Mabondia Sweet Kalulu wa Dar es Salaam kushoto na Zumba Kukwe kulia na katikati ni mwandaaji wa pambano hilo George Nyasalu akishuhudia mabondia hao baada ya kupima uzito na afya jana.
Na John Gagarini, Kibaha
BONDIA Zumba Kukwe wa Maili Moja wilayani Kibaha Mkoani Pwani ambaye leo anapambana na bondia Sweet Kalulu amesema kuwa lengo lake kubwa ni kupambana na Thomas Mashali au Kalama Nyilawila.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha wakati wakipima uzito na kupima afya kwenye ukumbi wa Container Bar alisema kuwa leo atamshinda mpinzani wake raundi ya tatu.
Kukwe alisema kuwa kwenye pambano lake la leo anatarajia kufanya vizuri kwa kumpiga mpinzani wake na kuwapa raha wapenzi wa ngumi wa mkoa wa Pwani.
"Nimejipanga vizuri kwenye pambano langu na sitawaangusha wapenzi wangu kwani niko kwenye uwanja wa nyumbani, naangalia mbele zaidi ninaowataka ni Mashali au Nyilawila," alisema Kukwe.
Aidha alisema kuwa anatarajia kuiweka Pwani kwenye ramani ya mchezo huo wa ngumi hivyo malengo yake ni kupambana na mabingwa wa Tanzania.
"Najiamini kuwa nina uwezo na baada ya pambano la leo safari yangu ya kuanza kutamba kwenye ulimwengu wa ngumi itaanza na nitahakikisha ngumi inakuwa juu mkoani Pwani," alisema Kukwe.
Kwa upande wake Kalulu alisema kuwa yeye hana maneno mengi anachosubiri ni muda tu ufike na kila mtu atajua nini kilichomleta Kibaha kwnai anauwezo.
Naye muandaaji wa pambano hilo George Nyasulu alisema kuwa lengo la kuandaa pambano hilo ni kuwahamasisha vijana wanaopenda mchezo huo kujitokeza ili kucheza mchezo huo.
Nyasulu alisema kuwa huo ni mwanzo kwani baadaye ataandaa mapambano mengi zaidi na nia ni kutoa bingwa wa ngumi Taifa kwani vijana wana uwezo.Jumla ya mapambano saba ya utangulizi yatachezwa.
Comments
Post a Comment