HISTORIA YA MAISHA NASIBU ABDUL DIAMOND PLATINUMZ.



HISTORIA YA MAISHA NASIBU ABDUL DIAMOND PLATINUMZ.
Mkali wa Bongo fleva, Nasibu Abdul au maarufu kwa jina la Diamond akipozi.

ANAITWA Nasibu Abdul au maarufu kwa jina la Diamond. Alizaliwa saa kumi na moja jioni ya Oktoba 2, 1989 katika Hospitali ya Amana iliyopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam. Wazazi wake walimpa jina la Nasibu wakiamini ni la bahati.

Diamond aliongea hivi karibuni na safu hii ya Mjue Huyu ambapo aliweka wazi mambo mengi ya maisha yake. Diamond akiwa hajapata ufahamu, yaani bado mdogo, wazazi wake walitengana kwa sababu ambazo bado hazijawa wazi na baba yake kumuacha na mama.
Kufuatia hali hiyo, ilibidi mama yake ahamie kwa mama yake mzazi (bibi wa Diamond), Tandale Magharibi, Dar. Hapo ndipo yakawa makazi ya mama huyo na mwanaye.
Mnamo mwaka 1995, Diamond alianza elimu ya awali katika Shule ya Chakula Bora iliyopo Tandale- Uzuri. Mwaka 1996 alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Tandale- Magharibi iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mwaka 2000, Diamond akiwa darasa la tano alianza kupenda muziki, hivyo akawa anakopi baadhi ya nyimbo za wasanii waliokuwa wakihiti ndani na nje ya Bongo na kuimba yeye katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. Kwa kuliona hilo, mama yake alianza kumnunulia kanda za albamu za wasanii tofauti hata kumwandikia baadhi ya nyimbo za wasanii hao ili mwanae aweze kuzishika na kuimba kirahisi.
Diamond alizidi kuupenda muziki ikabidi mama yake awe anampeleka kwenye matamasha mbalimbali ili mwanae apate nafasi ya kuimba.

Baadhi ya ndugu walimjia juu mama huyo wakidai anamharibu mtoto badala ya kumuhimiza masomo anamwingiza kwenye muziki ambao walidhani haukuwa na faida yoyote.


Comments