MATOLA, PEP, NA MAFANIKIO ALIYOYATAMANI VAN GAAL KUTOKA LA MASIA….



MATOLA, PEP, NA MAFANIKIO ALIYOYATAMANI VAN GAAL KUTOKA LA MASIA….

matola

Na Baraka Mbolembole

Luis Van Gaal alikuwa na ' ndoto kubwa ', mkufunzi huyo raia wa Uholanzi alishinda taji la ligi ya mabingwa Ulaya, Mei, 1994 akiwa kocha wa Ajax Amsterdam. Van Gaal aliwahi kunukuliwa akisema anataka siku moja kushinda ubingwa wa Ulaya akiwa na wachezaji 11 kutoka Academy ya La Masia-shule ya vipaji vya soka ya klabu ya FC Barcelona ya Hispania.

La Masia ni ' zao' la shule ya soka ya klabu ya Ajax ambayo, Van Gaal aliipatia ubingwa wa ulaya huku akiweka rekodi ' isiyofikiwa' hadi sasa. Ajax ndiyo timu iliyochukua ubingwa wa klabu barani Ulaya ikiwa na wachezaji wenye wastani wa umri mdogo zaidi. Licha ya mafanikio hayo, Van Gaal alitaka jambo la maana zaidi katika historia ya soka lakini hakuwahi kulipata. Ndoto ya kutwaa ubingwa wa ulaya akiwa na ' kundi la nyota 11 kutoka La Masia' ilishindikana baada ya kocha huyo wa sasa wa klabu ya Manchester United ' kuwakumbatia' wachezaji wa kigeni zaidi huku wale raia wa Uholanzi wakitawa Camp Nou.

Michael Reizger, Frank na Ronald Debour, Phillip Cocu, Zenden, Marc Overmans na Patrick Kluivert walikuwa wachezaji wasiokosekana katika kikosi cha kwanza cha Van Gaal pale Camp Nou, wote hao walikuwa ni wachezaji wa timu ya taifa ya Uholanzi ambao waliupendezesha mchezo wa ' total football' wakiwa na Uholanzi katika fainali za kombe la dunia, 1998, Ufaransa na Uefa Euro, 2000, iliyofanyika kwa ushirikiano wa nchi mbili za Uholanzi na Ubelgiji.

Oranje walitajwa kama timu ' isiyo na bahati' yote kutokana na kandanda la kuvutia kutoka kwa nchi hiyo ya Ulaya. Rivaldo Ferreira, Geovanni, Thiago Motta, Luis Figo, Ricardo Quaresma ni wachezaji wengine kutoka nchi za Brazil na Ureno ambao walipewa kipaumbele na Van Gaal katika kikosi cha kwanza cha Barcelona wakati huo. Soka zuri, mpira wenye mbinu na mipango ni vitu ambavyo vilivutia wengi kuwatazama Barca, lakini haikuwahi kuwateka wapenzi wengi wa soka kwa kuwa timu hiyo ' haikuwa ikitwaa mataji au kufanya vizuri katika ligi ya ulaya'.

Xavi Hernandez, Pep Guardiola na mchezaji wa zamani wa Real Madrid ambaye aligeuka kipenzi cha mashabiki pale Camp Nou, Luis Enrique walikuwa wazawa pekee ambao walibaki katika mipango ya Van Gaal. Barcelona haikuwa na taji la La Liga kwa misimu mitano mfululizo ambayo Van Gaal alifanya kazi kwa vipindi viwili.

Alipoondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Mholanzi mwenzake, Frank Rijkaard mambo yalibadilika kwa kuwa Barca ilitwaa mataji mawili ya La Liga na moja la Ulaya katika kipindi cha miaka mitano. Miaka miwili ya mwisho ya Rijkaard ilikuwa ni migumu kwa klabu nzima, timu haikutwaa taji lolote ( 2007, 2008 huku msimu wa mwisho, Rijkaard akimaliza katika nafasi ya nne na kutolewa katika nusu fainali ya ulaya na Manchester United.

Wazo ambalo alikuwa nalo, Van Gaal lilikuja kufanyiwa kazi na Pep Guardiola-nahodha wa zamani wa Barca chini ya Van Gaal. Pep alikuwa kocha wa La Masia-Barcelona B kwa miaka miwili, na aliweza kuitoa timu hiyo ya pili ya Barca ligi ya tatu hadi ligi ya Segunda B ( Ligi daraja la kwanza ). Alipopewa kazi ya kukinoa kikosi cha kwanza cha Barcelona, Agosti, 2008 alitangaza wazi kuwa hatohitaji huduma ya wachezaji, Ronaldinho Gaucho, Deco De Souza na Samuel Eto'o.

Si sababu za 'kibaguzi' ambazo zilimfanya, Pep kuwatema nyota hao, ' sababu za kimpira' zilihitaji jambo hilo litokee. Gaucho, Deco na Eto'o ' walijiona walishamaliza', walitajwa kama wachezaji ' chachu ya mafanikio' ya Barcelona ambayo ilififia kwa miaka mingi. Watatu hao waliipaisha timu, lakini waliiporomosha kwa kasi baada ya kutumia muda mwingi kufanya maisha ya nje ya uwanja huku wakimkosoa kocha wao. Pep, alitaka kutengeneza ' Barca mpya' ambayo msingi wake ni La Masia sehemu ambayo watoto zaidi ya 300 huitimu mafunzo ya soka kila mwaka.

Siku ya kwanza akiwa katika mazoezi ya Barcelona kama mkufunzi mkuu, Pep alimuita pembeni kiungo, Xavi na kumwambia huku akimuonyesha kwa kidole alipo, Andres Iniesta;

" Unamuona yule kijana, naomba umpe ushirikiano katika kila kitu. Naitengeneza timu yangu kupitia yule ( Iniesta)". Ulikuwa ujumbe wa kwanza kwa wachezaji lakini ulifikishwa kwa siri kubwa. Aliyefahamu ni Xavi kwa upande wa wachezaji, na Pep kwa upande wa benchi la ufundi. Iniesta mwenyewe hakufahamu chochote, na Xavi alijua hilo tu.

Ila Pep alikujana ' ingizo la ajabu', alimpandisha katika kikosi cha kwanza cha Barca kutoka timu ya pil kijana mwenye rekodi za ajabu Sergio Busquetsi. Wakati huo timu ya Rijkaard ilikuwa ikiwategemea zaidi, Edmilson, Thiago Motta na Yaya Toure katika nafasi ya kiungo wa ulinzi ambaye alicheza nyuma ya Deco, Gaucho na Lodovic Giuly. Pep alivunja muhimili huo huku falsafa ya soka la kushambulia na kupasiana likimpatia mafanikio makubwa katika msimu wake wa kwanza ambao alitwaa mataji matatu kwa mpigo, Copa del Rey, La Liga na ligi ya mabingwa ulaya.

Gerlad Pique ni kijana wa La Masia ambaye, Pep alimsajili kutoka Manchester United. Golikipa, Victor Valdes, C. Puyol, Pique, Xavi, Bisquets, Iniesta, Leonel Messi wote walitwaa ubingwa wa ulaya wakitokea, La Masia. Pedro Rodriguez aliongezeka miaka miwili baadae waliposhinda ubingwa wa ulaya kwa mara ya tano na ya mwisho mwaka 2011. Hata, Pep hakufanikiwa kuchukua ubingwa wa ulaya akiwa na wachezaji 11 kutoka La Masia, alifanikiwa kuchua mara mbili ubingwa huo katika miaka minne aliyofanya kazi Camp Nou, mara ya kwanza, 2009 alichukua akiwa na wachezaji saba katika kikosi cha kwanza kutoka shule ya soka ya klabu hiyo, mara ya pili alichukua akiwa na vijana nane kutoka La Masia.

SULEIMANI MATOLA SI PEP ILA MTAZAME VIZURI…….

Kwa nini nimeeleza yote haya. Unamtaza vipi, Suleimani Matola? nahodha wa zamani wa klabu ya Simba SC ambaye alishinda mataji 13 tofauti akiwa na beji hiyo. Matola amezaliwa kuwa ' mshindi daima', mchezaji bora zaidi namba 6 kuwahi kutokea katika ' karne mpya ya soka la Tanzania'. Alipokwenda Afrika Kusini na kucheza soka la kulipwa kwa miaka miwili katika timu ya Super Sports United, 2005-07 alifanikiwa kushinda taji la PSL
Aliporudi Tanzania alisajiliwa tena na Simba kabla ya kupelekwa kwa mkopo katika timu ya Moro United. Mwaka 2008 alijiunga na Azam FC na alikuwa miongoni mwa wachezaji walioisadia timu hiyo kupanda daraja na kucheza ligi kuu katikati ya mwaka huo. Matola aliamua kustaafu soka la ushindani na kugeukia kazi ya ukocha. Baada ya kazi ya kujitolea akishirikia na Geofrey Nyange Kaburu wawili hao walianzi ' timu kivuli ya vijana ya Simba
katikati ya mwaka 2009.
Hadi wanafikia wazo hilo, Kaburu alivutiwa na kipaji na uwezo wa ufundishaji wa Matola ambaye alitwaa taji la kombe la Taifa ' Taifa Cup' akiwa na timu ya Mkoa wa Singida katikati ya mwaka huo. Kaburu aliamua kumuendeleza Matola kwa kumsaidia kupata kozi mbalimbali za ukocha ambazo zimeendelea kumpatia mbinu mpya. Matola alifanikiwa kushinda mataji mawili katika muda wa miaka mitatu akiwa na timu ya vijana.
Pia, Matola alikuwa kocha wa kikosi cha vijana cha Simba ambacho kilipewa nafasi ya kucheza michuano ya ' Muungano, timu nne za Bara na nne za Visiwani ambazo zilimaliza katika nafasi nne za juu katika ligi kuu zao'. Matola alitwaa ubingwa huo katikati ya mwaka 2012. Edward Christopher alikuwa nyota wa ' michuano' huku vijana wengine kama, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Said Ndemla, Miraj Adam, Abdallah Seseme, William Lucian, Haroun Chanongo, Ramadhani Singano wakitia ' fora' kwa mchezo wao mzuri.

Miaka miwili imepita, Simba ikiwa bila taji lolote tangu walipotwaa ubingwa wa Super8, wachezaji watano walianza katika kikosi cha kwanza siku ya Jumamosi iliyopita dhidi ya mahasimu wao Yanga. Singano alikuwa mchezaji wa sita wa U21 ambaye ametokea timu ya pili, kiungo huyo wa kushoto aliingia katika kipindi cha pili wakati, Lucian, Isihaka, Mkude, Ndemla na Chanongo walipoanza. Manyika Peter Manyika, Mohammed Hussen na Elius Maguli walikuwa vijana wengine wa U21 ambao walianza katika mchezo huo.

Simba wameonyesha mfano mzuri lakini ni lazima waendelee kuwasaidia vijana hao kukua vizuri kimchezo. Ni jambo la kujiamini sana ambalo wamelifanya, na endapo wataendelea kuwajenga vijana hao katika mwendo huo upo uwezekano wa timu hiyo kupata mafanikio kupitia mradi wao wa soka la vijana. Nyange Kaburu, makamu wa rais wa sasa wa Simba amewahi kunieleza kuwa lengo kuu la klabu ni kutengeneza wachezaji wao wenyewe, kuwatumia kimpira na kibiashara. Kama ungekuwepo uvumilivu kidogo tu, Shomari Kapombe angekuwa nahodha wa Simba katika mchezo wa Jumamosi, huku Christopher akiongoza mashambulizi. Kwa hili, Barca ya Pep si Simba ya Matola, ila mtazame vizuri Sele.

0714 08 43 08



Comments