CECAFA YAACHA DENI JINGINE RWANDA



CECAFA YAACHA DENI JINGINE RWANDA

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
WAKATI mabasi mawili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), yanashikiliwa kwa amri ya mahakama baada ya shirikisho hilo kushindwa kulipa deni la Sh. mil 50 katika Hoteli ya Safina Holding za malazi ya maofisa wa Kombe la Kagame 2012, imefahamika kwamba Shirikisho la Soka Rwanda (Ferwafa) nalo lina deni Rwf mil 257 (sawa na Sh. mil 333.28).
Fedha hizo ni gharama za huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na hoteli na mashirika ya usafirishaji ambayo yaliingia makubaliano na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) wakati wa michuano ya Kombe la Kagame nchini humo Agosti mwaka huu.
rwa
Msemaji wa Ferwafa, Moussa Hakizimana amethibitisha kuwa shirikisho bado halijalipa baadhi ya gharama za hoteli na mashirika ya usafirishaji lakini akaongeza kuwa wako katika mchakato wa kulipa.
Aidha, Msemaji huyo ameitupia lawama Wizara ya Michezo na Utamaduni ya Rwanda (MINISPOC) kwa kuahidi kutenga bajeti isiyotekelezeka.
"Hatukutarajia hili. Wametuambia kwamba bajeti ilitengwa lakini watalipa nusu ya kile kilichopangwa. Tunalishughulikia suala hili na linaweza kuchelewa lakini serikali inalitambua," amekaririwa na in2eastafrica.
Bajeti nzima ya Kombe la Kagame nchini Rwanda mwaka huu ilikuwa Rwf mil 417 (Sh. mil 540.77) lakini MINISPOC imelipa Rwf mil 160 (Sh. mil 207.49) na kiasi cha fedha ambacho hakijalipwa ni kinatajwa kuwa Rwf mil 257 (Sh. mil 333.28).



Comments