BARUA KWA SHEM KARENGA TOKA KWA FRED MOSHA



BARUA KWA SHEM KARENGA TOKA KWA FRED MOSHA

Mpenzi wa muziki maarufu na mtangazaji aliyebobea katika uchambuzi wa muziki wa Tanzania, kaandika barua hii kwa Shem Karenga

 hqdefault

Barua ya wazi kwa Mzee Shem Karenga

Kwako Mzee Shem Karenga

BINAFSI kama walivyo wanadamu wengine nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuondoka kwako duniani mara baada ya kupigana vita vikubwa vya kimuziki kupitia kazi zako ulizofanya katika kipindi chote cha uhai wako.

Ni masikitiko kwangu hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa umeondoka katika kipindi ambacho bado busara zako zinahitajika katika tasnia hii ya muziki hasa muziki wa dansi ambao kwa hakika kila siku iendayo kwa Mungu umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kudharauliwa kwa makusudi mazima na hao wanaoitwa wadau.

Hata hivyo sina budi kukubaliana na hali ilivyo na nitazidi kukuombea kwa Mwenyezi Mungu akupe tuzo lako unalostahili kulingana na kazi kubwa na ya kutukuka ya kutuelimisha, kutuonya na kutuburudisha sisi mashabiki wa muziki wa ndani na nje ya Tanzania.

Hata hivyo licha ya kuwa umeondoka, nitarudia tena kukuomba uifanye kazi hii ya kuwaambia magwiji wenzio waliokutangulia mazingira ya muziki wa Tanzania uliyoyaacha huku duniani, kazi ambayo pia nilimpa Kamanda Muhidin Maalim Gurumo wakati alipoondoka duniani.

Wape salamu nyingi sana magwiji hao kama akina Salum Abdallah, Mbaraka Mwinshehe, Juma Kilaza, Michael Enock, Juma Mrisho, Athuman Machapati, Athuman Muba, Athuman Tembo, mliyefanya kazi wote kuanzia enzi za Tetema Segere na hatimaye Segere Matata, Abel Baltazar, Marijani Rajabu, Wilson Peter na nduguye George Peter na hata wanamuziki vijana kwako kama TX Moshi, Nico Zengekala na magwiji wengine wengi.
Kwanza jambo la kwanza ninalokuomba Mzee Shem uwaambie magwiji hao kuwa sisi mashabiki wa muziki wa Tanzania tunawamiss sana kwa kuwa kuondoka kwao kumeacha pengo kubwa sana la muziki hapa nchini na kwamba siku hizi mambo yamebadilika sana kwenye huo muziki wa dansi hapa nchini kiasi kwamba watu na bendi siku hizi wanajiendea muzabwamuzabwa kama alivyosema Marijani Rajabu kwenye wimbo wake Dunia imani imekwisha wa mwaka 1984.

Jambo la pili ambalo binafsi ningekuomba uwaambie kuwa siku hizi muziki wa dansi wa Tanzania umepoteza uhalisia wake kiasi kwamba wanamuziki wetu wenye asili ya kitanzania wanauvaa utaifa mwingine kabisa na kusahau ngoma asilia za kitanzania zikiwemo Mkwaju Ngoma, Kisonge, Kabango, Kilua na ngoma zingine ambazo ziliupamba muziki wa kitanzania zikiwemo nyimbo zako mwenyewe.

Wape mifano ya nyimbo zako kama Dada Lemi, Asha, Mapenzi hayana mganga na Belaombwe ulizotunga kwa mitindo ya ngoma za Kisonge na Kabango za asili ya Kigoma na kupata umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania na kuitangaza Tabora Jazz kimataifa zaidi.

Waambie siku hizi wanamuziki wetu wa dansi hasa vijana wanavyouvaa ukongo kiasi kwamba wanabadili hata lafudhi za mazungumzo yao huku wengine wakijiona kuwa hawakupaswa kuwa watanzania kama tulivyo sisi ambao siku zote tunaendelea na tutaendelea kuutukuza na kuuthamini utanzania wetu kupitia fani zetu tulizonazo.

Siku hizi wanamuziki hawa wa kitanzania tulionao wanajifanya akina JB Mpiana, Werrason, Koffi Olomide, Ferre Gola, Fally Ipupa na wanamuziki wengine wa kikongo huku nyimbo zao zikiwa jukwaa la kutumiana salamu na kutajana tu majina bila sababu za msingi na kwamba hata kama wimbo una ujumbe mzuri, bado unaharibiwa na mtindo huo wa kutajana majina na kutumiana salamu kana kwamba nyimbo hizo zimekuwa vipindi vya salamu vya redio ambavyo wasikilizaji hutuma post cards ama kupiga simu na kutuma salamu.

Wape mifano na hili bila shaka hata wanamuziki wa kikongo waliokaa Tanzania na ambao wako huko na hasa Dk Remmy Ongala, magwiji wenzio wa Maquis, Fauvvette, Safari Sound na bendi zingine zilizokuja wakati huo namna zilivyopata sifa kubwa kuutukuza utanzania na kusaidia kutangaza utamaduni na ngoma za kitanzania kupitia nyimbo zao achilia mbali wao wenyewe walikuwa na asili ya Kongo.

Wape mifano ya nyimbo kama vile Athuman wa Makassy ulioimbwa kwa kiswahili, kinyakyusa na kinyamwezi, pia Mangolibo wa Maquis ulioimbwa kwa kibondei, Ntale wa OSS ulioimbwa kwa kiswahili na kinyamwezi, Mwipungu wa haohao OSS ulioimbwa kiswahili na kinyakyusa namna zilivyokuwa na mashiko licha ya kuwa asilimia tisini kama sio tisini na tano ya wanamuziki waliokuwa kwenye bendi hizi walikuwa wakongo.

Muombe Dk Remmy akusaidie kulielezea hili namna alivyopata shavu la ziara kwenye mataifa mbalimbali makubwa Barani Ulaya kupitia muziki huku akiutangaza muziki wa Tanzania kwenye matamasha makubwa na ya kimataifa, jambo ambalo halifanywi na wanamuziki wetu wa kitanzania na ambao hata wakipata nafasi ya kwenda huko Ulaya huishia kuimba tu kwenye sherehe za Birthdays na matamasha madogo sana yanayowahusu watanzania wenyewe na watu wa Afrika Mashariki.

Waambie namna akina Vumbi, Kanku Kelly na wengine ambao tunao bado huku duniani namna wanavyoitangaza Tanzania kimataifa kupitia kazi zao za muziki licha ya kuwa wao wenyewe wana asili ya hukohuko Kongo lakini wanafanya hivyo kwa mapenzi na nchi hii na kujiona kuwa ni sehemu ya maendeleo ya Tanzania.

Jambo jingine ninalokuomba uwaambie magwiji hao wenzio ni kuwa siku hizi kwa makusudi kabisa vyombo vingi vya habari kama si vyote vimeupiga teke kabisa muziki wa kitanzania tena ule muziki wa dansi halisi la nyumbani na badala yake kuupa nafasi zaidi muziki uliopewa jina la 'Bongo Flavour' wenye vionjo vya kimagharibi na ambao umebadili kabisa mitazamo na maisha ya vijana wengi na kujiona kuwa wao ni wamarekani wa Tanzania.

Waambie kuwa siku hizi tuna waandishi na watangazaji wengi wanaojitapa kuwa wanafanya vipindi vya muziki na ambao kwa hakika hawaujui kabisa muziki na badala yake wanajikita zaidi kwenye muziki wa aina moja tu, huo nilioutaja na ambao hauna historia yoyote inayoakisi Tanzania na katika hili naamini kuwa Mtangazaji mkongwe wa muziki Julius Nyaisangah atakusaidia kulieleza maana amekaa kwenye tasnia hii kwa muda mrefu huku mchango wake katika kukuza muziki wa dansi la Tanzania unajulikana na sisi wachache tuliobakia na ambao hatutaki kuyumbishwa na wimbi hilo la kupiga ama kukumbatia muziki usio asili yetu tukiendelea kupita kwenye njia zilezile ambazo Nyaisangah alipita.

Waambie siku hizi nyimbo hizo za Bongo Flavour zinapigwa kwenye vituo vya Redio na Televisheni kwa misingi ya kirafiki na kwa kiasi kikubwa rushwa inayotolewa kwa hao watangazaji na waandishi wa habari kutoka kwa wasanii hao na hivyo kulazimisha kupiga nyimbo hizo hata kama zingine zinakiuka maadili ya kitanzania kuanzia uvaaji, maudhui ya wimbo wenyewe na hata uchezaji huku siku hizi kwa wasanii wa kike kuvaa vibaya na kukata viuno tena vile vya unyagoni imeonekana kuwa fasheni na kwamba hakuna mtu anayelikemea hili huku Serikali yetu nayo ikiwa imekaa kimya kana kwamba haioni uchafu unaoendelea.

Waambie namna wanamuziki wetu wanavyokosa uzalendo wa kweli wa kuipenda nchi yao kwa kuimba masuala mbalimbali ya kimaadili na kimantiki yanayojitokeza kwenye nchi yetu na badala yake wanajikita zaidi kuimba mapenzi tena mapenzi ya ndani kabisa ya chumbani huku jamii ikionekana kufurahia nyimbo hizo chafu zenye uvundo na kama kawa hata Serikali yenyewe inalifurahia na kuwaona wanamuziki wa aina hiyo ndio wanaojua kazi kuliko wanamuziki wanaotunga nyimbo zenye kuonya, kuelimisha na kuelekeza nini kifanyike pindi inapozuka migogoro ya kibinadamu, kuanzia migogoro ya kinafsia hadi migogoro ya kijamii.

Waambie zile enzi zao za kuhamasisha uwajibikaji makazini, kukemea rushwa na ufisadi, kukemea maovu mengine ya kijamii, siku hizi hazipo tena na badala yake zipo enzi za I love you Baby, Kata viuno nifurahi, unadhani kama vile TANESCO walijua mimi ntaua, na uchafu mwingine mwingi huku vyombo vya habari vikitulazimisha tupende ujinga huo usiomithilika na hatimaye kusambaratisha kabisa maadili mazuri ya kimuziki yaliyokuwepo miaka hiyo na enzi zenu nyinyi.

Siku hizi hata kile kinachoitwa mmomonyoko wa maadili kimekuwa kikichangiwa na mambo mengi na kwa hakika muziki na nyimbo hizo za kijinga zinachangia kwa kiasi kikubwa zaidi, kiasi kwamba muziki huo unaathiri hata vijana wetu wa shule ambao nyakati za mitihani hasa ile mitihani inayoamua mustakabali wa maisha yao, vijana hao hawajibu kabisa maswali ya mitihani hiyo kiufasaha na badala yake wanaandika mistari ya Bongo Flavour, ajabu kweli.

Jambo jingine ninalokuomba Mzee wangu uwaambie magwiji wenzio huko ni namna hawa wanaoitwa wadau wa muziki ambao binafsi kwangu hawana sifa hata chembe ya kuitwa wadau, namna wanavyouporomosha kwa makusudi muziki wa dansi na badala yake kuukuza huo unaoitwaBongo Flavour.

Waambie kuwa zile enzi zenu zakujaza kumbi za starehe kama Lumumba A, Uhazili na kumbi zingine ambazo Tabora Jazz ilikuwa inapiga miaka hiyo, kuwa kwa sasa zimekwisha huku bendi nyingi zikilazimika kupiga kwa kiingilio cha kinywaji tofauti na ilivyokuwa zamani huku hao wanaoitwa wadau wakitumia nafasi zao kuukandamiza kabisa muziki wa dansi kwa kukataa tena kwa makusudi kuunga mkono muziki huo kwa madai kuwa ati umepitwa na wakati.

Ok siwalaumu sana kwa kuwa wengi wao ni vijana na hawajui namna gani muziki wa dansi ulivyobeba historia kubwa ya kupigania uhuru na kuisaidia Serikali kutekeleza sera zake na itikadi yake hasa ya Ujamaa na Kujitegemea na badala yake wameukuta tu muziki huo huku kwa makusudi kabisa wakiwa hawataki kabisa kujifunza namna muziki wa dansi ulivyo na nafasi kubwa katika kuakisi historia ya nchi kama ilivyofanyika zamani.

Wadau hao ambao wengine hata wanamiliki vyombo vya habari wamekuwa hawaupi kipaumbele muziki huu wa dansi kuanzia hata kwenye vituo vyao na hata wao wenyewe huku wakijifanya kuwa karibu na muziki huo na wanamuziki na kujifanya wanatoa maelekezo ya namna ya kuuboresha muziki ambao wao wenyewe hawaujui.

Jambo jingine ninalokuomba uwaambie ni namna wanamuziki wenzio wakongwe na ambao bado tunao huku duniani wanavyohadhirika kana kwamba dunia ya muziki wa Tanzania ikiwemo Serikali haiwaoni na imewatupa mkono licha ya kuwa wameisaidia Serikali kutunga na kuimba nyimbo ambazo kama nilivyosema zilisaidia kueneza sera na itikadi ya Serikali na kuisaidia Serikali kuhamasisha mipango yake kama vijiji vya ujamaa, kilimo cha kufa na kupona, uwajibikaji, kukemea rushwa na mambo mengine chungu mzima na kuwafanya wanamuziki kukata tamaa na kazi hiyo ama kuimba huko kwa kuzingatia hali walizonazo wazee wao hao jambo ambalo pia linachangia kupungua kwa kasi upatikanaji wa wanamuziki wa kweli.

Wape mifano ya bendi kongwe za Msondo na Sikinde ambazo zinaonekana kama vile hazipo kabisa kwenye ulimwengu huu wa muziki na badala yake hao wa kizazi kipya na bendi zisizokuwa na maadili ndizo zinazopewa nafasi kubwa siku hizi na kwamba hazijaliwi.

Mzee Shem Karenga, yako mengi ambayo binafsi nilitaka nikuambie na nikuombe uwaambie lakini kwa barua hii fupi haya yanatosha na kama kuna mengine unayoyakumbuka basi ni vizuri uwaambie magwiji wenzio ili watambue na kuona hali halisi ilivyo.

Nakuombea kwa Mungu aipokee roho yako na upumzike kwa Amani

Amina

Wasalam

Fred Mosha

 



Comments