olimpiki, ambayo
hufanyika kila baada ya miaka minne?

Mwanariadha huyo mstaafu kwa sasa anakumbukwa sana kutokana na kauli
yake aliyoitoa baada ya kumaliza mbio hizo za marathoni licha ya
kutumia saa nyingi zaidi ya washiriki wengine waliomaliza mbio hizo.

"Nchi yangu (Tanzania), haijanituma kuja kuanza mbio ila imenituma
kuja kumaliza mbio, "alisema Akhwari baada ya kuulizwa na waandishi wa
habari sababu za kumaliza mbio hizo huku akivuja damu miguuni badala
ya kujitoa.


Kauli hiyo hadi leo imekuwa ni kitu cha kuwatia moyo washiriki na
mkimbiaji huyo wazamani hadi leo amekuwa akikumbukwa na jamii ya
Olimpiki duniani kwa uzalendo wake wa kuhakikisha anamaliza mbio hizo
na sio kujitoa bila kumaliza.

ALIKOTOKEA AKHWARI:
Baada ya kuangalia sababu za mkimbiaji huyo kupata sifa kimataifa hasa
katika Michezo ya Olimpiki, sasa tuangalie nguli huyo wa riadha
alivyofanya kweli katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Akhwari alikuwa mwanariadha wa kwanza kufungua mbio za kimataifa kwa
kupata ushindi nchini Ugiriki mnamo mwaka 1963, ambapo alishika nafasi
ya pili nyuma ya Joel Adeli wa Marekani.


 
 WAKATI alivyokuwa akikimbia riadha

Kwa ushindi huo ulizawadiwa jani ambalo halinyauki lililokuwa
likitumiwa enzi hizo kabla ya vikombe  pamoja na hundi ya dola 1,000
na Marekani, ambazo wakati huo zilikuwa ni pesa nyingi.

Hatahivyo, baada ya kurejea nchini na hundi yake hiyo alinyanganywa na
aliyekuwa mgeni rasmi aliyekuja kuwapokea uwanja wa ndege, ambaye
wakati huo alikuwa na wazifa mkubwa katika wizara ya michezo.

Anasema kuwa aliambiwa kuwa eti pesa hiyo inaingia katika mfuku wa
Kuendeleza Michezo, lakini wala haikuwa hivyo na badala yake pesa hizo
anasisitiza kuwa, ziliingia katika mfuko wa kigogo huyo wa Serikali.

Katika mazungumzo yetu huko nyumbani kwake Mbulu mkoani Arusha,
Akhwari anaelezea jinsi alivyofanya vizuri katika mashindano
mbalimbali ya riadha.


 muonekakano wake kwa sasa


Yafuatayo ni mahojiano amabyo mwandishi wa makla hii aliyafanya na
mkongwe huyo wa riadha hapa nchini Stephen John:

Mwandishi : Ndugu Stephen maswala ya riadhaa ulijiingiza rasmi mwaka gani?

Stephen: Nakumbuka ndugu mwandishi nilianza rasmi mnamo mwaka 1958
enzi za ukoloni na wakati huo nilikuwa ni mwanafunzi shule ya Msingi
na hasa yalikuwa ni mashindano ya Quin Day katika maadhimisho yake.

Mwandishi: Hayo mashindano yako ya kwanza yalikuwaje ?

Stephen : Yalikuwa ni mashindano ya kilomita zipatazo 15 na tulikuwa
Wanariaadha wapatao 70 nilishika nafasi ya 40 katika mashindano hayo
ya Queen Day au Siku ya Malkia.

Mwandishi: Baada ya kuibuka na ushindi huo mambo yalikuwaje ?

Stephen: Nilizawadiwa  Soda nakiri kuwa wakati huo ilikuwa ni mara
yangu ya kwanza kunywa soda  na sikunjwa peke yangu nilikunywa na
kugawana na wenzangu hiyo soda.

Mwandishi: Nini kiliendelea mara baada ya mashindano hayo ya Queen day?

Stephen : Tuliendelea na mazoezi ila wanne tuu ndio walikubali
kuendelea nami na tukaendelea nao hadi katika mashindano ya mkoa,
ambapo mashindano ya East Afrika waliniacha na mimi nikaenda peke
yangu.

Mwandishi: Katika mashindano ya East Afrika hali ilikuwa vipi?

Stephen : Katika Mashindano yale yaliyofanyikia Nairobi nilikuwa ni
mshindi wa kwanza  na ikapelekea kuchaguliwa kwenda katika mashindano
ya Jumuiya ya Madola.

Mwandishi : Haya mashindano ya Jumuiya ya madola yalifanyika nchi gani?

Stephen: Yalifanyika nchini Austaria na yalikuwa ya Full Marathoni,
yaani mbio za umbali wa kilometa 42 na nilishika nafasi ya sita katika
ya wanariadha wa mataifa mbalimbali.

Mwandishi:  Harakati yako katika riadha wapi?

Stephen :  Haikuishia hapo ndugu mwandishi mnamo mwaka 1963
nilikwenda  nchini Ugiriki kushiriki mashindano ya kimataifa
kwa upande wa mbio za marathoni.

Mwandishi: Matokeo ya mashindano hayo ya Ugiriki yalikuwaje?

Stephen : Nilishika nafasi ya pili  nyuma ya John Adel wa Marekani,
aliyekuwa akitisha kwa wakati huo na kupewa zawadi pamoja na hundi ya
dola elfu moja ya kimarekani.

Mwandishi:  Baada ya kujua hayo ni nini ulifanya ?

Stephen :  Nilikasirika nikaamua kususa riadha na kurudi kijijini na
baada ya miaka miwili nikarudi tena katika riadha mara baada ya
kuombwa na aliyekuwa mkuu wa majeshi enzi hizo  Jenerali Sarakikya.

Mwandishi : Mara baada ya kurudi katika riadha vipi uliendelea kushinda?

Stephen : Ndio ila nakumbuka Mwaka 1968 katika mshindano ya Mexico
fainali ya Olimpiki   mashindano y a kilomita 42  na nilimaliza nikiwa
majeruhi.

Mwandishi: ilikuwa vipi hadi ukapata majeraha hayo?

Stephen : Nilikimbia kiomita kama 30 nikateleza na kudondoka katika
barafu wakati huo Mexico katika barabara ilikuwa imetanda barafu
nikaumia vibaya sana katika mguu madktari wakanitibu na kunishauri
nisiendelee nikaamua kuendelea kumalizia kilomita 12 zilizobaki.

Mwandishi :  Katika Mashindano hayo kuna kauli uliyoitoa na kuonyesha
hali yako ya uzalendo ni ipi hiyo?

Stephen : Nakumbuka nilisema kuwa kuwa Nchi yangu ya Tanzania
haikunituma huko Mexico kuanza mbio ila imemtuma kumaliza mbio hizo.

 Mwandishi : Nini kilikusukuma kusema hivyo?

Stephen: Kwa kuwa nilikuwa peke nimekwenda kuwakilisha nchi yangu
sikutaka kutia aibu nchi yangu ni kaweka moyo wa kizalendo mbele.

Mwandishi: Unadhani kwamba wanariadha wa sasa wana moyo wa uzalendo
kama nyinyi wa zamani?

Stephen : Yaani ndugu mwandishi wanariadha wa sasa hawana uzalendo
kabisa wanapenda pesa ndio sababu inapelekea riadhaa kufa.

Mwandishi: Unashauri gani kwa wanariadha wa sasa?

Stephen : Nawataka wawe na moyo wa kizalendo na pia wajitume katika
mazoezi yao binafsi na wasitegemee sana mazoezi ya kambi au kufanya
mazoezi kwa ajili ya mashindano yanapokaribia.

 Mdada wa libeneke la kaskazini ambaye pia ni mwandishi wa habari wa habari hizi  Woinde Shizza akiwa anaongea na mzee John wakati alipomtembelea nyumbani kwake mbulu mkoani Manyara

 Mwandishi: Je kwa upande wa Serekali yetu una lipi la kutoa rai?

Stephen : Natoa rai kwa Seriakali iendelee kutoa ushirikiano mkubwa kwa
wanaoenda katika mashindano hata kama wamerudi na hawana ushindi.

Mwandishi: Ni ushirikiano gani unaotaka hasa kwa Serikali kutoa?

Stephen :Tumezoe timu ikirudi inaachwa halafu na kutegemea mara baada
ya mashindano mengine kuanza na ndio waanze kutafuta wanaanza
kutafutwa hii inaua Riadhaa inataka wawekwe kambini wasahihishwe
makosa waaliyafanya katika mashindano.

Hadi sasa hivi nguli huyu wa Riadha amebaki akiishi Huko mbulu na
amebakia akijishughulisha na kilimo huku akiwa na watoto wapatao sita
na Mtoto mmoj anafuata nyayo zake katika Riadha anayeitwa Rogat John
ambaye ameweka makazi yake jijini hapa.

 hii ndo nyumba ya mzee Akhwari mwanariadha aliyeweza kuipeperusha vyema bendera ya tanzania miaka ya nyumba


Makala hii imeandikwa na  Na Mwandishi Woinde Shizza kwa  uzamini wa Tanzania media fund


Comments