Ndanda waikimbia Azam Nangwanda…..


Ndanda waikimbia Azam Nangwanda…..

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
BAADA ya Kikosi cha Ndanda FC kuukimbia mji wa Mtwara, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC wamesema watakuwa wenyeji wa mji huo kuelekea mechi yao ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini humo.
Akiwa Mtwara leo mchana, Ofisa Habari wa Ndanda FC, Idrissa Bandali ameuambia mtandao huu kwa simu kuwa kikosi chao kimeingia mafichoni kwenye kambi maalum nje ya mji huo kujiweka sawa kabla ya kuivaa Azam FC.
"Azam ni timu nzuri, tunaielewa vizuri ndiyon maana tumeamua timu iweke kambi maalum nje ya mji kusaka dawa ya kupata ushindi Jumamosi," amesema Bandali.
Hata hivyo, ofisa habari huyo hakuwa tayari kutaja mahali ambako timu yao imepiga kambi kwa madai kuwa ni siri.
Baada ya kupata kocha mpya, Omar Mingange aliyesaini mkataba wa miaka miwili, Bandali amesema wanaendelea kusaka kocha wa makipa kuziba pengo la Muharami Mohamed aliyetimuliwa.
Msemaji wa Azam FC,Jaffari Iddi, amesema kikosi chao kinatarajiwa kuondoka jijini kesho asubuhi kwenda Mtwara tayari kwa mechi yao ya Jumamosi dhidi ya timu hiyo iliyopoteza mechi nne mfululizo baada ya kushinda 4-1 ugenini dhidi ya Stand United mjini Shinyanga.
NDANDA
"Kama wao wamehama mjini, basi sisi tutakuwa wenyeji. Tunakwenda mapema ili tukazoee mazingira na baadaye Jumamosi tutawakarisha Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda," amesema Jaffari.
Azam FC ilipokea kichapo cha kwanza baada ya kucheza mechi 38 za VPL bila kupoteza ilipofungwa 1-0 nyumbani dhidi ya JKT Ruvu, kikiwa pia ni kipigo cha kwanza kwa kocha wake Mcameroon Joseph Omog tangu atue msimu uliopita akiiingoza timu hiyo katika mechi 18 bila kupoteza hata moja.
Aidha, Meneja wa timu ya Azam, Jemedari Said amesema kikosi chao kinachokwenda Mtwara kitakuwa na mshambuliaji wake kutoka Haiti, Lionel Saint-Preux aliyeanza mazoezi siku mbili zilizopita baada ya kupona maumivu ya nyama aliyoyapata katika mechi ya Ngao ya Jamii waliyolala 3-0 dhidi ya Yanga Septemba 14.
Azam iliyoshinda mechi tatu, sare moja na kupoteza moja, iko nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 10, tatu nyuma ya vinara Mtibwa Sugar wakati Ndanda FC iliyotimua kocha mkuu, Dennis Kitambi na kocha wa makipa, iko nafasi ya pili kutoka mwisho ikiwa na pointi tatu.



Comments