Kila kitu kimekwisha kwa Uganda, ila wanatupa funzo hili…


Kila kitu kimekwisha kwa Uganda, ila wanatupa funzo hili…

ADEBAYORNa Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,

Timu ya Taifa ya Uganda ilianguka kwa mara ya tano mfululizo katika harakati za kufuzu kwa michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON. 'Cranes' walihitaji walau sare tu katika mchezo waliopoteza ugenini dhidi ya Guinea ili wafuzu kwa fainali za Gabon mapema mwakani.

Mchezaji ambaye ameiwakilisha Uganda kwa miaka zaidi ya 13, Andy Mwesigwa aliondolewa uwanjani kwa kadi nyekundu dakika chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili.

Nahodha huyo wa Uganda alitolewa kwa kadi nyekundu wakati, Cranes wakiwa nyuma kwa bao 1-0. Kikosi cha mkufunzi raia wa Serbia, Micho kilipiga shuti moja tu katika lango la wapinzani kwa muda wote wa mchezo. Uganda walikwenda, Guinea kwa lengo la kufuzu kutoka 'kundi la kifo ' ambalo pia lilijumuhisha nchi za Ghana iliyofuzu kama mshindi wa kwanza wa kundi, naTogo iliyomaliza katika nafasi ya mwisho.

Micho1

Mpango wa kwenda kucheza soka la kujilinda ulikufa kabisa baada ya mlinzi-mchezaji na mwenye uzoefu zaidi katika safu ya ulinzi kuondoshwa uwanjani. Uganda iliishinda, Ghana kwa bao 1-0 mwishoni mwa wiki iliyopita, jijini, Kampala na kuruka hadi katika nafasi ya pili ya kundi hilo la tano, lakini kitendo cha kushindwa kupata sare tu ili wafuzu kwa fainali hizo kubwa zaidi za soka barani Afrika.

Kilichotokea kwao ni hali ya kufadhaisha, lakini wataendelea kukumbuka kipigo kutoka kwa Togo katika uwanja wa Nambole mwezi uliopita na kujiuliza ' kwa nini walikubali kufungwa katika michezo yote miwili dhidi ya timu hiyo ya Afrika Magharibi. Togo ilinufaika na ushindi wa michezo yote miwili dhidi ya Cranes kwani ziliwasaidi kwenda Ghana wakiwa na nafasi ya kufuzu. Uganda ilikuwa imefungana pointi saba na Guinea lakini walikuwa na faida ya kufuzu mbele ya timu hiyo kwa matokeo ya sare.

Pointi nne wamechukua kwa vigogo Ghana na nne nyingine dhidi ya Togo zingeweza kuipeleka timu hiyo AFCON, 2015. Ni muendelezo wa matokeo ya kukatisha tamaa, walishindwa kidogo kufuzu kwa fainali za Ghana, 2008, wakaanguka katika michezo ya mwisho wakati wa kufuzu kwa fainali za Angola, 2010, na zile za Gabon & Equator Guinea, wakafungwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti na Zambia na kushindwa kufuzu kwa fainali za Afrika Kusini, 2013.

Uganda ndiyo watawala wa soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Ni timu bora lakini imekuwa ikikosa bahati ya kufuzu. Mbinu ndogo za kupata ushindi katika michezo ya ugenini imekuwa sababu kubwa ya timu hiyo kushindwa kufuzu. Lakini wanaweza kutupa funzo kubwa kuwa kupoteza mchezo katika uwanja wa nyumbani ni makosa makubwa. Togo walichukua pointi tatu Nambole, Guinea na Ghana wote waliacha pointi, hakuna timu iliyotoka salama kati ya hizo mbili zilizofuzu.

Uganda ilipangwa katika kundi gumu ambalo lilihusisha timu tatu zilizozoeleka katika fainali hizo kutoka ukanda wa Magharibi mwa Afrika.

Kizazi cha kina Mwesigwa kimefikia mwisho lakini kimetengeneza njia sahihi kwa Taifa hilo la Afrika Mashariki. Wachezaji wamejitunza kwa muda mrefu huku wakijifunza mbinu mpya kila leo, wachezaji kama Mwesigwa ni msingi imara wa timu lakini huwezi kuwapata kama wachezaji wenyewe hawatajitunza. Uganda imefeli lakini wanaekelea katika mwelekeo bora, siku moja watafuzu.



Comments