AZAM KUANZA KUIANDALIA DOZI YANGA KESHO


AZAM KUANZA KUIANDALIA DOZI YANGA KESHO

jemedari

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC baada ya mapumziko ya wiki mbili kesho wataanza mazoezi kujiweka fiti kabla ya kuwavaa Yanga katika mechi yao ya raundi ya nane ya ligi hiyo msimu huu.
Meneja wa timu ya Azam, Jemedari Said amesema jijini Dar es Salaam leo kuwa kikosi chao kitaanza mazoezi mepesi kesho Jumatatu bila mshambuliaji wake Piere Saint Preux ambaye amerejea kwao Haiti na kiungo Michael Bolou ambaye pia amerejea kwao Ivory Coast.
"Kocha msaidizi George Simbe atawasili kesho, wachezaji wanaanza kukusanyika kesho na tutaanza mazoezi kesho pia. Tutaanza kwa mazoezi mepesi maana wachezaji walikuwa mapumzikoni. Lazima twende mdogo mdogo," Jemedari amesema.
"Baada ya kuwasili kwa kocha msaidizi, itatolewa ratiba nzima itatolewa ya mpaka Desemba 28 tutakapocheza dhidi ya Yanga."
Amesema beki wao mpya Serge Wawa atawasili nchini Desemba Mosi na kwamba wachezaji wao walioko kwenye kambi ya Zanzibar Heroes kwa ajili ya michuano inayoonekana kubuma ya Kombe la Chaleni, wataungana na wenzao kesho kwa sababu tayari uongozi wa Azam FC umewasiliana na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).
Azam itakayoiwakilisha Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani, iko nafasi ya pili katika msimamo wa VPL ikiwa na pointi 13 sawa na Yanga walioko nafasi ya tatu, Nafasi ya kwanza inakaliwa na mabingwa wa Tanzania Bara 1999 na 2000, Mtibwa Sugar.



Comments