SIMBA IKASOME MASHAIRI NA KAULI ZA UMOJA ZILIZOMSHANGAZA JIMMY CARTER.


SIMBA IKASOME MASHAIRI NA KAULI ZA UMOJA ZILIZOMSHANGAZA JIMMY CARTER.

Mwaka 1990 alizaliwa mtoto wa ajabu huko Marekani. Matthew Stepanek,mtoto aliyewashangaza wamarekani wengi.Stepanek aliishi miaka 13 tu Duniani.Kabla umauti kumkuta akiwa na umri huo wa miaka 13 alishatunga Vitabu bora vitano vya mashairi.Wamarekani walikua wakimuita 'peace advocate'(wakili wa amani) kutokana na mashairi yake yaliolenga hasa kwenye Amani,Umoja na Mshikamano. Mashairi yake yaliwasisimua watu wengi wakiwamo watu maarufu kama Oprah Winfrey, Larry King.Lakini zaidi alikua Jimmy Carter,Rais wa 39 wa marekani.Carter alidiriki kusema "katika maisha yangu yote sijawai kumshuhudia mtu wa ajabu kama Stepanek".Jimmy Carter alikua muumini mkubwa wa mashairi ya Stepanek yaliyohamasisha umoja baina ya watu wa Marekani. "Unity is strength.when there is teamwork and collaboration,wonderful things can be achieved".(Umoja ni nguvu.Kila kwenye ushirikiano na kufanya kazi kwa umoja,Mambo mazuri yanaweza kufikiwa).Hii ni moja ya kauli zake pendwa na ya kukumbukwa ya Stepanek iliyohusu umoja.
Huo ni Ubongo wa mtoto aliyeishi kwa miaka 13 tu lakini unashinda bongo za watu wengi wenye umri mkubwa.Nashukuru Mungu nilikua mmoja wa watu walioshuhudia mechi ya Simba na Prisons katika uwanja wa Sokoine.Wakati nasafiri kuelekea mbeya mpaka naangalia dakika 90 za mechi hiyo niligundua kuwa Simba ina tatizo moja tu la kukosa umoja.Simba imekosa hekima aliyekuwa nayo mtoto mdogo Stepenak.Simba haina umoja kuanzia kwa viongozi,Wanachama,Benchi la ufundi mpaka wachezaji.
Benchi la ufundi la simba bila shaka limekosa mawasiliano mazuri.Wakati mechi ikiendelea kuna muda niliona Phiri na msaidizi wake Matola wanapishana kauli.Napata mashaka kama maamuzi ya kiufundi kama yanatolewa na benchi nzima au mtu mmoja pekee.Tangu nianze kushuhudia soka sijawai ona mabadiliko mabovu mwalimu anafanya kama aliyoyafanya phiri.Kwa kumuingiza kiemba na kutoka kwa Ndemla pale phiri alizidiwa akili na mamilioni ya watanzania. Kuna muda naona kabisa Phiri anafanya maaumizi bila kushirikisha benchi lake la ufundi.Sidhani kama Matola aliridhia mabadiliko yale mabovu yaliyofanywa na kocha phiri.Phiri anaweza kuwa kocha mzuri kuliko Matola,Lakini Matola anawajua wachezaji wa simba vizuri kuliko Phiri.Wachezaji wengi wa simba wamefika hapo walipo kwa nguvu za Matola.Phiri anachopaswa kufahamu kuwa Matola ana nguvu kubwa ndani ya kikosi cha Simba.Lakini pia kuna tetesi ndani ya timu hiyo ya kuwa kocha huyo msaidizi anahusika kuigawa timu hiyo kupitia baadhi ya wachezaji,nilipomuuliza kocha huyo alikataa katakata,lakini lisemwalo lipo kama halipo basi li njiani.Kitu cha msingi ni kumaliza tofauti zilizopo ndani ya benchi la ufundi.Lazima kuwepo na umoja, ushirikiano na mawasiliano mazuri kati ya kocha na wasaidizi wake.
aveva

Nikihama kwenye benchi la ufundi nagundua pia wachezaji wa simba pia wamegawanyika.Kuna siku niliandika kuhusu simba walivyokosa muunganiko 'chemistry'.Lakini wakati wa mechi yao na Prisons nikagundua kuna mgawanyiko zaidi ya 'chemistry' ndani ya timu hiyo.Nilianza kugundua tu wakati Singano anatoka kupisha Haruna chanongo.Jicho la chanongo liliniambia kuna kitu kinaendelea ndani ya kichwa cha Singano.Pia machozi ya Okwi na Jonas Mkude kuna kitu yalikua yanamaanisha.Waswahili wanasema 'ukimuona mtu mzima analia ujue kuna jambo'.Jicho la chanongo kwa Singano,Machozi ya okwi na mkude,Pia kujituma kwa wachezaji wachache uwanjani kunanifanya niamini kabisa kuna kitu kinaendelea baina ya wachezaji wa simba.Niliposikia Amri kiemba amesimamishwa Simba wala sikushangaa,Lakini bado nawaza kama Singano nae ataendelea kuwa mchezaji wa Simba.Wachezaji wa simba waliopo wanaonekana hawapo tayari kufanya kazi pamoja.Wachezaji hao licha ya kutoelewana ndani ya uwanja wanaonekana hawaelewani zaidi nje ya uwanja.
Nikirudi kwa viongozi wa simba nahisi huko ndipo matatizo yanapoanzia.Kuna viongozi Simba wanaonekana kuwa na sauti kubwa ndani ya timu kuliko vyeo walivyo navyo.Siku hizi yupo kiongozi ambaye anatoa taarifa zote za simba ingawa si msemaji wa simba.Msemaji ni yeye,Mwenyekiti wa kamati ya ufundi ni yeye na mara nyingine huvaa viatu hata vya Raisi wa klabu.Kuna muda nafikiria nguvu ya Raisi wa simba ndani ya timu hiyo.Nahisi kuna watu wana nguvu zaidi ya Raisi huyo wa simba.Pia kuna taarifa nilizipata za kutokuwa na maelewano kati ya viongozi wawili wa juu wa simba.Sasa kama baba na mama hawaelewani ndani ya nyumba watoto ndani ya nyumba hiyo wataanzaje kuelewana?.Wachawi wakuu wa simba ni viongozi wenyewe.Kutoelewana kwao ndio kunaleta kuhujumiana.
Kiukweli hali ya simba si nzuri,hali hiyo inapelekea hata kuchukiana baina ya wanachama wa matawi ya timu hiyo.Viongozi wa simba inabidi wawekane sawa na kila mmoja ajue mipaka ya uongozi wake sambamba na kushirikiana na viongozi wengine na kuvunja makundi yaliyopo ndani ya timu hiyo.Kuelewana kwa viongozi kutaleta maelewano baina ya wanachama,benchi la ufundi na hata wachezaji.Biblia yangu inaniambia hata Mungu hupendezwa na watu wanaokaa pamoja na kufanya kazi kwa umoja.Kama viongozi hao wanaona tabu kusoma biblia yangu basi wakasome mashairi ya umuhimu wa umoja ya Stepanek yaliyomshangaza Raisi Jimmy Carter.
Na ALLEN KAIJAGE
Kaijagejr@gmail.com
0655106767



Comments