Na Noreen Ahmad Globu ya                Jamii
        HUKU Dk. Damas Ndumbaro,                akiwa amekata rufaa kupinga adhabu ya kifungo cha miaka                saba kujihusisha na soka ndani na nje ya nchi iliyotolewa                na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),                amesema ataendelea kufanya kazi zake za kuwawakilisha                wadau wa soka watakaohitaji huduma yake ya uwakili.
        Akizungumza jijini Dar                es Salaam leo, Ndumbaro alisema kuwa TFF na Kamati zake                hazina mamlaka ya kumfungia kufanya kazi za uwakili                isipokuwa Jaji Mkuu wa Tanzania na serikali.
        Ndumbaro alisema kuwa                anashangaa kuona amehukumiwa na Kamati ya Nidhamu kwa kosa                la maadili na kuongeza kwamba kamati hiyo haikupaswa                kusikiliza tuhuma zilizokuwa zinamkabili.
        Alisema kuwa adhabu hiyo                aliyopewa ni dalili za wazi za 'chuki' dhidi yake kwa                sababu yeye alichokizungumza ilikuwa ni maamuzi ya klabu                12 za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambazo zilikubaliana                na kumteua yeye kupitia Kampuni yake ya Uwakili ya Maleta                & Ndumbaro ya jijini.
        "Sikuzungumza kwa niaba                yangu, nilikuwa na ridhaa ya klabu 12, isipokuwa Stand                United na Coastal Union, Kamati hii inatumiwa na Jamal                Malinzi, ndio kamati iliyoipa ushindi Stand United kupanda                Ligi Kuu," alisema Ndumbaro.
        Wakili huyo ambaye pia                ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba                alisema kuwa alianza kuonekana ni adui mara baada ya                kukataa kushiriki katika ufujaji wa fedha ambapo kwa                vipindi vitatu tofauti alikataa kusaini hundi za fedha                ambazo TFF iliomba kutoka kwenye Bodi ya Ligi Kuu (TPL).
        Alisema kwamba kwa sasa                shirikisho hilo linakabiliwa na ukata baada ya kutumia                kiasi cha Dola za Marekani 696,823 bila ya kupata kibali                cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambao wamezitoa kwa                ajili ya udhamini wake wa timu ya Taifa (Taifa Stars).
        Mbali na matumizi hayo,                pia Jamal Malinzi anadaiwa kujilipa binafsi Dola za                Marekani 159,140 ndio maana sasa wanaamua kufidia fedha                hizo katika gharama nyingine ikiwamo makato ya Sh.1,000                kwa kila tiketi," alisema Ndumbaro.
        Aliongeza kuwa                anashangaa kuona TFF inaendelea kukata Sh. 1,000 katika                kila tiketi za mashabiki wanaoingia uwanjani kushuhudia                mechi za Ligi Kuu Bara na kutaja kiasi kilichokatwa hadi                kufikia jana ni Sh. milioni 193.2 zilizotokana na                mashabiki 193,257 walioingia viwanjani kushuhudia michezo                ya ligi iliyoanza Septemba 20 mwaka huu.
        Alisema pia anashangaa                kuona rufaa yake aliyokata tangu Oktoba 21 mwaka huu                haijapangiwa siku ya kusikilizwa lakini kikao cha Kamati                ya Nidhamu kilichokutana kumjadili kilichukua siku mbili.
        Aliongeza kuwa leo                Oktoba 31 mwaka huu siku ya 10 na hakuna dalili za                kusikilizwa, tutaendelea kuhesabu,  mambo mengi yako                katika rufaa.
        Alisema kwamba yeye                hajawahi kutoa siri za shirikisho na kueleza kuwa kanuni                za ligi na mikataba inayoingiwa si siri.
        
Comments
Post a Comment