CHAZ BABA ACHAFUA HALI YA HEWA MASHUJAA BAND …tetesi za kusimamishwa zazagaa



CHAZ BABA ACHAFUA HALI YA HEWA MASHUJAA BAND …tetesi za kusimamishwa zazagaa
CHAZ BABA ACHAFUA HALI YA HEWA MASHUJAA BAND …tetesi za            kusimamishwa zazagaa

RAIS wa Mashujaa Band, Chaz Baba wiki iliyopita alichafua hali ya hewa kwenye bendi yake baada ya kukwaruzana na viongozi wa ngazi za juu wa bendi hiyo na baadae kutoonekana kwenye maonyesho yaliyosalia ya wiki nzima.

Ilikuwa ni katikati ya wiki kwenye ukumbi wa Flamingo Magomeni ambapo inadaiwa Chaz Baba alichukizwa na kitendo cha Jado FFU aliyekuwa amesimamishwa, kurudishwa kazini bila yeye rais wa bendi kujulishwa.

Saluti5 imeelezwa kuwa Chaz Baba ambaye alichelewa kufika ukumbini, alikuwa mbogo baada ya kukuta Jado FFU yupo mzigoni.

Ripota wa Saluti5 amedai mtafaruku ulikuwa mkubwa kiasi cha mashabiki wengi kubaini kuwa kuna 'sintofahamu' inayoendelea.

Baada ya onyesho hilo, Chaz Baba hakuonekana tena kazini wiki hiyo, huku wengine wakisema kasimamishwa kazi na wengine wakisema kajisimamisha mwenyewe.

Hata hivyo mmoja wa viongozi wa Mashujaa Band licha ya kukiri kuwa Chaz Baba alikosa adabu, lakini akaweka wazi kuwa mwimbaji huyo hakusimamishwa.

Naye Chaz Baba alipoulizwa na Saluti5 alisema hajasimamishwa wala kujisimamisha bali hajaonekana kazini kufuatia kusumbuliwa na tumbo.

"Tumbo lilikuwa linanisumbua nikashindwa kufika kazini kwa siku mbili tatu, ila yaliyopita yamepita, wiki hii ntakuwepo kazini kama kawaida," alisema Chaz Baba kwa njia ya simu.

Kwa wiki za hizi karibuni kumekuwa na ukosefu wa nidhamu kwa baadhi ya wasanii wa Mashujaa Band na kupelekea baadhi ya yao kusimamishwa kazi.

Mbali na mwimbaji Jado, wasanii wengine waliokumbana na rungu la nidhamu, ni marapa Sauti ya Radi na Ferguson.



Comments