EL MERRIKH WAOMBA KUSHIRIKI KOMBE LA MAPINDUZI


EL MERRIKH WAOMBA KUSHIRIKI KOMBE LA MAPINDUZI

IMG_0558-0.JPG

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Klabu ya El Merrikh ya Sudan imeomba kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepangua tena ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kupisha michuano hiyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF zilizopo Posta, Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Boniface Wambura amesema wameziruhusu timu za Azam, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga kushiriki michuano hiyo itakayoanza keshokutwa na kumalizika Januri 13 Visiwani Zanzibar.

"TFF imetoa ruhusa kwa timu hizo kucheza mashindano hayo baada ya kuhakikishiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kuwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wake imeondolewa mahakamani.

Kutokana na timu hizo kushiriki Kombe la Mapinduzi, mechi zao za raundi ya tisa na 10 za VPL zitachezwa katikati ya wiki baada ya kumaliza mechi zao za michuano hiyo. Hivyo mechi za VPL ambazo hazitachezwa wikiendi hii ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Yanga, na ile ya Mgambo Shooting dhidi ya Simba.

"Mechi za wikiendi ijayo (raundi ya 10)zinazopisha michuano hiyo ni kati ya Kagera Sugar na Azam, Coastal Union na Yanga, Mbeya City na Simba, na Mtibwa Sugar dhidi ya Tanzania Prisons," amesema zaidi Wambura.

Hii ni mara ya tatu kwa TFF kupangua ratiba ya VPL baada ya kufanya hivyo mwanzoni mwa msimu wakiipanga kuanza Septemba 20 badala ya Agosti 24 kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.

TFF pia ilipangua mechi za raundi ya nne za ligi hiyo ikalazimika zichezwe Oktoba 18 badala ya Oktoba 12 kupisha mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Taifa Stars dhidi ya Benin.

EL MERRIKH
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Haji Salum aliyekuwa amefuana na Wambura leo, amesema wamepokea ombi la mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Sudan, timu ya El Merrikh kushiriki michuano hiyo.

"Ratiba ya michuano itatoka rasmi kesho maana tunasita kuitoa kwa sasa baada ya kupokea ombi la El Merrikh ambao wanataka waje pia kushiriki. Kufikia kesho tutakuwa tumeshajua ujio wao na ratiba itatoka," amesema Salum.

El Merrikh imepangwa kuanza na Azam FC katika hatua ya awali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani, hivyo ni wazi kwamba inataka kulitumia Kombe la Mapinduzi kwa maandalizi na kuwasoma wapinzani wake.

Salum amesema Simba SC na mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi, KCC FC ya Ligi Kuu ya Uganda, wataondoka jijini Dar es Salaam kesho mchana kwenda Zanzibar huku akitaja zawadi kuwa ni Sh. milioni 10 kwa mabingwa na Sh. milioni tano kwa mshindi wa pili.

IMG_0558-0.JPG



Comments