SIMBA YAMPANDIA DAU SSERUNKUMA ATUA DAR



SIMBA YAMPANDIA DAU SSERUNKUMA ATUA DAR





Licha ya Katibu Mkuu wa Klabu ya Gor Mahia, Chris Omondi jana kunukuliwa na mtandao wa futaa.com akieleza kuwa wamekata mzizi wa fitna kwa kukubaliana kumuongeza mkataba wa miaka miwili mshambuliaji wao, Dan Sserunkuma, ametua nchini jana mchana kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo na Klabu ya Simba, imefahamika.
Sserunkuma ambaye pia ni mchezaji wa kikosi cha kwanza cha timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes), jana alipelekwa moja kwa moja katika hospitali moja jijini ili kufanyiwa vipimo vya afya na baada ya hapo ndiyo aendelee na mazungumzo ya kusaini mkataba na Simba.

Chanzo cha gazeti hili kilieleza kwamba tayari Kamati ya Usajili ilishampitisha mshambualiaji huyo kinara wa mabao ya Ligi Kuu ya Kenya na kumpandia dau na kwamba vipimo alivyofanyiwa ni kutaka kuondoa hofu ya kusajili mchezaji mwenye majeraha sugu.

"Sserunkuma ametua  mchana huu (jana mchana) alipelekwa kufanyiwa vipimo ili tusirudie makosa ya huko nyuma", kilisema chanzo chetu.

Taarifa zaidi zinasema kwamba mchezaji huyo bado hawajafikia makubaliano ya fedha za usajili mpaka pale watakapopata majibu ya vipimo vya afya.

"Tukishajua hali yake kiafya kila kitu kitazungumzika, kubwa ilikuwa ni mchezaji kufika Dar es Salaam...kila upande utatoa mapendekezo na hatimaye kusaini mkataba", aliongeza.

Taarifa za awali zilieleza kuwa Sserunkuma anataka dau la Dola za Marekani 20,000 na mshahara wa Dola za Marekani 2,000 kwa mwezi.

Rais wa Simba, Evans Aveva na Katibu Mkuu, Stephen Ally, wamekataa kuthibitisha ujio wa mchezaji  huyo.

Kocha wa The Cranes, Mserbia, Sredojevic Milutin 'Micho' ni mmoja wa waliopendekeza usajili wa Sserunkuma kuhamia Simba ili kuisaidia kurejesha heshima yake katika Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
CHANZO: NIPASHE


Comments