COASTAL: TUTATETEA TAJI KOMBE LA UHAI MSIMU HUU




COASTAL: TUTATETEA TAJI KOMBE LA UHAI MSIMU HUU

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam

hhh

TIMU ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (U20) ya Coastal Union imesema imepania kuhakikisha inatetea taji lake inalolishikilia la michuano ya Kombe la Uhai kwa kufanya vizuri katika mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuanza hivi karibuni nchini.
Coastal Union U20 walitwaa taji hilo msimu uliopita baada ya kuifunga Yanga kwenye mechi ya fainali ya mashindano hayo msimu uliopita iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.
Meneja wa timu hiyo, Abdul Ubinde amesema maandalizi ya timu hiyo kuelekea michuano hiyo yanaendelea vizuri na timu yao inaendelea na mazoezi yake kila siku kwenye Uwanja wa Disuza jijini Tanga asubuhi na jioni chini ya Kocha Joseph Lazaro ambaye amepania kutetea taji hilo.
Ubinde amesema kuwa katika mashindano hayo msimu huu timu hiyo itaingia ikiwa na lengo moja la kuhakikisha wanapambana kutetea ubingwa wake kwa sababu ya uimara wa kikosi hicho.
"Hatuendi kushindana kwenye michuano hiyo, bali kuhakikisha tunatetea taji letu la ubingwa wa michuano hiyo ambao sisi tunaingia kama mabingwa watetezi," amesema.
Ameongeza kuwa kikosi cha timu hiyo kimeimarika vilivyo na kipo tayari kushiriki mashindano hayo kwa mafanikio kutokana na kuwa na wachezaji mahiri wenye uwezo wa kuleta changamoto kwenye michuano hiyo.
Kikosi hicho kinaundwa na wachezaji nyota akiwamo mlinda mlango namba mbili wa kikosi cha Coastal Union inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Fikirini Suleiman 'Mapara', Mohamed Twaha 'Dijong', Mtenje Albano na Mohamed Omari 'Hungry'.
Meneja huyo amesema kuwa wachezaji wa timu hiyo wapo kwenye morali ya kuhakikisha wanafanya vizuri kwa kucheza kwa umakini mkubwa, lengo likiwa kupata matokeo mazuri kila mechi watakayocheza.



Comments