BAADA ya kuonekana kama kutulia kwa malumbano baina ya Rais wa          Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na wakili na mdau mkubwa wa          soka nchini, Damas Ndumbaro, aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba,          Ismail Aden Rage amelichochea tena suala hilo, safari hii          bungeni akihoji ukubwa wa makato na uhalali wa mgawo unaokwenda          kwenye mfuko wa Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA).
          Siku chake kabla ya kupigwa kwa mechi ya kwanza ya watani wa          jadi nchini, Simba na Yanga msimu huu, TFF ilitangaza kuanzisha          mfuko mpya 'Jichangie' kwa lengo la kusaka fedha kwa ajili ya          maendeleo ya soka la vijana nchini ukitaka kukata asilimia tano          ya fedha za udhamini wa klabu kutoka Kampuni ya Huduma za          Mawasiliano ya Vodacom Tanzania na Kampuni ya Azam Media          iliyonunua haki za matangazo ya televisheni ya mechi za Ligi          Kuu.
          Uamuzi huo ulipingwa vikali na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom          Tanzania Bara (VPL) kupitia wakili Ndumbaro ambaye ni daktari wa          sheria. Malumbano ambayo baadaye yalisababisha TFF imfungie kwa          miaka saba kujihusisha na shughuli za soka ndani na nje ya          mipaka ya Tanzania.
          Huku hali ikionekana kutulia baada ya malumbano ya takriban          miezi miwili, Rage analiibua suala hilo, tena akiwa ndani ya          mjengo (bungeni) mjini Dodoma, ukumbi ambao umejaa watu wenye          taaluma mbalimbali na wengi wao wakiwa ni wanasiasa.
          Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alisimama          bungeni mjini humo Ijumaa ya wiki juzi na kutaka kama serikali          ina habari ya makato ambayo klabu zinakatwa ni makubwa.
          Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na          Michezo, Juma Nkamia alisema DRFA kinanufaika kwa kupata fedha          nyingi za makato ya mapato ya milangoni katika VPL bila kuwa na          kazi yoyote.
          Nkamia alisema DRFA wanapata fedha nyingi za mapato ya milangoni          ambazo hazijulikani zinakokwenda wala kazi ambayo zinafanyia.
          "Lazima tuchukue hatua," Nkamia alisema huku akikiri makato          yanayokatwa kwa klabu ni makubwa na kueleza kuwa awali alikutana          na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), TFF na wadau wengine wa soka nchini          kuangalia namna makato hayo yatakavyopungua.
          "DRFA katika mechi moja wanapata mgawo mara mbili kwenye ile          fomu ya mgawanyo wa mapato… na hawana kazi yoyote wanayoifanya          zaidi ya kusubiri mapato.
          "Sasa timu za vijana wanaohangaika ni TFF na serikali… lakini          mapato yale yanayokatwa na makubwa kupita kiasi. Tumezungumza          nao kuona njia za kuyapunguza.
          "Leo ni timu kubwa mbili tu ndiyo zinaweza kuingiza mapato          mengi… ni Yanga na Simba , Yanga ikicheza na Ndanda inaingiza          mapato mengi sana kuliko Ndanda ikicheza na Stand United lakini          makato bado ni yale yale."
          Makato ya ajabu ajabu, yasiyo na msingi na mengine mengi          yanayofanana, ambayo yanabadilishwa-badilishwa majina tu licha          ya kubeba maana moja, yameendelea kuzikamua hadi tone la mwisho          klabu za Ligi Kuu katika kampeni "nzito" ambayo binafsi ninaona          imedhamiria kuhakikisha haziendelei.
          Mathalani, katika mechi iliyopita ya watani wa jadi, Simba na          Yanga iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam          Oktoba 18, zilipatikana Sh. milioni 427 lakini zaidi ya Sh.          milioni 49 zilikatwa kinyonyaji na TFF kwenda mfuko mpya wa          'Jichangie' jambo ambalo linapingwa vikali na Ndumbaro ambaye          kabla ya kutupwa jela ya soka, alikuwa mjumbe wa TPLB.
          Katika mfuko huo mpya unaoonekana kumuumiza kichwa Rage, TFF          ililamba Sh. milioni 24.77, Yanga walipata Sh. 17,339,700 na          DRFA Sh. 7,431,300.
          Mgawo mwingine wa mapato hayo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa          na TFF, ni Sh. milioni 43.67 ya uwanja, gharama za mchezo Sh.          milioni 24.75, Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) Sh. milioni 23.29, TFF          (ikapata mgawo mwingine) Sh. milioni 17.47, DRFA (nao wakalamba          pesa nyingine) Sh. milioni 10.19, timu mwenyeji, Yanga (ikapata          mgawo wa pili) Sh. milioni 100.46, timu ngeni, Simba ilipata Sh.          milioni 71.34, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) Sh. 65,176,932          wakati Sh. milioni 21.36 ilichukuliwa na CRDB kama asilimia tano          ya gharama za tiketi.
          Mambo ya msingi ya kujiuliza hapa ni vipi DRFA itengenezewe          mwanya wa kupata mapato mengi kuliko klabu ilhali haina shughuli          yoyote ya maana inayoifanya zaidi ya kusubiri mapato ya          milangoni kama ilivyoelezwa na Nkamia? TFF wana maslahi yepi na          chama hiki?
          
          Shirikisho linaonekana kuiweka kando Ilani ya Uchaguzi ya Rais          wake wa sasa Jamal Malinzi iliyosisitiza kutetea mapato ya klabu          na sasa imeyarudisha makato ya kinyonyaji ambayo kwenye Uwanja          wa Taifa yalikuwa 17 kabla ya kufutwa na aliyekuwa Naibu Waziri          wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala.
          Makala, sasa Naibu Waziri wa Maji, alilazimika kutoa tamko la          kuyafuta makato hayo Januari 22, mwaka jana baada ya NIPASHE          kuchapisha ripoti iliyofichua 'uozo' uliokuwa ukifanywa na          baadhi ya watendaji wa TFF kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa          wa serikali huku baadhi yao wakijiita Wachina na kulamba Sh.          milioni mbili kwa kila mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa.
          Makato hayo yalikuwa: Maandalizi ya uwanja (pitch preparation),          Uwanja (asimilia 10 sasa 15%), Usafi na ulinzi wa uwanja, Ulinzi          wa mechi, Gharama za mchezo, Umeme (Sh. 300,000 kwa kila mechi          U/Taifa), Wachina (stadium technical support) Sh. 2,000,000,          Tiketi, Posho ya msimamizi wa kituo Sh. 120,000, Kamishna wa          mechi Sh. 250,000, Waamuzi Sh. 440,000, Mwamuzi wa akiba,          70,000, Mtathimini wa waamuzi Sh. 254,000 (ilivyokuwa msimu          uliopita), Kamati ya Ligi, FDF, DRFA na VAT.
          Licha ya juhudi za wizara yenye dhamana ya michezo nchini          kupunguza makato, vilio vimekuwa vikubwa sasa kwa sababu ni          makato mengi mno yanayoua timu zetu changa ambazo zinahitaji          sapoti ya serikali na TFF lakini suala hili linaonekana kufanywa          kinyume na watendaji wa sasa wa shirikisho.
          Miongoni mwa makato yanayochefua ni mgawo wa vyama vya soka vya          mikoa husika hasa, DRFA ambao binafsi sijaona kitu cha maana          kilichofanywa na chama hicho. Ninakumbuka baada ya gazeti hili          kuhoji juu ya uhalali wa makato 17 ya kinyonyaji Uwanja wa          Taifa, DRFA walionekana kushtuka na kuanda semina ya makocha          jijini Dar es Salaam.
          Makato wanayopewa DRFA ni ya nini na yanakwenda kufanyia kazi          gani ikiwa kwa sasa vyama vya soka vya wilaya za Dar es Salaam          (Kifa – Kinondoni, Tefa – Temeke na IDFA – Ilala) vyote          vimeshapewa hadhi ya mikoa na vinaendesha ligi zao? Hiki ndicho          Rage na wadau wa soka nchini wanataka wafafanuliwe kwa kina.
          Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema mwaka juzi kuwa          makato hayo yanawaumiza na kuwakwaza kiuchumi, hivyo akazitaka          klabu kuungana ili kulipatia ufumbuzi suala hilo ambalo limekuwa          tatizo kubwa kwa maendeleo ya klabu za soka nchini.
          Naye Meneja wa Azam FC, Patrick Kahemele alizigeukia klabu kuwa          zenyewe ndizo zinapaswa kujilaumu kwa kuipa madaraka makubwa TFF          katika kupanga gharama za tiketi, kiingilio na makato mengine ya          gharama za mechi husika, hali ambayo mwishowe huwaacha          wakiambulia fedha kidogo mno kutokana na mapato ya milangoni.
          "Haya yote yanatokea kwa sababu mwanzo wetu haukuwa mzuri. Klabu          hazina umoja. Kama tungeungana katika hili, kusingekuwa na          malalamiko," alisema Kahemele.
          Aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema shirikisho          linalazimika kutoa fedha Sh. 200,000 kwa kila mechi inayochezwa          kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mafuta ya magari ya polisi.
          Simba na Yanga ziliwahi kutishia kutocheza tena kwenye Uwanja wa          Taifa kuepuka makato makubwa misimu kadhaa iliyopita na serikali          iliwapoza kwa kuahidi kushughulikia suala hilo.
          Hata hivyo, inaonekana hakuna juhudi za kulishughulikia suala          hilo hivi karibuni, huku TFF ikianzisha makato mapya ya          kinyonyaji baada ya serikali kuyafuta yaliyokuwa yanaihusu.
          Katika ukokotozi wake, Ndumbaro alisema kama utaratibu wa          ukataji makato ya milango utaendelea kama ulivyopangwa na Kamati          ya Mashindano ya TFF kwa kurudisha makato ya kinyonyaji, DRFA          itakuwa inalamba fedha nyingi kuliko klabu za VPL kwa msimu.
          Ikumbukwe kuwa marekebisho ya Kanuni za Ligi za TFF toleo la          2014 yaliyosababisha kuongezwa kwa mfuko mpya wa 'Jichangie'          yamefanywa na Kamati ya Mashindano badala ya Kamati ya Sheria na          Hadhi za Wachezaji ya TFF, kinyume cha taratibu na Katiba ya          shirikisho hilo, hii ikiwa ni kwa mujibu wa Ndumbaro.
          CHANZO: GAZETI LA NIPASHE Novemba 24, 2014
Comments
Post a Comment