Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
KLABU ya Soka la Mbeya City imetoa onyo kwa klabu kongwe nchini, Simba na Yanga kuacha kufanya mazungumzo na kiungo wake fundi Steven Mazanda kwa kuwa nyota huyo bado ana mkataba na klabu hiyo pendwa jijini Mbeya.
Mazanda, aliyeonesha maajabu msimu uliopita akiiongoza timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), yuko jijini Dar es Salaam huku ikiripotiwa na vyombo vya habari nchini kuwa amekuja kufanya mazungumzo ya kusajiliwa na moja kati ya klabu hizo kongwe nchini.
Msemaji wa Mbeya City, Dismas Ten ameuambia mtandao huu leo kuwa wamepata taarifa kupitia vyo,bo vya habari kwamba kiungo wao tegemeo Mazanda yuko Dar es Salaam na anafanya mazungumzo ya kusajili wa watani wa jadi Simba na Yanga.
Ten amewataka viongozi wa timu hizo mbili kufuata taratibu za usajili kwa kuwa Mazanda ni mchezaji halali wa Mbeya City na bado ana mkataba naye.
"Taratibu za usajili ziko wazi, klabu hairuhusiwi kuzungumza na mchezaji ambaye mkataba wake na klabu anayoichezea haujamalizika au kubakisha muda usiopungua miezi sita," Teni amesema.
"Mazanda bado ana mkataba na timu yetu (Mbeya City). Tumesikia yuko huko (Dar es Salaam) lakini haishangazi kwa sababu hiki ni kipindi cha mapumziko. Kilichotushangaza ni kusikia kwenye vyombo vya habari anafanya mazungumzo ya kusajili na Simba na Yanga.
"Taratibu za soka zitaamua kama suala hilo ni kweli linafanyika kwa sasa."
Aidha, Ten ameendelea kusisitiza kuwa mkanganyiko uliojitokeza kuhusu kujiuzulu kwa kocha wao, Juma Mwambusi, litatolewa ufafanuzi na uongozi wiki ijayo.
Jumamosi ya wiki iliyopita, Mwambusi aliyeibuka kocha bora wa VPL msimu uliopita, alitangaza rasmi kubwaga manyanga kuinoa timu hiyo kwa madai kuwa amechoshwa kutupiwa lawama kutokana na matokeo mabaya ya Mbeya City FC msimu huu ilhali uongozi unajua fika kinachoigharimu timu hiyo kwa sasa.
Mbeya City iko mkiani mwa msimamo wa VPL baada ya kupoteza mechi zote nne zilizopita. Ina pointi tano baada ya kushinda mechi moja dhidi ya mabingwa wa 1988 wa Tanzania Bara, Coastal Union, suluhu dhidi ya JKT Ruvu na Ruvu Shooting kabla ya kupigwa 1-0 na mabingwa watetezi Azam FC, 2-0 dhidi ya mabingwa wa 1999 na 2000, Mtibwa Sugar, 2-1 dhidi ya Mgambo Shooting na 1-0 dhidi ya Stand United.
Comments
Post a Comment