MBEYA CITY: MWAMBUSI BADO KOCHA WETU



MBEYA CITY: MWAMBUSI BADO KOCHA WETU

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Licha ya Kocha Juma Mwambusi kutangaza rasmi kuachia ngazi kuinoa Mbeya City, uongozi wa timu hiyo pendwa mkoani Mbeya umesema bado unamtambua kocha huyo bora msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kama kocha wake halali, mtandao rasmi wa klabu hiyo umeeleza.
Jumamosi iliyopita Mwambusi alitangaza kuachana na timu hiyo iliyouanza vibaya msimu huu wa VPL kwa kupoteza mechi nne mfululizo za mwisho na kuwa mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo mpaka sasa.
Mwambusi alisema kuwa amechoka kulaumika ilhali viongozi wanajua kinachoitafuna timu hiyo msimu huu.

MBEYA CITY
TAARIFA YA MTANDAO RASMI WA MBEUA CITY INASOMEKA KAMA IFUATAVYO:-

"Uongozi wa Halmashauri ya jiji la Mbeya unapenda kuwaarifu mashabiki na wadau wa Timu ya Mbeya City Fc kuwa suala lililojitokeza wiki iliyopita kuhusiana na kocha mkuu wa timu hii Juma Mwambusi kujiuzulu, litatolewa maelezo na ufafanuzi wiki ijayo.

Hivyo basi mashabiki na wadau wa timu ya Mbeya City Fc mnaombwa kutulia mpaka ufafanuzi au taarifa rasmi juu ya jambo hili itakapotolewa, pia mashabiki mnaombwa kuwa makini na baadhi ya watu ambao wanataka kutumia mwanya huu kuzusha chokochoko nyingi kwa lengo la kuleta mgawanyiko na kuvuruga umoja wetu.

Kwa sasa Juma Mwambusi bado ni mwalimu wa Mbeya City Football Club."



Comments