FAHAMU ALICHOKISEMA PHIRI BAADA YA KUPEWA MECHI 2 SIMBA


FAHAMU ALICHOKISEMA PHIRI BAADA YA KUPEWA MECHI 2 SIMBA

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Kocha mkuu wa Simba, Mzambia Patrick Phiri amesema kuvunjwa kwa mkataba wake hakutakuwa na manufaa yoyote kwa klabu hiyo ya Msimbazi iliyopoteza ghafla matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba iliyoko nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi hiyo, imeambulia sare tano mfululizo katika mechi tano zilizopita hali iliyopelekea uongozi kumtaka kocha huyo ashinde mechi mbili zijazo, vinginevyo atatimuliwa.
Akiwa mjini Iringa ambako timu yake leo jioni inacheza mechi ya kirafijki dhidi ya Lipuli kujiandaa kwa mechi ya raundi ya tano dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi, Phiri amesema ajira yake si suala muhimu Simba bali wanapaswa kuumiza vichwa kufikiri namna ya kuisaidia timu hiyo kongwe nchini.

phiri
Kocha huyo alikiri kupewa taarifa hiyo na uongozi wa juu wa Simba uliokuwa mjini Mbeya mwishoni mwa wiki chini ya Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva, ambao pia uliwasimamisha na kuwataka kurejea Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi viungo Amri Kiemba na Shaban Kisiga pamoja na winga Haroun Chanongo muda mfupi baada ya timu yao kutoka sare ya 1-1 na wenye Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini humo Jumamosi.
"Ni kweli utawala umenipa mechi mbili kuhakikisha timu inashinda, kinyume chake wamesema watavunja mktaba wangu. Lakini ajira yangu Simba si suala muhimu kwa sasa kulijadili. Kilicho muhimu kwetu kwa sasa ni kuangalia matatizo yanayoikabili timu na kuyatafutia dawa," amesema Phiri.
"Mimi nina muda mfupi, sidhani kama ajira yangu ni tatizo Simba," ameongeza kocha huyo mwenye historia ya kuipa ubingwa wa Tanzania Bara timu hiyo bila kupoteza hata mechi moja.
Simba anainoa Simba kwa awamu ya tatu baada ya kuifundisha pia 2005 na 2010. Ni kocha wa 18 kuifundisha timu hiyo ndani ya miaka 16 tangu 1998



Comments