BASATA yatoa msukumo Tamasha la Krismasi



BASATA yatoa msukumo Tamasha la Krismasi
SERIKALI kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemtaka Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama kuongeza ufanisi zaidi katika Tamasha la Krismasi mwaka huu kwa sababu  kupitia matamasha yake anafanikisha matakwa ya jamii yenye uhitaji maalum. 

Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mungereza alisema  kwa mwenendo huo bora unaofanywa na Msama anatoa wito kuendeleza mwenendo huo ili kuisaidia jamii.
 
Mungereza alisema Msama anafanikisha hayo kwa sababu anaipenda jamii ambako alitoa wito kwa wadau wa muziki wa Injili kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo linalotarajia kuanza Desemba 25 hapa nchini ili kufikia malengo stahili.
 
Katibu huyo alisema mbali ya kuchangia jamii pia kupitia tamasha hilo wananchi  wa maeneo husika wanapata fursa nyingi katika maeneo yao kama madereva bodaboda, texi na biashara nyingine.
 
"Wananchi wa mikoa itakayofikiwa na tamasha hilo watambue kwamba ni lao, hivyo wajitokeze kwa wingi kwani viingilio vitakavyopatikana vinasaidia wenye uhitaji maalum kama yatima, wajane, walemavu na wengineo," alisema Mungereza.
 
Kuhusu waimbaji, Mungereza alisema waichukulie sanaa kwamba ni kazi  watumie vipaji vyao hasa wakifikiria jamii kwani wanahitajika kutoa elimu ya uraia kutoka kwao.
 
Katika hatua nyingine, Kampuni ya Msama imepokea kibali cha kufanikisha Tamasha la Krismasi mwaka huu ambako kampuni hiyo imejipanga kufanya tamasha hilo katika baadhi ya mikoa hapa nchini.
 
Naye mmoja wa Watendaji wa Kampuni ya Msama, Jimmy Rwehumbiza aliyepokea kibali cha Tamasha la Kriamsi aliishukuru Basata kwa kufanikisha kibali sambamba na kupokea ushauri na mapendekezo yanayotolewa mara kwa mara yanayofanikisha matamasha hayo.


Comments