MUELEKEO WA LIVERPOOL: BRENDAN RODGERS ALIPOTUNGA MTIHANI WENYE WASAHIHISHAJI WENGINE




MUELEKEO WA LIVERPOOL: BRENDAN RODGERS ALIPOTUNGA MTIHANI WENYE WASAHIHISHAJI WENGINE

rogers

You'll Never Walk Alone, moja ya nyimbo maarufu kabisa katika viwanja vya soka. Nyimbo ambayo pengine inaimbwa na vilabu zaidi ya vitatu duniani lakini hapana shaka ikisikika tu watu hutambua Liverpool wapo uwanjani. Ni nyimbo ambayo maneno yake hukupa imani ya kuvuka mto kwa miguu. Hii uwaleta walevi na wale wasio mahala pamoja, wakorofi na wastaarabu sehemu moja na washika dini kwa wapagani sehemu moja. Ikiimbwa hii kila mmoja uelewa jambo moja tu, Liverpool. Ni nyimbo hii ambayo Simao Sabrosa alibaki akishangaa na asiamini kama timu aloifunga ilikuwa inashangiliwa kuliko yake iliyoshinda, ni sababu hii ambayo Thiery Henry aliwahi kukiri Anfield ni sehemu ambayo yeye hupenda kucheza. Naamini hata Gerrard ni nyimbo hii ndio inampa sababu kadhaa za kuendelea kuwa pale. Lakini Kuna tofauti moja kubwa katika hii nyimbo nayo ni wakati. Wakati umepita sasa na nyimbo inaimbwa vile vile lakini katika maadhi tofauti. Namna mbili tofauti, wakati kipindi Mike Tyson akiwa ananyanyasa ulingoni na Liverpool ilikuwa moja ya timu ambazo usingejiuliza Mara mbili katika timu mbili bora zaidi Uingereza, wakiwa na ugonjwa wao usiokoma(ukame wa ligi kuu Uingereza) bado walibaki timu iliyotoa mwanga katika upande wa pili(makombe mengine). Walau nyimbo ya YNWA ilikuwa sahihi Sana kutumika, ilitumika kwa ufasaha. Kila siku ungewaza Kuna anga la Dhahabu mbele Yao, walikuwa na upande wa kujipigia kifua kule Ligi ya mabingwa Ulaya.

Umeiona Liverpool ya sasa? Umeitizama inavyocheza? Unamjua mchezaji wao bora mpaka sasa? Mechi bora walioicheza mpaka Leo ni mechi ya kirafiki dhidi ya Borrusia Dortmund. Kama Kuna msimu ambao ile nyimbo Yao ilitendewa haki basi ni msimu ulioisha, na kama Kuna msimu ambao ile nyimbo ilitakiwa kuimbwa kwa nguvu zaidi basi ni msimu huu. Kuna wakati inakupasa kujiuliza, tatizo ni nini. Je ni wachezaji wapya? Je ni Suarez kuondoka? Ama ni Sturridge? Wengi watasema Suarez lakini Liverpool walijua fika huyu bwana angeondoka, inaweza kuwa shida Sana lakini bado napata wasiwasi. Ukiitazama Liverpool ya sasa unapata zaidi ya maswali 10 kwa wakati mmoja. Lakini maswali yote kwa wale wasiopenda shida anaweza kukujibu kwa namna moja tu, MTIZAME KOCHA. Hata Mimi nimewaza hivyo pia acha nimtizame Brendan Rodgers. Najaribu kujiuliza je ni huyuhuyu aloitengeneza Liverpool iliyokuwa inamaliza michezo yake katika kipindi cha kwanza? Ni huyu alokosa ubingwa kutokana na kuteleza kwa kipenzi cha washabikibwa Liverpool? Kwa kuwa yupo mbali ikabidi nitizame mwenendo wake ili nijipe Majibu sahihi mwenyewe.

Kama Kuna meneja ambaye aliingia msimu mpya akiwa na Imani kubwa basi hapana shaka jina la Brendan Rodgers litakuwa miongoni mwa wale waliokuwa wanaongoza hiyo orodha. Huitaji akili nyingi kujua hili. Brendan aliamini ametengeneza filosofia ambayo iliwatesa na ingeendelea kuwatesa wapinzani. Ni filosofia ambayo wachache ufanikiwa nayo haswa kama Una mchezaji mwenye jina kubwa klabuni. Brendan Rodgers aliamini ametengeneza "free flowing team" yaani timu yenye mtirirko huru na ndio maana si ajabu kuona kuwa alikuwa na washambuliaji waliofunga magoli mengi zaidi na akawa na beki aliyefunga goli nyingi zaidi. Kwake jukumu la mchezaji la awali lilikuwa ushambuliaji na sio uzuiaji na ndio maana Sio ajabu kuona mchezaji aliyekuwa anatumika kama kiungo wa Ulinzi kuongoza orodha ya waliosaidia upatikanaji wa magoli mengi katika ligi. Hapa Rodgers aliamini kaweza, hata Mimi niliamini hivyo, hapana shaka hata wewe msomaji pia. Ungempinga vipi wakati ameshakuonyesha uwanjani? Kama Kuna vitu Liverpool walishavijua vinakuja basi ni suala la Luis Suarez kuondoka. Hapa ndipo hesabu za Rodgers katika wepesi zaidi zilipoanzia. Katika kalamu na karatasi yake alijiuliza kilichowanyima ubingwa msimu uliopita, Jibu akapata jepesi kabisa na haraka, ilikuwa safu yake ya ulinzi. Kisha akatizama timu yake ilifunga magoli mangapi akagundua kuwa kama angeondoa magoli ya Suarez Liverpool bado ilikuwa inasalia kuwa timu ya pili nyuma ya Man City kwa magoli mengi. Hapa ndipo maamuzi yake SAHIHI yalipokuja. Mtu wa muhimu kabisa wa kuziba pengo la Suarez alitakiwa kwanza atoke katika safu ya Ulinzi, Kisha alihitaji mtu wa ushambuliaji ambaye angeweza kumpatia magoli walau 16/18 maana yake anagalu nusu ya alofunga Suarez. Hapa ndipo mawazo ya aina ya kina Falcao yakapotea, aliamini aina hii ingetaka itizamwe yenyewe kabla ya timu jambo ambalo lingeharibu utaratibu. Na katika ulinzi apunguze magoli ya kufungwa walau kwa nusu yabaki 25 kutoka 50. Hapa Liverpool ingefunga magoli machache kuliko msimu uliopita lakini wangekuwa na wastani mzuri wa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa kuliko msimu uliopita. Hapa ndipo Rodgers alipofungia mahesabu na kuamini kuwa ameandaa mtihani mpya ambao wapinzani ungewatoa jasho. Pamoja na kwamba wasahishaji wangekuwa hao hao ila kuyajua Majibu yake ingekuwa ngumu Sana. Hapa akafungua pochi akaelekeza nguvu katika maeneo yenye shida zaidi, ulinzi na kiungo basi akaitafuta fukwe ya Miami ilipo huki taratibu akisubiri kuamua Kati ya Balloteli na Remy nani aingie. Bahati mbaya alisahau vitu 3 vya msingi. Tatizo kubwa la ulinzi lilikuwa kiungo mkabaji wa asili( Heshima kwa Gerrard ndio dhambi pengine inayomtafuna), Kiwango na matumizi ya Henderson(huyu ndio alikuwa nguzo ya Liverpool) pia hakukumbuka Afya ya Sturridge. Hapa ndipo mtihani wake ulipovuja, hapa ndipo kila meneja amepata Majibu, bahati mbaya hakuna muda wa kutunga mwingine, na hii ndio adhabu ya kalamu yake mwenyewe.

Unamfahamu Napoleon Bonaparte moja ya viongozi wenye roho ngumu na ya kigaidi kuwahi kuiongoza Ufaransa. Aliwahi kusema " Dini ndio sababu inayowafanya masikini wasiue matajiri" hapa ndipo mashabiki wa Liverpool walipo. Wanaishi katika dini yenye imani kali, wameishi wakiamini Kuwa Huwezi Kutembea Peke Yako, ukiharibu tumeharibu wote. Nyimbo ya YNWA ni msingi mkubwa unaowaongoza, bahati mbaya mdomo unaimba lakini rohoni wengi wanatamani kumuazima Roman Abramovich utendaji. Usahihi wa hii nyimbo sio wakati huu, sio wakati ambao Liverpool inafungwa mechi tano mfululizo. Usahihi wake ni kama msimu uliopita unaimba ukiamini ukifungwa Leo utafurahi katika mechi 7 au 8 zijazo. Hata Bob Peasley na Bill Shankly makocha waliotengenezewa sanamu katika malango ya uwanja waliweka utaratibu huu. Brendan Rodgers anaishi katika kivuli hiki, dini hii ina utaratibu unaomlinda. Utaanzaje kwenda na bango la Brendan Out wakati kabla na baada ya mechi unaimba You'll Never Walk Alone.( hutokaa utembee mwenyewe). Lakini kila nikitizama mwenendo wa Liverpool sidhani kama yupo salama Sana. Wale wamiliki akina Henry ndio watu pekee ambao hawaishi katika hii dini, wao wanaamini katika michezo mingine kabisa. Ningekuwa na uwezo ningemtumia Brendan ujumbe mfupi tu, "UNAIJUA DINI YA HENRY. Najua jambo la kwanza angekumbuka King Kenny Dalglish. Muda unaenda na usalama wa Brendan upo katika mikono miwili tu. Ya kwake mwenyewe na ya wapinzani. Hata hivyo mwandishi maarufu Maggie Ghallager aliwahi kusema hakuna kazi ngumu kama ya kuwa mwalimu mzuri. Hata Nyerere hakufanikiwa hapa ndio maana wapo wanaompinga hadharani. Hata Brendan yupo hapa ndio maana naweza kuyatabiri maamuzi ya John Henry, naamini hata wewe ushayajua. Tatizo la Brendan ni moja tu mpaka sasa mtihani alotunga ulivujia kwa wasahihishaji wengine. Sioni Liverpool ikibadilika karibuni kabla ya kocha hajabadilika.
Ahsanteni
By Nicasius Coutinho Suso



Comments