Na Mwandishi Wetu Mbeya
KIPA kinda wa Simba, Peter Manyika Jr amejikuta akilia kama          mfiwa baada ya kufungwa goli la usiku katika sare ya bao moja          dhidi ya Tanzania Prisons mjini hapa jana.
          Goli la winga mtokea benchini Hamis Maingo dakika moja kabla ya          mechi kumalizika liliipa sare ya usiku Prisons kwenye Uwanja wa          Kumbukumbu ya Sokoine mjini hapa jana na kumuacha kipa huyo          akiangua kilio baada ya kuikosesha timu yake ushindi wa kwanza          msimu huu.
          Baada ya mechi kumalizika kipa nambari moja Simba Ivo Mapunda          alimfuata Manyika Jr kumkumbatia huku akimwambia "vumilia mdogo          wangu, ndivyo mpira ulivyo."
          Goli la Simba lilifungwa na mshambuliaji kutoka Uganda, Emmnuel          Okwi dakika nne tu baada ya kipyenga cha refa Othman Lazi kutoka          Morogoro kupulizwa.
          Goli walilofingwa lilionekana kumuuma zaidi Manyika Jr kwani          wakati wenyeji wanafanya shambulizi, alikuwa amelala amelala          kuashiria kuumia ikiwa ni janja ya kupoteza muda lakini baada y          mfungaji kukaribia lango, kipa huyo aliyedaka mechi ya watani          wiki mbili zilizopita, aliinuka lakini tayari alikuwa          ameshachelewa.
          Ni goli la kwanza kwa kipa huyo msimu huu huku makipa chaguo la          kwanza Ivo na chaguo la pili Hussein Sharrif 'Casillas'          wakifungwa magoli mawili kila mmoja.
          Kwa matokeo hayo, Simba inakamata nafasi ya 11 katika msimamo wa          ligi ikiwa na pointi tano baada ya kuambulia sare katika mechi          zote tano za mwanzo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
          Mechi ya jana pia ilikuwa ya 11 kwa wekundu kucheza ligi kuu          bila kupata ushindi tangu waifunge Ruvu Shooting mabao 3-2 miezi          saba iliyopita.
Comments
Post a Comment