KIPIGO CHA AZAM FC NA STORI YA MBWIGA BWIGUKE KUTOKA AZAM COMPLEX HADI SANTIAGO BERNABEU!



KIPIGO CHA AZAM FC NA STORI YA MBWIGA BWIGUKE KUTOKA AZAM COMPLEX HADI SANTIAGO BERNABEU!

Na Shaffih Dauda

KIMAHESABU huwezi kutoka pointi A kwenda B bila kupitia kitu kiitwacho mchakato hapa katikati!
Maisha siku zote ni mchakato mrefu na huwa unahitaji kujiamini, kujituma na kuvumilia.
Tanzania hii kuna watangazaji wengi wa redio wenye vipaji vikubwa, lakini kila mtu ametoka kimpango wake.
Wengine safari yao haijawahi kupitia michakato migumu kufika hapo walipo, lakini wengine wakisimulia njia walizopitia utabaki kushangaa tu!.
Dunia hii inazingatia sana rekodi kubwa wanazoweka watu, lakini kuna mambo ambayo hutokea kwenye maisha ya watu wa kawaida na huwa yanafurahisha na kutoa somo kubwa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Azam fc walifungwa goli 1-0 na Maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Chamazi Complex.
2

Mrisho Ngasa ( kushoto ), Shaffih Dauda na Freddy Montero kwasasa anaichezea Sporting Lisbon ya Ureno.

Haya ni matokeo ya kawaida katika soka, lakini yamejenga rekodi moja 'matata' kwa Mtanzangazaji wa kituo cha redio na Televisheni cha Clouds, Mbwiga Mbwiguke.
Wengi wamemfahamu Mbwiga kutokana na umahiri wake wa kutangaza hususani kuchekesha, lakini hawajui kufungwa kwa Azam kumeweka rekodi gani.
Ngoja nikwambia kitu! Mwezi Julai, 2011 nilikwenda nchini Marekani kutazama mechi ya kirafiki kati ya timu ya Seatle Sounders dhidi ya Manchester United ya England.
Hii ni safari yenye kumbukumbu kwangu kwasababu nilimuona kiungo mshambuliaji wa Tanzania, Mrisho Khalfani Ngassa 'Anko' akifanya majaribio ya kusaka nafasi ya kucheza soka la kulipwa katika ligi ya Marekani.
Ngassa wakati huo alikwenda kufanya majaribio katika timu ya Seattle ya Marekani akitokea Azam FC, lakini kwa bahati mbaya mambo yalimwendea vibaya.
Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha! Safari yangu ikafikia ukingoni na ikanibidi nirudi nyumbani Tanzania. Nakumbuka ilikuwa kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
3

kutoka kushoto :Ashley Young,Shaffih Dauda na Luis Nani

(Kama kawaida yangu, napenda sana kujiweka 'fiti' kwa kufanya mazoezi. Nikawaza kuhusu hilo baada ya safari, nikabeba vifaa vyangu na kwenda uwanja wa shule ya msingi Muhimbili ambapo nafanyia mazoezi.
Nakumbuka baada ya kumalizika kwa mazoezi, nilijipumzisha na baadhi ya wachezaji wenzangu, Clement Kahabuka ( mchezaji wa zamani wa Simba SC) , Munje ( rafiki wa karibu wa Mbwiga), pamoja na Ally Mayay ( mchezaji wa zamani wa Yanga SC).Pia alikuwepo Mbwiga Mbwiguke.
Huyu ni mtu wa 'ajabu' sana! Wakati tunapiga 'stori', Mbwiga alikuwa anatoa simulizi zake za kuvunja mbavu, hakika kila mtu alipata burudani 'bab kubwa'.
Muda ulizidi kwenda , Mbwiga ' akanipiga mzinga'. Jamaa alikuwa ' kachoka' kweli. Ilinibidi niende kwenye gari yangu na kuchukua kiasi kidogo cha hela na kumpatia. Nakumbuka ilikuwa ni Tsh.2000/= , haraka akaitia mfukoni akijua ni Tsh.5000/=
Mbwiga aliondoka na wenzake na walipofika maeneo ya 'Fire' walitaka kugawana ile hela, wote walijua ni Tsh.5000/=! Lakini alipoitoa mfukoni na kuifungua akakuta ni ' buku mbili'. Nini kilifuata?
Kesho yake nikiwa katika shughuli zangu, nilipata simu kutoka kwake. Katika uongeaji wake wa utani akaniambia; "wewe ni mjanja sana, mimi nilijua umenipa dola ulizorudi nazo kutoka Marekani kumbe umenipa ' Buku 2'. Niliondoka nikiwa na matumaini makubwa, jamaa zangu walikuwa wameniganda hadi tunafika stendi wakijua ni ' mzigo wa maana'. Tulipofungua na kukuta ni 2000 tulichoka, ikabidi tuanze kupanga mipango ya kugawana nauli".
1

Mbwiga Mbwiguke ( kushoto ) akiwa na shabiki rafiki wa Ramadhan Chombo 'Redondo' -picha hii ilipigwa tarehe 23/8/2011 ( siku ambayo Azam FC ilifungwa kwa mara ya kwanza na African Lyon kwenye uwanja wa chamazi )

Nimekumbuka kitu! wakati tunapiga 'stori' pale uwanjani kuhusu mambo ya mpira, Ally ( Mayay) akaniambia; " Mchukue huyu mtu-akimaanisha Mbwiga". Jibu langu lilikuwa rahisi tu! nitamchukua.
Baada ya pale hatukukutana tena na Mbwiga mpaka Agosti 23 mwaka 2011, siku ambayo Azam fc kwa mara ya kwanza walipigwa goli 1-0 na Africa Lyon katika uwanja wao wa Chamazi Complex.
Wakati Azam wakifungwa kwa mara ya kwanza katika uwanja wao, Mbwiga yeye alikuwa akifanya kazi za usafi ndani ya uwanja huo baada ya mechi kumalizika.
Mbwiga alikuwa akiokota chupa za maji zilizotumika, kuweka mazingira ya uwanja katika hali ya usafi, lakini alikuwa ni mchekeshaji mzuri kwa mabosi wake pale Azam.
Nakumbuka baada ya mechi hiyo kumalizika nilikuwa nafanya mahojiano na kiungo Adam Kingwande wa Lyon ambaye alifunga bao pekee la Lyon.
Ikiwa ni muda umepita, kwa mara nyingine tena Mbwiga alifika mahali nilipokuwa na Kingwande akiwa na 'Yule shabiki wa Ramadhani Chombo 'Redondo'.

4

Adam Kingwande ( kushoto )-mfungaji wa bao pekee la African Lyon mnamo 23/08/2011

Mbwiga akaniambia; "Kaka hapa tunaishi kama Simba" akimaanisha kuwa bila kuwa na nguvu hupati chakula na akaniomba nimtoe buku. Nilimsikiliza na kumuelewa kwasababu nilikuwa nimevutiwa na uzungumzaji wake wa kuchekesha.
Nakumbuka baada ya wiki moja nilimpigia simu na kuanza kumrekodi akiwa kule kule Azam Complex.
Baadaye aliniambia kuwa kila nilipokuwa nikimpigia simu akiwa Azam Complex ilimbidi ajifiche ili awe huru kuzungumza.
Wakati mwingine nilikuwa nikimpigia simu akiwa katika daladala jambo ambalo lilimfanya kuomba muda ili atakaposhuka tuzungumze.
Cha kukumbuka zaidi ni kwamba, kwa mara ya kwanza Azam fc inafungwa katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Lyon miaka mitatu iliyopita, ndio wakati ambao Mbwiga alipata fursa ya kuanza kufanya mambo Clouds FM.

5

Mbwiga Mbwiguke akiwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu siku ambayo Azam FC ilipoteza mchezo wa pili kwenye uwanja wa Chamazi dhidi ya JKT Ruvu…..

Ilikuwa ni siku ya Ijumaa ya tarehe 26/8/2011 ambapo alianza kuripoti Clouds FM kwa kutumia simu akiwa kazini kwake ( wakati huo Azam Complex Chamazi).
Stori inayovutia sasa ni kwamba, maisha yamekwenda kasi kwa Mwiga kutokana na upambanaji wake.
Ni rekodi nzuri sana! Wakati Azam fc inafungwa bao 1-0 kwa mara pili jumamosi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu, Mbwiga alikuwa katika dimba maarufu la Santiago Bernabeu kushuhudia mechi kali ya El Clasico baina ya Real Madrid na Barcelona.
Matokeo hayo waliyopata Azam fc yanafanana na yale waliyopata dhidi ya Africa Lyon miaka mitatu iliyopita na Mbwiga akiwa mfanyakazi wa usafi katika uwanja wa Azam Complex.
Safari hii Azam wanafungwa tena nyumbani kwao kwa mara ya pili, Yule Yule Mbwiga alikuwa nchini Hispania.
Hakika Mbwiga ni mpambanaji wa kweli, ametumia vyema kipaji chake na sasa ni mtu maarufu nchini. Je, Mbwiga ana nini na Azam FC? Je siku Azam FC ikifungwa tena kwenye uwanja wa Chamazi Mbwiga atakuwa wapi ?



Comments