mexime: Simba wataalam wa kuchonga maneno, nitawajibu Jumamosi uwanjani


mexime: Simba wataalam wa kuchonga maneno, nitawajibu Jumamosi uwanjani

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
MECKY Mexime, kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, amesema hana muda wa kufikiri kuhusu sharti la kuifunga timu yake lililotolewa na uongozi wa Simba kwa benchi la ufundi timu hiyo ya Msimbazi badala yake atawajibu uwanjani wakati timu hizo zitakapopambana katika mechi ya raundi ya sita ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Jumamosi.
Akizungumza na mtandao huu akiwa kambini Manungu, Turiani jana mchana, Mexime alisema Simba ni wataalam wa kuongea lakini akawataka kuelewa kwamba kikosi chake kimejipanga kufanya kweli msimu huu.
"Kuna maneno mengi yanasemwa kuhusu mechi yetu dhidi ya Simba. Mara lazima makocha wao washinde mechi yetu, vinginevyo watafukuzwa, hayo ni maneno tu. Kazi itakuwapo uwanjani Jumamosi," amesema Mexime.
Nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars amesema kikosi chake kiko salama na kinaendelea kujifua kambini Manungu km 100 kutoka mji wa Morogoro na kitaingia mjini humo Jumamosi tayari kuikabili Simba.

mecky
" Tunamshukuru Mungu hatuna mchezaji anayeumwa, tutajibu tambi za Simba uwanjani kwa sababu msimu huu tumepania," ameongeza kocha huyo aliyeweka wazi kwamba msimu huu Mtibwa itamaliza katika moja ya nafasi mbili za juu.
Mtibwa Sugar inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 13, tatu mbele ya Azam na Yanga zilizopo nafasi za pili na tatu, haiojafungwa na Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri tangu msimu wa 2011/12 ilipopoteza 2-1 kabla ya kushinda 2-0 msimu wa 2012/13 na kutoka sare ya bao moja msimu uliopita.
Usajili wa mshambuliaji Ame Ally Shomary kutoka Chuoni FC ya Ligi Kuu ya Zanzibar, kumeiimarisha zaidi safu ya ushambuliaji ya Mexime ikifunga magoli nane huku safu ya ulinzi ikiruhusu goli moja tu, tofauti na Simba waliofunga magoli matano na kufungwa matano pia.
Safu ya ulinzi ya Simba iliyopwaya mno baada ya kutemwa kwa beki Mkenya Donald Mosoti itakuwa na wakati mgumu mbele ya washambuliaji Ame, Musa Mgosi na Vicent Barnabas ambaye mara nyingi amekuwa akitokea benchini na kufanya 'vitu vya maana'.
Mtibwa imepanga kushinda mechi 10 kati ya 13 mzunguko wa kwanza wa VPL msimu huu.



Comments