FAHAMU WALICHOKISEMA YANGA BAADA YA KASEJA KUTAKA KUVUNJA MKATABA NAO



FAHAMU WALICHOKISEMA YANGA BAADA YA KASEJA KUTAKA KUVUNJA MKATABA NAO

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
BAADA ya kipa Juma Kaseja kuweka wazi kwamba yuko tayari Mkataba wake Yanga uvunjwe iwapo klabu hiyo haitatekeleza mambo mawili, moja kuanza kumpa nafasi za kudaka katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani umejibu kauli hiyo.
Kupitia meneja wake, Abdulfatah Salim, Kaseja ameipa masharti Yanga SC kama inataka kubaki naye immalizie fedha za usajili wake za usajili Sh. milioni 20 na pia kuanza kumpa nafasi ya kudaka.
Alipotafutwa na mtandao huu baada ya kuenea kwa taarifa za Kaseja kutaka kuondoka Yanga, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu amesema: "Mchezaji Juma Kaseja hana meneja anayetambulika na taasisi yoyote, iwe YANGA, TFF au hata FIFA."
Njovu ameenda mbali zaidi akinukuu baadhi ya vipengele vya FIFA kwa kusema: "Mawakala wa wachezaji wahatambuliwi na FIFA tangu 2001. Mawakala wa wachezaji wanasajiliwa moja kwa moja na kila chama cha soka. Hivyo, hakuna kitu kama hicho kuwa na wakala wa FIFA wa mchezaji."
Aidha, Njovu amesema: "Jukumu la kupanga timu ni la kocha, wala si mtu yeyote."
kas

ALICHOKINUKUU NJOVU HIKI HAPA KWA KIINGEREZA
"Players' agents have not been licensed by FIFA since 2001. Players' agents are licensed directly by each association. Therefore, there is no such thing as a FIFA players' agent."

Kaseja, kipa huyo namba moja wa zamani wa Tanzania, hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga chini ya kocha Mbrazili Marcio Maximo.
Katika kipindi cha kocha Mholanzi Hans van der Pluijm, Kaseja alikuwa anadaka kwa zamu na kipa chaguo la kwanza Yanga, Deogratius Munishi 'Dida'.
Abdulfatah amesema kuwa katika mkataba wao walioingia na Yanga, walikubaliana kukamilishia malipo ya mwisho ya dau la usajili ya (Sh milioni 20) ifikapo Januari 15, mwaka huu, lakini klabu hiyo hadi sasa alidai haijafanya hivyo.
Amesema wakati wanavumilia hilo, bado mteja wake hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza jambo ambalo ni hatari kwa kipaji cha kipa huyo wa zamani wa Simba.
Abdulfatah amesema wanayaingiza masharti hayo yote kwa maandishi na kuyapeleka kwa uongozi wa Yanga uyatekeleze, vinginevyo hatua za kuuvunja mkataba zitafuata. Meneja huyo, hakutaka kuweka wazi lini watakabidhi barua hiyo kwa uongozi wa Yanga, hata hivyo.
Kaseja ameidakia Yanga mechi 15 tangu asajiliwe mwishoni mwa mwaka jana, akiwa kipa huru baada ya kuachwa na Simba kwa madai ya kushuka kiwango. Kati mechi hizo, tano ni za Ligi Kuu na moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi hizo Kaseja amefungwa mabao 10, yakiwamo matatu Yanga ikilala 3-1 mbele ya mahasimu, Simba katika mechi ya 'ndondo ya 'Nani Mtani Jembe' iliyomfukuzisha kocha Mholanzi Ernie Brandts.
Pamoja na kuwa kipa chaguo la kwanza Simba kipindi hicho, Kaseja hakuwahi kumvutia Maximo alipokuwa akiifundisha timu ya taifa (Taifa Stars) na wakati fulani alidiriki kuwaita Ali Mustafa 'Barthez' na Dida, akimuacha Kaseja.
Wakati Kaseja akitaka kuvunja mkataba wake na Yanga, tayari kumeshaanza kuenea taarifa kuwa timu yake ya zamani ya Simba inataka kumrejesha wakati wa usajili wa dirisha dogo msimu huu



Comments