Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Rais wa Simba SC, Evans Aveva amesema mshambuliaji Emmanuel Okwi hatapewa fungu lolote kutokana na malipo ya dola la Marekani 300,000 (Sh. milioni 509) ambazo Shir8ikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limeiamuru Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kuilipa klabu hiyo ya Msimbazi.
Baada ya Simba SC kushinda kesi, FIFA imeiamuru Etoile du Sahel kuilipa Simba SC kiasi hicho cha fedha sanjari na asilimia mbili (2%) ya usumbufu kutokana na malipo ya mauzo ya Okwi kutoka Simba SC kwenda klabu hiyo ya Tunisia.
Etoile imepewa siku 30 na FIFA kuanzia Desemba 5, mwaka huu kuhakikisha inalipa fedha hizo kwa Simba SC na Aveva amemwaga sifa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Simba SC, Ismail Aden Rage kwa kufanikisha kufikiwa kwa hatua hiyo.
Akizungumza na mtandao huu leo mchana, Aveva amesema Okwi hatapewa fungu lolote kutokana na malipo hayo kwani fedha hizo ni mali ya klabu na yeye kama mchezaji alishalipwa chake na Etoile wakati wa kusainisha mkataba.
"Fedha hizo ni mali ya Simba SC, Okwi hana chake hapo. Yeye ameshapewa fungu lake na Etoile kabla ya kusaini mkataba wa kujiunga nao," amesema Aveva.
Okwi alijiungana Etoile Januari mwaka jana akitokea Simba SC lakini aliamua kuikacha kutokana na kile kilichoelezwa kutolipwa kwa wakati, akajiunga na Yanga SC lakini wakashindana pia kwa tatizo hilo hilo kabla ya kuamua kurejea tena Simba SC.
OKWI KUOA KESHO
Katika hatua nyingine, Aveva amesema Okwi anatarajia kufunga ndoa kesho jijini Kampala, Uganda kabla ya kurejea nchini kuungana na timu katika maandalizi ya mechi zinazofuata za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
"Okwi si kwamba anaendelea na usumbufu wake, timu inaendelea na mazoezi hapa Dar es Salaam na yeye hayupo kwa sababu maalum. Kesho atafunga ndoa Kampala na badji yetu tumealikwa," amesema Aveva.
Comments
Post a Comment