RAGE: SIMBA MSIMTIMUE PHIRI



RAGE: SIMBA MSIMTIMU PHIRI

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam

ISMAIL Aden Rage, aliyekuwa mwenyekiti wa Simba, ameuomba uongozi mpya wa klabu hiyo kutomtimua kocha Patrick Phiri kutokana na matokeo mabovu ya timu yao kwa kuwa Mzambia huyo ameikuta timu ikiwa na hali mbaya.
Uongozi mpya wa Simba chini ya Rais Evans Aveva umemtaka Phiri ashinde mechi mbili zijazo dhidi ya vinara wa msimamo Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting, vinginevyo kibarua chake katika klabu hiyo ya Msimbazi kitaota nyasi.
Akizungumza katika kipindi cha 'Spoti Leo' cha Radio One usiku wa kuamkia leo, Rage amesema Phiri amerudi Simba katika kipindi kigumu, hivyo anapaswa kupewa nafasi zaidi ya kukisuka kikosi cha timu hiyo.
"Phiri amekuja muda wakati mbaya Simba, Tuna matatizo ya 'defence' (ulinzi) tangu kuondoka kwa (Donald) Mosoti. Sijui kwa nini beki huyo aliondolewa Simba," amesema Rage.
"Kama ningelikuwa bado kiongozi wa Simba, ningeangalia mchezaji mwingine wa kumwacha badala ya Mosoti, kwanza jina lake tu, anatisha yule kijana," ameongeza Rage huku akikosoa vikali vitendo vinavyoashiria ushirikina vilivyotawala Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu.
rage
Amesema kuwa watu wanaoamini ushirikina, hawana imani ya Mungu huku akipinga pia kusimamishwa kwa wachezaji watatu wa Simba; viungo Amri Kiemba na Shabani Kisiga pamoja na winga Haroun Chanongo.
"Ninawaheshimu viongozi wapya wa Simba kwa sababu ni viongozi wetu. Ninaamini mazungumzo yao na wachezaji waliosimamisha yatakuwa mazuri na watawarejesha kikosini kwa sababu tatizo la Simba ni kuondoka kwa Mosoti," amesema.
"Kama hutaki sare na kufungwa, usiingie kwenye mashindano. Sisi tunachotakiwa ni kujifunza kwa nchi zilizoendelea kisoka, kuandaa timu kuanzia timu za vijana. Inashangaza kuona tunawekeza zaidi katika imani za kishirikina," amesema zaidi Mbunge huyo wa Tabora Mjini (CCM).
Simba iliyokamata nafasi ya 10 katika msimamo wa VPL baada ya kuambulia sare katika mechi tano zote za mwanzo, Jumamosi itakuwa na mtihani mgumu mbele ya kikosi cha kocha Mecky Mexime cha Mtibwa Sugar ambacho hakijapoteza mechi hata moja tangu kuanza kwa msimu Septemba 20 kikiongoza ligi kwa kushinda mechi nne na kutoka suluhu mara moja dhidi ya Pilisio Morogoro.
Simba haijapata ushindi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro dhidi ya mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Tanzania Bara 1999 na katika mwaka wa mabadiliko ya karne tangu iliposhinda 2-1 msimu wa 2011/12. Timu hiyo ya Msimbazi ilifungwa 2-0 na wakatamiwa hao wa Manungu, Turiani msimu wa 2012/13 kabla kutoka sare ya bao moja msimu uliopita.



Comments