SIMBA WAANZA KUIWINDA YANGA NANI MTANI JEMBE 2



SIMBA WAANZA KUIWINDA YANGA NANI MTANI JEMBE 2

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
michuzi
SIMBA iliyofufua matumaini baada ya kupata ushindi wa kwanza msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), kikosi cha Simba kitaingia kambini Jumatatu Novemba 24 kujiandaa kwa mechi ya Nani Mtani Jembe 2 dhidi ya Yanga itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Desemba 13.
Simba iliyokuwa imekaa kwa miezi nane bila kupata ushindi VPL, ilipata ushindi wake wa kwanza katika mechi yao ya raundi ya saba walipoifunga Ruvu Shooting bao 1-0 na kukata kiu ya ushindi iliyokuwapo kwa siku 252.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC, Said Tully ameuambia mtandao huu jijini Dar es Salaam leo kuwa kikosi chao kitaanza mazoezi kesho Jumatatu kujiweka fiti kabla ya kukikabili kikosi cha Mbrazil Marcio Maximo.
"Kocha mkuu (Patrick Phiri) atawasili katikati ya wiki, Jumatano au Alhamisi. Timu itaanza mazoezi kesho Jumatatu ikiwa chini ya kocha msaidizi Seleman Matola," Tully amesema.
"Tutaanzia gym kabla ya kuendelea na mipango mingine. Tunatambua tutakuwa na mechi ngumu dhidi ya Yanga."
Yanga ambao wataanza mazoezi Jumatano kwenye uwanja wa shule ya sekondari Loyola, wanahitaji kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1 katika mechi ya mwaka jana ya Nani Mtani Jembe.
Tayari timu hiyo ya Jangwani imeshatangaza kuachana na mshambuliaji wake Mbrazil Geilson Santos Santana 'Jaja' na imeweka wazi kwamba nafasi ya straika huyo huenda ikachukuliwa na kiungo Mbrazil Emerson De Oliveira Neves Rouqe (24) anayetarajiwa kuwasili jijini Jumanne mchana kwa ajili ya majaribio na kufanyiwa vipimo endapo akifuzu.
Jaja amefunga goli moja tu katika mechi saba zilizopita za VPL, na amekuwa akizodolewa na mashabiki wa Yanga kwamba hastahili kucheza kwenye timu kubwa kama hiyo



Comments