Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL)            inayoshirikisha timu 24 zitakazocheza katika makundi manne ya            timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza            kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu.
                 Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la            Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyoketi jijini Dar es Salaam            jana (Oktoba 29 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Geofrey            Nyange ilipitia maandalizi maandalizi ya ligi hiyo ikiwemo            mwongozo wake (roadmap).
                 Kwa mujibu wa mwongozo huo, usajili            wa wachezaji utamalizika Oktoba 31 mwaka huu. Kipindi cha            pingamizi ni kuanzia Novemba 1 hadi 7 mwaka huu wakati Kamati            ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inatarajia kukutana Novemba 11            mwaka huu kwa ajili ya kupitisha usajili.
                 Pia Kamati ya Mashindano imepitisha            viwanja vya timu zote, isipokuwa uwanja wa timu ya Mpanda            United ya Katavi na ule wa Town Small Boys ya Tunduru mkoani            Ruvuma. 
                 Uwanja wa Town Small Boys            haukupitishwa kwa vile hauna uzio wa kudumu ( wa chuma) wa            kutenganisha wachezaji na washabiki, na pia ufikaji wa timu            Tunduru ni mgumu kutokana na ubovu wa barabara ikizingatiwa            kuwa ligi hiyo itachezwa hadi kipindi cha Masika.
                 Kwa upande wa uwanja wa Mpanda            United, umekataliwa kwa vile hauna vigezo vya msingi            vinavyotakiwa ikiwemo vyumba vya kubadilishia nguo, kutokuwa            na nyasi na uzio wa kudumu kutenganisha wachezaji na            washabiki.
                 Kutokana na uamuzi huo, Mpanda United            sasa itatumia Uwanja wa Mandela uliopo Sumbawanga wakati Town            Small Boys itachezea mechi zake kwenye Uwanja wa Majimaji            mjini Songea.
        
Comments
Post a Comment