SIMBA WAANZIA YANGA GYM CHANONGO BADO MOSHI MWEUSI



SIMBA WAANZIA YANGA GYM CHANONGO BADO MOSHI MWEUSI

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Kikosi cha Simba chini ya kocha msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola leo kimeanza mazoezi kwenye gym ya Oil Com, Kijitonyama jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya 'Nani Mtani Jembe 2′ dhidi ya Yanga itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Desemba 13.
Kikosi hicho kilipewa mapumziko ya wiki mbili baada ya kusimama kwa wiki saba kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL). Kupisha usajili wa dirisha dogo, mashindano ya Kombe la Uhai, michuano iliyobuma ya Kombe la Chalenji na mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Swaziland dhidi ya Taifa Stars.
Kikosi hicho kinachowakosa kiungo Amri Kiemba aliyetua kwa mkopo Azam FC na winga Haroun Chanongo aliyesimamishwa, kimeanza mazoezi hayo ya saa mbili kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi.
Msemaji wa Simba, Hamphrey Nyasio amesema jijini Dar es Salaam kuwa wataendelea na mazoezi ya gym kwa siku saba wakati uongozi ukiangalia sehemu nzuri ambayo timu itakwenda kuweka kambi kuandalia dozi Yanga.
Aidha, winga Chanongo amesema kuwa hajajulishwa na uongozi juu ya ratiba ya mazoezi na hajui kinachoendelea katika kikosi cha Simba.

simba

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Nyasio amesema kuwa sakata la kusimamishwa kwa Kiemba, Chanongo na Shaban Kisiga kwa sasa lipo chini ya Rais wa Simba (Evans Aveva), ambaye amepanga kukutana na vyombo vya habari kulizunguzia.
Watatu hao walisimamishwa muda mfupi baada ya kutoka sare ya bao dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya Oktoba 25 na kumriwa kurejea jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi na uongozi.
Simba iliifunga Yanga mabao 3-1 katika mechi ya kwanza ya Nani Mtani Jembe iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Desemba 21 mwaka jana, kipigo ambacho kilifukuzisha benchi lote la ufundi la Yanga lililokuwa linaoongozwa na Mholanzi Ernie Brandts na msaidizi wake Felix Minziro pamoja na aliyekuwa kocha wa makipa Mkenya Razak Ssiwa.



Comments