KIUNGO WA SIMBA SC AMRI KIEMBA ASAJILIWA AZAM FC, AVUTA DAU LA SH 10 MILIONI.



KIUNGO WA SIMBA SC AMRI KIEMBA ASAJILIWA AZAM FC, AVUTA DAU LA SH 10 MILIONI.

Dar es Salaam. Simba imekubali kumwachia kiungo wake Amri Kiemba achezee kwa mkopo Azam ambako atasajiliwa kwa dau la Sh10 milioni. 


Habari ambazo gazeti hili limezipata zinasema kuwa katika majadiliano baina ya timu hizo mbili, Simba imewapa masharti Azam kuhakikisha hawamtumii Kiemba kwenye mechi kati yao ikiwa ni pamoja na kumlipa mshahara kiungo huyo. 


Simba imetaka ipewe Sh10 milioni na fedha hizo kesho (leo) ziwasilishwe kwa viongozi wao, na pia imetoa masharti Kiemba asicheze kwenye mechi baina ya Simba na Azam na Azam ndio itakayowajibika kumlipa Kiemba mshahara. 


Mwenyekiti wa Azam, Said Mohamed akizungumzia suala hilo, kwa kifupi alisema: "Kesho (leo) Simba itatoa tamko, kila kitu kimeshakamilika." 


Katibu mkuu wa Simba, Stephen Ally alisema wamepokea barua ya majibu kutoka Azam hivi karibuni ya kukataa kutoa kiasi Sh26 milioni huku ikisisitiza kumtaka kwa mkopo. 


"Tunashukuru tumepokea barua ya majibu kutoka Azam ya kumhitaji Kiemba katika usajili wa dirisha dogo, hata hivyo bado hatujamalizana nao. Kuna masuala ambayo hawajayakamilisha, vuta subira hadi kesho (leo)," alisema. 


Katika hatua nyingine, klabu ya Gor Mahia ya Kenya imewaruhusu Simba kuzungumza na mshambuliaji wao, Dan Sserunkuma, huku ikitoa sharti la kumtaka kipa Ivo Mapunda pamoja na Sh60 milioni kama sehemu ya kukamilisha usajili huo. 


Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier alilimbia gazeti hili jana akisema: "Hatujamzuia Sserunkuma kuzungumza na Simba, tumempa uhuru yeye na wakala wake kufanya hivyo, lakini atakapofikia pazuri basi atatushirikisha na sisi kupitia kwa wataalamu wetu tutaangalia ofa ya Simba na kuangalia sisi tunahitaji nini kisha tutatangaza bei tunayotaka. 


"Kama Simba wanamuhitaji basi wajipange pia kwa kuja na Mapunda pamoja na fedha kwani Sserunkuma kwa sasa anawindwa na timu tano tofauti zikiwamo nne za nje ya Afrika na moja ya Kenya. Thamani yake ipo juu sana kwani amekuwa mfungaji bora wa msimu uliopita." 


Naye beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema Simba kwa sasa haimuhitaji Sserunkuma na badala yake inahitaji kuweka jitihada za kutafuta beki mzoefu. Pawasa alisema," Sserunkuma ni mchezaji mzuri na mwenye uwezo wa kimataifa, amedhihirisha hilo, lakini aina ya uchezaji wake ni kama ile anayocheza Okwi, mashaka yangu ataingia kwenye njia za Okwi ambaye pia ni mchezaji wa kutegemewa Simba," alisema Pawasa.
MWANANCHI

Comments