Kampuni bingwa ya kusafirisha vifurushi, City Delivery Service (CDS), imeandaa tamasha kubwa la muziki wa dansi litakalofanyika jijini Dar es Salaam mwezi ujao tarehe 25.
Tamasha hilo litakalofanyika kwenye viwanja vya TCC Chang'ombe, litashuhudia bendi nne kali zikisimama jukwaa moja na kuonyeshana ufundi, lakini kama vile hiyo haitoshi, kutakuwa pia na burudani ya muziki wa taarab.
Mratibu wa tamasha hilo, Khamis Dacota, ameiambia Saluti5 kuwa bendi zitakazotumbuiza ni FM Academia, Malaika Band, Mapacha Watatu na Msondo Ngoma Music Band.
Kwa upande wa taarab, Dacota amelitaja kundi jipya la Ogopa Kopa Classic Band chini ya Malkia Khadija Kopa, kuwa ndilo litakalosababisha buradani ya mambo ya kimwambao.
Mratibu huyo amesema tamasha hilo ni sehemu tu ya mambo kadhaa ya kiburudani, michezo na kijamii, yatakayofanywa na CDS katika mwezi huo wa Januari.
"CDS inatimiza miaka 10 tangu kuzaliwa kwake, na hivyo kampuni hiyo chini ya mkurugenzi wake Masoud Wannani (pichani juu), imeamua kufanya sherehe kubwa itakayoandamana na tamasha hilo la muziki wa dansi pamoja na mambo mengine kem kem," alisema Khamis Dacota.
Comments
Post a Comment