Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
BAADA ya kutua nchini jana akitokea kwao Brazil, kiungo mkabaji Emerson de Oliveira Neves Roque ameanza mazoezi mepesi akiwa na Kikosi cha Yanga kwenye uwanja wa shule ya sekondari Loyola jijini Dar es Salaam leo huku uongozi wa Yanga ukisita kumpa mkataba.
Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu amesema jijini Dar es Salaam leo kuwa haijulikani lini kiungo huyo atapewa mkataba wa kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani.
"Siwezi kutabiri Emerson atapewa mkataba lini," amejibu kwa kifupi Njovu baada ya kuulizwa na mtandao huu huku kukiwa na taarifa kwamba uongozi wa Yanga hautaki kukurupuka kumpa mkataba mchezaji huyo hadi pale atakapofuzu majaribio na vipimo vya afya kwa kuwa kocha mkuu Mbrazil Marcio Maximo aliuingiza mkenge kwa mshambuliaji aliyetimka Genilson Santos Santana 'Jaja'.
Jaja aliyeifungia Yanga mabao sita katika mechi 11 (moja katika mechi saba za Ligi Kuu ya Vodacopm Tanzania Bara – VPL) alizocheza katika kikosi cha Maximo, amedaiwa na uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani kukataa kurejea nchini baada ya mapumziko kutokana na kinachodaiwa kukumbwa na matatizo ya kifamilia.
Pengine, uongozi wa wanajangwani umeamua kumalizana naye kistaarabu baada ya kutoridhishwa na kiwango chake.
Mshambuliaji huyo aliyekuwa ameteka vichwa vya vyombo vya habari nchini wakati wa ujio wake uliokwenda sanjari na kiungo Mbrazil mwenzake Andrey Coutinho ameshindwa kung'ara VPL licha ya kufunga magoli mawili ya video katika mechi ya Ngao ya Jamii waliyoinyanyasa Azam FC kwa kuipa kipigo cha mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Septemba 14.
Emerson aliyesafiri kwa zaidi ya saa 11 kutoka jijini Rio de Janeiro, Brazil, ameungana na wachezaji wengine wa Yanga katika mazoezi ya leo ambayo yalikuwa ya kukimbia kimbia yaliyofanyika chini ya Maximo na msaidizi Leonardo Neiva raia wa Brazil pia.
Waandishi wa habari na mashabiki wa Yanga hawakuruhusiwa kuingia kwenye uwanja huo leo na wamelazimika kuyafuatilia mazoezi hayo wakiwa nje ya uzio unaozunguka uwanja na shule hiyo.
Endapo Emerson akifuzu majaribio na vipimo vya afya, imeelezwa na uongozi wa Yanga kwamba ataingia mkataba na klabu hiyo ili aitumikie VPL na michuano ya kimataifa. Yanga itakuwa mwakilishi wa Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani
Comments
Post a Comment