Kuelekea mchezo muhimu na mgumu wa kundi E wa ligi ya mabingwa ulaya (UEFA Champions League) baina ya Manchester City na Bayern Munich ya Ujerumani utakaopigwa katika dimba la Etihad, jijini Manchetser leo, kiungo wa timu hiyo Mfaransa Samir Nasri ameonya kuwa endapo watapoteza kuna uwezekano baadhi ya nyota wakaondolewa katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu
Klabu ya Manchester City inashikilia mkia katika kundi hilo lenye timu za AS Roma na CSKA Moscow ambazo pia zinaumana siku ya leo. City wana alama mbili tu katika mechi nnee walizocheza mpaka sasa na ni wazi watakuwa wameondolewa katika kinyang'anyiro hich endapo watashindwa kuifunga Munich leo huku moja kati ya CSKA au Roma ikishinda.
Mchezaji huyo mwenye miaka 27, alibainisha kuwa: "Tunahitaji kufanya kila linalowezekana tufuzu, vinginevyo mwaka ujao ni wazi kutakuwa na nyota wapya na mabadiliko makubwa katika klabu hii." Kihistoria Manchester city haijawahi kuvuka hatua ya 16 bora ya michuano hiyo na endapo watatolewa itakuwa ni mara ya tatu katika kipindi cha misimu minne.
Ikiwa chini ya kocha kutoka chini, Chile, Manuel Pellegrini, walau klabu hiyo iliambulia kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza msimu uliopita. Nasri aliwaambia waandishi wa habari.
"KiukwelI, ukiangalia viwango vya mishahara na viwango vya nyota husika kuwa 90% ya kiwango cha dunia, halafu timu ishindwe kufuzu hatua hii ya makundi ni pigo kubwa na klabu nasi sote."
Kitakwimu tangu walipochukua klabu hiyo mwezi Agosti, 2008, wamiliki wa klabu hiyo Sheikh Mansour Bin Zayed al-Nahyan na familia ya kitawala kutoka Abu Dhabi wametumia takribani £1billion kufanya usajili wa nyota mbalimbali.
Kwa upande mwingine, Kiungo wa miamba ya Ujerumani, Munchen aliye katika fomu, Mhispania Xabi Alonso amedai kuwa mwenendo wa Manchester City ulaya unadhihrisha kuwa wakati mwingine matumizi makubwa ya pesa sio kila kitu katika upatikanaji wa mataji. Alisema, "Hakuna uhakika kuwa utafanikiwa kwa matumizi, mchezo wa mpira wa miguu siyo hisabati".
Hata hivyo kiungo huyo amedokeza kuwa ukiwatizama City ni wazi muda wao wa kufanya vizuri ulaya hauko mbali pamoja na kuwa kila msimu unaweza ukadhani wanafuzu na wasifanye vizuri.
City imekuwa na mwenendo mbovu ulaya, msimu ulopita (2013-2014) ilikomea hatua ya mtoano ya 16 baada ya kufungwa na Barcelona, msimu wa 2012-2013 walikomea hatua ya makundi, 2011-2012 walimaliza nafasi ya tatu na hivyo kuangukia michuano ya Europa ambako pia hawakufanya vizuri baada ya kukomea hatua ya 16 bora, hali kama hiyo pia ilikuwepo msimu mmoja kabla (2010-2011). Ikumbukwe msimu mmoja kabla hawakufuzu kabisa kwa michuano ya ulaya (2009-2010).
Mpaka sasa msimu huu Man City wametoa sare mbili, moja nyumbani dhidi ya Roma na nyingine ugenini Urusi walipoifuata CSKA Moscow mapema mwezi huu, City pia wakipoteza michezo miwili katika kundi hilo.
Mlinzi wa klabu hiyo kutoka Argentina Martin Demichelis amesema mwenendo wa timu hiyo unawavunja moyo wachezaji wa timu hiyo. Akasema: "Hatufurahishwi na hali hii kwani tuna timu nzuri na hivyo tunapaswa kufanya vizuri zaidi. Katika mchezo wa leo klabu hiyo itawakosa baadhi ya nyota wake muhimu wakiwemo Yaya Toure na Fernandinho wenye kutumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Comments
Post a Comment