Bertha Lumala na mtandao
Baraza linalosimamia Ligi Kuu ya Kenya (KPL) limetupilia mbali pendekezo lililotolewa na Shirikisho la Soka nchini humo (FKF) kuongeza idadi ya timu za ligi hiyo kutoka 16 hadi 18 msimu ujao (2015).
Katika taarifa yake iliyosainiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa KPL, Jack Oguda, msimu wa 2015 wa KPL utaendelea kuwa na timu 16 kama kama ilivyokuwa katika misimu iliyopita huku akitoa sababu za kupinga mapendekezo ya FKF kuongeza timu mbili zaidi.
HARAMBEE STARS INAHITAJI MUDA MWINGI
-Baraza linapinga KPL kuwa na timu 18 na kuthibitisha kwamba msimu wa 2015 utaendelea kuwa na timu 16 na Sababu hizo zilizowekwa kwenye mtandao wa futaa.com kama:
-Timu ya Taifa (Harambee Stars) inahitaji muda zaidi wa kucheza mechi za kimataifa za kirafiki ili kupanda katika viwango vya FIFA na hili haliwezekani kama idadi ya timu itaongezwa katika ligi na kuleta mabadiliko ya ratiba.
MAJERAHA KWA WACHEZAJI YATAONGEZEKA
-Suala la afya za wachezaji wetu limeangaliwa kwa kina na imebainika kwamba kama ligi itarefuka kwa kuwa na timu nyingi zaidi, kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza majeraha kwa wachezaji na kuna klabu chache zinazowajibika kwa kutoa bima ya afya kwa wachezaji, jambo ambalo limekuwa likiathiri utendaji wa timu ya taifa.
-2008 wakati ligi ilipolisaidia shirikisho kuiendesha Harambee Stars, timu ilifanmikiwa kuwa katika nafasi nzuri ambayo haikuwahi kutokea kwenye viwango vya FIFA ikikamata nafasi ya 68 na klabu zililazimika kutoa michango yake mwaka huo. Inashangaza kwamba hadi sasa timu ya taifa iko nafasi ya 116 ikimaanisha kwamba tunarudi nyuma kisoka.
-Majadiliano ya kuongeza muonekano wa ligi yalifanywa 2004 katika mkutano wa kamati husika ya Fifa (FIFA Normalization Committee) na Makubaliano ya Cairo, Misri (Cairo Agreements) yaliyohusisha FIFA, CAF, Serikali, klabu na shirikisho na fomula (mbinu) iliyokubaliwa ni kupunguza idadi ya timu kutoka 24 hadi 16 ili kuongeza ubora, ushindani, soko na weledi. Kiwango kimeonekana na bado tunasisitiza katika ubora na tunapinga wingi wa timu.
MICHUANO YA AFRIKA
-Kutokana na utafiti katika michuano ya CAF, nchi pekee zenye ligi zenye zaidi ya timu 16 ni Nigeria na Misri, ambazo zina idadi kubwa ya watu kuliko Kenya na zina pato kubwa (GDP) la kuziwezesha ligi zake lakini hazijafanikiwa kufuzu kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika. Ligi tajiri Afrika ni PSL yenye timu 16 kama ilivyo kwa ligi nyingi barani Afrika zilivyo na uwezo wa kuhimili kuendesha ligi za timu 16 na 14.
-Katika kuongeza idadi ya timu, washiriki watahitaji kuongeza mzigo (fedha) za uendeshaji na hii ina hatari ya kudhoofisha au wakati mwingine kuua kabisa ligi kama ilivyowahi kutokea miaka ya 2000 wakati klabu ziliposhindwa kumudu maandalizi ya mechi. Ligi imekuwa ikijaribu kwa nguvu zote kuwa na mfumo wa timu za vijana kwenda sambamba na timu kubwa, kuimarisha miundombinu, kulipa mishahara ya wachezaji, mabenchi ya ufundi, maofisa wa klabu na waamuzi lakini kutokana na uhaba wa fedha, hilo halijafanikiwa.
-KPL inaheshimu misingi ya utawala bora na itaendelea kuheshimu taratibu za FIFA, CAF, FKF na Katiba yetu. Kamati ya Utendaji ya FKF iliyokutana na kuamua kuongeza idadi ya timu ligi kuu hadi timu 18, haikwenda sanjari na matakwa ya kikatiba kulingana na wajumbe wa Daraja la Kwanza na KPL hawakualikwa katika mkutano huo kinyume cha Katiba na kwa vyovyote vile maamuzi yaliyochukuliwa yalikuwa kinyume cha sheria na Katiba ya FKF yenyewe.
SUPERSPORT YAGOMEA
-Kumeibuka mvutano kati ya FKF, KPL na Supersport kuhusu kuongezwa kwa idadi ya timu ligi kuu, huku KPL na SuperSport wanaodhamini ligi hiyo wakipinga maamuzi hayo.
Ikumbukwe kuwa siku chache baada ya FKF kutoa pendekezo hilo, mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC na AFC Leopards ya Ligi Kuu ya Kenya, Boniface Ambani alipinga vikali maamuzi hayo na kuyaita 'maamuzi yaliyokosa weledi, uadilifu na yaliyojaa rushwa'.
Comments
Post a Comment