MTIBWA: SIMBA INACHEZA KAMA TIMU DARAJA LA NNE


MTIBWA: SIMBA INACHEZA KAMA TIMU DARAJA LA NNE

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
UONGOZI wa Mtibwa Sugar umesema haukihofii kikosi cha Simba kuelekea mechi baina yao itakayopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro Jumamosi kwa kuwa timu hiyo kwa sasa inacheza ovyo kama timu ya daraja la nne.
Simba chini ya kocha Mzambia Patrick Phiri aliyepewa sharti la kushinda mechi mbili zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara ili kulinda ajira yake, Jumamosi itakuwa na kibarua kigumu mbele ya kikosi cha kocha mzawa Mecky Mexime kinachoshikilia usukani wa msimamo wa ligi hiyo kikiwa kimeshinda mechi nne na kutoka sare mara moja.
Akiwa Morogoro, msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema timu yao iko imara na haina cha kupoteza dhidi ya Simba.
"Simba ni timu mbovu msimu huu, inacheza ovyo kama timu ya daraja la nne," amesema Kifaru.
"Wana wachezaji vijana lakini hawajitumi. Watawaua wazee na mashabiki wao wanaokuja kuangalia mechi yetu ijayo. Waje Uwanja wa Jamhuri waone namna tunavyoifunza soka Simba Jumamosi.

MTIBWA
"Tunamshauri kocha Patrick Phiri na wasaidizi wake waanze kukusanya kila kilicho chao Simba maana sharti walilopewa ni gumu mbele ya Mtibwa Sukari. Mechi yetu dhidi ya Mbeya City ndiyo ilikuwa ngumu, kwa Simba ni kunawa tu," amesema zaidi Kifaru.
Simba iliyoko nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi baada ya kuambulia sare tano mfululizo katika mechi tano zilizopita, haijawahi kuifunga Mtibwa kwenye Uwanja wa Jamhuri tangu msimu wa 2011/12 iliposhinda 2-1. Msimu wa 2012/13 ilipigwa 2-0 kabla ya kulazimishwa sare ya bao moja msimu uliopita.
Mtibwa Sugar iliyowahi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara mara mbili mfululizo 1999 na katika mwaka wa mabadiliko ya karne, inajinafasi kileleni mwa msimamo wa VPL msimu huu ikiwa imejikusanyia pointi 13 katika mechi tano, pointi tatu mbele ya mabingwa watetezi Azam FC walioko nafasi ya pili na Yanga walioko nafasi ya tatu.
Simba itatua mjini Morogoro Ijumaa ikitokea Iringa ilikopiga kambi kujiandaa kwa mechi ya Jumamosi.



Comments