‘ STARS MABORESHO WAPEWE NAFASI YA KUCHEZA MICHEZO YA KUFUZU, OLIMPIKI, 2016, BRAZIL……


' STARS MABORESHO WAPEWE NAFASI YA KUCHEZA MICHEZO YA KUFUZU, OLIMPIKI, 2016, BRAZIL……

Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,

aishi
( Aishi Manula, golikipa wa timu ya Taifa ya Vijana na ile ya wakubwa, Taifa Stars)

Kikosi cha Nigeria ambacho kilishiriki na kutwaa ubingwa wa michuano ya Olimpiki, Atalanta, Marekani, 1994 kilijumuhisha wachezaji waliokuja kutamba barani Ulaya kama, Sunday Oliseh, Austin Jay Jay Okocha, Finidi George, Tijani Babangida, Celestine Babayaro, Godwin Okpara, Victor Ikpeba, Nwanko Kanu wakali wengine wengi. Nigeria iliweka historia ya kuwa timu ya kwanza kutoka barani Afrika kutwaa taji medali ya dhahabu katika michuano hiyo inayofanyika kila baada ya miaka minne wakati wa majira ya kiangazi.

Chini ya kocha, Mjerumani, ' Super Eagle' iliifunga Brazil katika hatua ya nusu fainali wakati huo kikosi cha Mario Zagallo kilikuwa na wakali kama, Roberto Carlos, Ronaldo De Lima, Rivaldo Fereirra, Cafu na asilimia kubwa ya wachezaji ambao waliifikisha Brazil katika fainali ya kombe la dunia, 1998. Nigeria ilisukwa kizalendo licha ya asilimia kubwa ya wachezaji kucheza Ulaya. ' Moyo wa safu ya ulinzi' alikuwa, Taribo West, hakika kilikuwa kizazi cha dhahabu kilichokosa bahati kutoka bara la Afrika.

Nigeria ile haikuwahi kutwaa taji lolote ndani ya bara la Afrika', kitendo cha kupoteza mchezo wa fainali mbele ya Cameroon katika ardhi ya nyumbani katika michuano ya AFCON, 2000 kiliwaumiza mashabiki wengi wa soka duniani ambao walikuwa wakiifuatilia kwa karibu timu hiyo kutoka Ukanda wa Afrika. Kandanda safi muda wote wa michuano, mkusanyiko wa vipaji bora vya soka vyenye uzalendo ndani ya uwanja vilivutia kutazama ' Tai wa Kijani' wakiuzungusha mpira kila sehemu ya uwanja.

Nigeria ilipotea baada ya miaka minne na hapo, ' Simba wasioshindika' wakawavutia wapenzi wa soka. Ushindi wa medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki, Sydney, Australia, 2000 ilikuja baada ya Cameroon kutwaa ubingwa wa AFCON, 2000 kwa kuichapa, Nigeria mwezi, April kwa changamoto ya mikwaju ya penalti. Cameroon walikuwa wakitawala mechi kutokana na kuwa na wachezaji wa ' nguvu-nguvu', Cameroon ilikuwa timu ambayo mataifa mengi ya ulaya ' hawakukuitaka'. Cameron ni mabingwa wa Olimpiki, 2000 tena waliinyamazisha timu iliyotawala dunia kwa miaka minne iliyopita ya Hispania.

Kina, Iker Casillas, Xabi Alonso, Xavi Hernandez, Carles Puyol walikuwa sehemu ya wachezaji wa kikosi cha Hispania ambacho kipoteza mchezo wa fainali wa michuano ya mwaka, 2000 mbele ya Cameroon kwa changamoto ya mikwaju ya penalti. Kiungo, Lauren Etame Mayer alifunga mkwaju wa mwisho wa penalti na kuipatia nchi yake taji.

Patrick Mboma, nahodha, Rigobert Song na Mayer walikuwa wachezaji watatu waliozidi umri wa miaka 23 ambao waliungana na kundi la yosso lililoongozwa na Samuel Eto'o. Ni rahisi kutwaa ubingwa wa Olimpiki kwa timu kutoka barani Afrika kuliko kufika hatua ya nusu fainali ya kombe la dunia. Michuano ya Olimpiki inahitaji mkusanyiko bora wa wachezaji U23, bila kujali ni ligi ipi wachezaji hao wachezaji hao wanachezaji. Kombe la dunia linahitaji maandalizi makubwa sana, wachezaji waliokomaa kiuzoefu, na walio kamili katika ushindani.

jezz

stars

Awamu ya pili ya maboresho ya timu ya Taifa ya kandanda ya Tanzania inaweza kuwa na mafanikio kama wachezaji hao wanaokuwa wakichaguliwa wataendelezwa katika hali ya ushindani. Huwa siungi mkono hoja ya kujitoa katika michuano ya kimataifa. Brazil, Hispani na sasa Ujerumani zimewahi kuwa na vipindi vigumu katika michuano ya kimataifa, barani Amerika na ulaya lakini nchi hizo hazikuwahi kukaa kando katika michuano ili kuandaa kizazi cha mafanikio.

Itazame, Ghana ni nchi iliyotumia vizuri michuano ya kombe la dunia, U21, 2009 kujihimarisha katika ngazi ya kidunia. Mchezaji kijana anapaswa kucheza mfululizo michezo ya ushindani kwa kuwa itamuendeleza kiushindani, kimbinu na kiufundi. Katika kikosi kilichotangazwa na Mkufunzi, Martin Nooij asilimia kubwa ya wachezaji hao wanacheza katika klabu za ligi kuu Tanzania. Kuna wachezaji wengine wamekuwa wakijumuhishwa hadi katika kikosi cha Taifa Stars.

Kuitwa kwao katika awamu ya pili ya ' Stars Maboresho' ni kutokana na ufinyu wa kupenya katika kikosi alisi cha Stars. Golikipa, Aishi Manula, walinzi Edward Charles, Miraj Adam, Hassan Mwasapili ni baadhi ya wachezaji U23 ambao wanatamba katika ligi ya Tanzania lakini hawajawahi kuiwakilisha, Stars.

Mpango huo wa kukusanya vijana wenye vipaji kutoka sehemu mbalimbali za nchi awali uliwahusisha zaidi vijana ambao hawakuwahi kucheza ligi za juu. Mlinzi wa timu ya Simba, Joram Mvegeke ni mmoja wa wachezaji kadhaa waliosajiliwa na timu za ligi kuu msimu huu, haya ni matunda ya ' Stars maboresho'.

Ukosefu wa ligi kuu ya vijana katika soka la Tanzania, ubabaishaji wanaofanyiwa vijana wanaofanya vizuri katika michuano ya muda mfupi ya Copa Coca Cola na Airtel rising stars, mipango mibaya ya klabu za ligi za juu kuhusu soka la vijana kumepelekea timu za Taifa za vijana kufanya vibaya katika kila michuano.

Licha ya kuwa na vipaji, timu za vijana za Tanzania zimekuwa zikitolewa kidhaifu katika michuano ya kimataifa. Mbinu, ufundi ni sababu ya kuanguka kwa kikosi cha U23, 2011 mbele ya Nigeria wakati wa kuwania nafasi ya kucheza michuano ya Olimpiki, 2012, London, England. Chini ya kocha mzawa, Julio kikosi kilichoundwa na wachezaji kama, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta, Himid Mao, Salum Abubakar, Juma Abdul, golikipa, Shaaban Kado na wengineo kiliweza kuwatoa mabingwa wa michuano wa mwaka, 2000, Cameroon kabla ya kubanwa katika uwanja wa Taifa na kufungwa 3-0 nchini, Nigeria katika raundi ya mwisho ambayo mshindi alifuzu kwa hatua ya makundi kuwania nafasi nne za bara la Afrika.

stars 1
( Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta wakiwa na kocha wa zamani wa Stars, Mdenish, Kim Poulsen)

Uwezo mdogo kiufundi na kimbinu ulifanya timu hiyo kushindwa kupata ushindi katika uwanja wa nyumbani na hilo lilichangiwa na kukosekana kwa michezo mingi kwa vijana wa Tanzania. Hoja yangu inalenga ' jaribio ambalo Tanzania' inaweza kulifanya ili ' kubahatisha ' kufuzu kwa michuano ya Olimpiki, 2016, Rio de Janeiro, Brazil kwa kujaribu kutumia asilimia kubwa ya vijana ambao wanapatikana katika mpango wa ' Stars Maboresho'. Tunahitaji ligi kuu ya vijana yenye ubora, lakini wakati huo huo tukijihimarisha kiuzoefu kwa kujaribu kufuzu katika kila michuano ya vijana inayokuja mbele yetu.

Kikosi na Nigeria, 1996 kilichaguliwa kutoka klabu za ulaya na hivyo pia ilikuwa kwa Cameroon, lakini uwezo wa Ghana katika kombe la dunia, 2009, Misri ulijumuhisha kundi kubwa la vijana waliokuwa wakicheza soka barani Afrika. Mshambulizi, Dominic Adiah alikuwa nyota wa michuano. Sasa kuna ulazima wa wadau wa kandanda Tanzania kujaribu kuusaidia mradi huo ambao wengi hatuupendi. Ligi kuu ya muda mrefu ya vijana itakuwa mkombozi wa soka la Tanzania, Stars Maboresho si tumaini la kufaa, tujaribu mpango huo kujaribu kwenda Brazil, 2016.



Comments