Ligi kuu ya England itaendelea tena wikiendi hii kwa michezo saba kupigwa siku ya Jumamosi na mingine miwili siku ya Jumapili. Vinara wa ligi hiyo 'wasioshindika' Chelsea watacheza na West Brom katika mchezo wa 12, ' The Blues' watakuwa Stamford Bridge na wanapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo. Kikosi cha Jose Mourinho kipo kileleni kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya timu ya Southampton. Chelsea wamekusanya pointi 29 wakati ' The Saints' wakiwa na pointi 25 katika nafasi ya pili.
Southampton watacheza ugenini Villa Park dhidi ya Aston Villa katika ' football Monday Night' wataendelea kubaki katika nafasi hiyo kwa sababu timu inayowafuata Manchester City haitakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 25 hata kama watashinda. Mabingwa hao watetezi, City wamekuwa na matokeo ya ' kupanda na kushuka' msimu huu, walipoteza mchez muhimu nyumbani dhidi ya Warusi, CSKA Moscow katika ligi ya mabingwa, na walilazimika kupambana ili kupata sare ya mabao 2-2 na QPR katika dimba la Loftus Road.
Newcastle ambao wameshinda michezo sita mfululizo watakuwa nyumbani kucheza na QPR katika uwanja wa St.James Park. Mchezo mwingine ni ule wa Stoke City dhidi ya timu ya mwisho, Burnely. Mchezo mkubwa zaidi ni ule wa Arsenal dhidi ya Manchester United,
Kuna wakati Patrice Evra aliwahi kusema kuwa mechi kati ya Manchester United v Arsenal huwakutanisha ' Wanaume' na ' Wavulana'. Evra alikuwa akiwadhiaki wachezaji wa Arsenal na kuwafananisha na rika la vijana ambao wanasafa kusaka mafanikio dhidi ya wanaume waliokomaa. Kikosi cha Arsene Wenger kimekuwa dhaifu mno dhidi ya United.
Kupoteza michezo saba kati ya 10 ya mwisho ni jambo ambalo linawapa ' unyonge' Arsenal ambao wameshinda mara moja. Wakati, Aaron Ramsey alipofunga bao pekee katika uwanja wa Emirates, April, 2011 na kuipa timu yake ushindi wa bao 1-0, mashabiki wa United walisikika wakiimba na kumshangilia Ramsey huku wakisema ni kijana wao! na hawakuumizwa kupoteza mechi kwa bao la kiungo huyo wa Wales ambaye aliitosa United na kuamua kujiunga na Arsenal wakati akitokea klabu ya Cardiff City, 2007.
Wenger alikosa dawa ya kumdhibiti, Sir Alex Ferguson na pia alishindwa kuifunga United ya David Moyes ambayo ilifungwa na timu zote zilizomaliza katika nafasi sita za juu msimu uliopita. Arsenal ikiwa kileleni mwa msimamo ililazishwa suluhu-tasa katika uwanja wa Emirates na kikosi kilichokuwa kimepoteza uelekeo. United waliishinda, Arsenal katika mchezo wa kwanza kwa mabao 2-1 katika uwanja wa Old Trafford. Wayne Rooney atakuwa akicheza kwa mara ya 31 dhidi ya Arsenal na nahodha huyo wa United anaweza kuvunja rekodi ya mshambulizi wa zamani wa Liverpool, Robbie Fowler kama mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi dhidi ya Arsenal.
Rooney tayari amefunga mabao 11 katika michezo 30 aliyocheza dhidi ya kikosi cha Wenger. Louis Van Gaal, kocha wa United amesema Rooney ataendelea kufunga mabao. Nahodha huyo wa England amefunga mabao saba katika michezo saba akiwa na ' The Three Lions', Rooney-mchezaji kijana zaidi kucheza michezo 100 akiwa na England alifunga mabao mawili katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya mahasimu wa Visiwa vya Uingereza, Scotland katikati ya wiki hii ataanza na Robbin Van Persie katika safu ya mashambulizi ya United. Van Persie amefunga mabao matatu dhidi ya timu yake hiyo ya zamani
Wenger ataendelea kukosa huduma ya walinzi wake, Laurent Koncielny na Matheu Debuchy lakini atawakaribisha kikosini kiungo-mshambulizi, Theo Walcott na mshambulizi, Oliver Giroud. Arsenal imekosa matokeo mazuri dhidi ya timu kubwa, tayari wamecheza na Everton, City, Chelsea na hakuna mchezo waliofanikiwa kupata pointi tatu. Walipoteza uongozi wa bao 1-0 na kupoteza mchezo kwa mabao 2-1 dhidi ya Swansea katika mchezo wa raundi ya 10.
Uwepo wa washambuliaji, Danny Welbeck na Alexis Sanchez umekuwa na nafuu katika upatikanaji wa mabao. Wawili hao wamefunga jumla ya mabao 12 katika ligi kuu. Sanchez amefunga mara nane wakati, Danny anakwenda kuikabili timu yake ya zamani akiwa amefunga mabao manne. United itamkosa kiungo-mlinzi, Daley Blindy kwa siku 10, lakini Criss Smalling, Marcos Rojo, Luke Shaw na Rafael Da Silva watakuwepo. Santiago Cazorla, Mikel Arteta, Matheu Flammini, Jacky Wilshere, Tom Rosisck wote wako fiti kwa mchezo wa kesho.
United itakuwa na Marouane Fellaini, Michael Carrick, Angel di Maria, Antonio Valencia, Adnan Januzaj, Darren Fletcher kuhakikisha wanaendeleza umwamba kwa wapinzani wao. Nani mshindi wa mchezo huu?. United wamefunga mabao 14 katika michezo sita ya mwisho dhidi ya Arsenal, labda kufunga tena Jumamosi hii kunaweza kuwapa asilimia kubwa ya kushinda. Arsenal imefunga mabao matano tu katika michezo sita iliyopita dhidi ya wapinzani wao, labda kutokufunga kwao mabao ya kutosha kunaweza kuwafungisha tena, lakini mwamuzi ni dakika 90.
Comments
Post a Comment