Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
BAADA ya mapumziko ya wiki mbili, Kocha wa Yanga, Marcio Maximo anatarajiwa kurejea nchini Jumatano akiwa na Wabrazil wenzake; msaidizi wake Leonado Neiva, viungo Andrey Coutinho na Emerson De Oliveira Neves Rouqe anayekuja kufanya majaribio.
Timu ya Yanga baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting katika mechi iliyofinyangwa na maamuzi mabovu ya refa Ngole Mwangole kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ilikwenda mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuanza kuipashia Simba kwa ajili ya mechi yao ya 'Nani Mtani Jembe 2′.
Yanga iliyo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), itaanza mazoezi kwenye uwanja wa shule ya sekondari Loyola jijini Dar es Salaam Jumatano kujiandaa kwa mechi ya 'Nani Mtani Jembe 2′ dhidi ya Simba itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Desemba 13.
Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu amesema jijini leo kuwa Maximo na nyota hao watatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Jumatano, tayari kuanza kwa maandalizi ya mechi hiyo dhidi ya Simba pamoja na mechi zinazofuata za VPL, wakiwa na mechi ngumu ya raundi ya nane dhidi ya Azam FC Desemba 28.
"Timu inaanza mazoezi siku ya Jumatano, kocha pamoja na nyota wetu kutoka Brazil watawasili pia siku hiyo. 'Coach' (Maximo) atakapowasili ndiyo ataamua kama kuna umuhimu wa kuweka kambi na ni wapi kambi iwekwe," amesema Njovu.
Emerson anakuja kufanya majaribio Yanga baada ya timu hiyo ya Jangwani kuthibitisha mwishoni mwa wiki kuachana na mshambuliaji wake Mbrazil Geilson Santos Santana 'Jaja'.
Licha ya kufunga magoli mawili mazuri katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Azam FC katika mechi ya Ngao ya Jamii msimu huu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Septemba 14, Jaja amekuwa na wakati mgumu kikosini Yanga baada ya kuwa butu VPL akifunga goli moja tu katika mechi saba za mwanzo.
Aidha, wakati mazoezi ya uwanjani yakianza Jumatano, Njovu ameweka wazi kwamba wachezaji wao wameanza mazoezi ya gym leo jijini Dar es Salaam chini ya kocha msaidizi Shadrack Nsajigwa 'Fuso'.
Comments
Post a Comment