TFF: HAKUNA TATIZO MCHEZAJI KUCHEZA DHIDI YA TIMU MOJA MARA TATU MSIMU MMOJA


TFF: HAKUNA TATIZO MCHEZAJI KUCHEZA DHIDI YA TIMU MOJA MARA TATU MSIMU MMOJA

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekiri kufanya makosa kuruhusu kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
VPL ilisimama kwa wiki saba Novemba 9 baada ya kuchezwa kwa mechi 49 za raundi ya kwanza hadi ya saba kupisha usajili wa dirisha dogo, mashindano ya Kombe la Uhai yanayoshirikisha Timu B za klabu za Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Chalenji.
TFF ilifungua dirisha dogo la usajili Novemba 15 na litafungwa Desemba 15 huku mechi za raundi ya nane hadi ya 13 ya mzunguko wa kwanza wa VPL bado hazijachezwa, hivyo kutoa mwanya kwa baadhi ya wachezaji watakaozihama timu zao kipindi hiki cha usajili kucheza mechi tatu dhidi ya timu moja.
bon
Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amekiri shirikisho hilo kujisahau katika suala hilo lakini akasisitiza kuwa hakuna tatizo kubwa mchezaji kucheza mechi tatu dhidi ya timu moja.
"Ilikuwa haijawahi kutokea hapa kwetu (Tanzania), tumejifunza kitu lakini mchezaji kucheza mechi tatu dhidi ya timu moja VPL haina tatizo, tatizo kubwa ni mchezaji kusajiliwa na zaidi ya timu mbili msimu mmoja. Hili linakatazwa kikanuni," amesema Mwesigwa.
Kiungo mkongwe wa Simba Amri Kiemba amejiunga na Azam FC kwa mkopo huku klabu hiyo ya Msimbazi ikiwabana wanalambalamba wasimtumie katika mechi zinazozikutanisha timu hizo mbili msimu huu.
TFF kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mshindano, Boniface Wambura imepinga vikali uamuzi huo wa Simba kwa kuwa kanuni zinamruhusu mchezaji huyo kukipiga dhidi ya timu iliyomtoa kwa mkopo kwenda timu nyingine, hata hivyo.
Mchezaji wa Ndanda FC aliyecheza dhidi ya Azam FC msimu huu, akisajiliwa Simba atacheza dhidi ya Azam mara tatu katika mechi za msimu mmoja wa ligi kuu, ikiwa ni mfano wa kilichokosewa na TFF kuruhusu dirisha dogo la usajili msimu huu lifunguliwe ilhali mechi za mzunguko wa kwanza bado hazijakamilika.



Comments