‘ BAADA YA KIEMBA, KISIGA, CHANONGO, ANAYEFUATA NI PHIRI………


' BAADA YA KIEMBA, KISIGA, CHANONGO, ANAYEFUATA NI PHIRI………

Na Baraka Mbolembole

Awali wakati wa majira ya usajili nchini, timu ya kandanda ya Simba SC iliamua kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake. Ikiwa chini ya rais, Evance Aveva, Simba iliamua kumfuta kazi aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mcroatia, Logarusic na kumuajiri, Patrick Phiri kutoka Zambia. Mabadiliko yalifanyika hasa, wachezaji wa kila aina walisajiliwa huku wale walioshindwa kufanya vizuri msimu uliopita wakiachwa.

Lengo ya uongozi mpya ilikuwa ni kuifanya klabu kurudi katika hali yake ya ushindani ambayo katika kipindi cha miezi 34 sasa imeshuka kwa kiwango kikubwa. Sijui sana kuhusu mwanzo wa tawala nyingine katika timu hiyo ulivyokuwa, lakini katika kipindi cha 14 ya karibuni nadiriki kusema, uongozi wa sasa umeanza vibaya zaidi. Sababu ni nyingi lakini kubwa zaidi ipo katika utawala.

Capture
Sehemu ya wachezaji wa kikosi cha Simba SC kilichomaliza katika nafasi ya nne msimu wa 2013/14 katika ligi kuu Tanzania Bara.

Simba inayumbishwa na viongozi wake wenyewe ambao wanakataa kukubali makosa waliyofanya mara baada ya kuingia madarakani. Kitendo cha kuwafuta uanachama baadhi ya waliokuwa wanachama wa klabu kinawagharimu wakati huu. Ulikuwa ni uamuzi ' mbaya' ambao awali nilisema utakuwa tatizo kwa timu. Hapa sizungumzii kuhusu sera za Aveva ambazo zilimfanya aingie madarakani, kwani kama utazama na kugusa huko vile ilivyo sasa ' ameshindwa vibaya', alikuwa na sera mbovu, lakini si hivyo ' sera ya pointi 3' imekufa, hivyo ni lazima zitazamwe sababu zilizofanya sera hiyo kutokuwa na mafanikio.

Katika mchezo wa kwanza wa msimu huu, Simba ilicheza na Coastal Union ya Tanga katika uwanja wa Taifa, ilionekana kama vile mambo yatakwenda sawa msimu huu baada ya Shaaban Kisiga kufunga bao la ' mkwaju wa penalti'. Lilikuwa bao la kwanza la msimu kwa Simba, na lilifungwa na mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kikosini tena ' kwa kutumia maarifa binafsi'. Amis Tambwe akafunga bao la pili, lakini mambo yalikuwa magumu dakika 25 za mwisho. Coastal walichomoa mabao yote na kutengeneza sare ya kufungana mabsao 2-2. Halikuwa tatizo, hakukuwa na hujuma.

1
Kiungo wa Simba SC aliyesimasimshwa Amri Kiemba ( kulia) akiwajibika katika mchezo dhidi ya Polisi Morogoro ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Mchezo wa pili ulikuwa ni dhidi ya Polisi Morogoro, pia ulipigwa katika uwanja wa Taifa. Simba iliongoza kwa bao la mshambulizi, Emmanuel Okwi. Ndani ya nusu saa ya mchezo. Mshambulizi wa zamani wa Simba Danny Mrwanda akiitumia vizuri ' pasi ya kupenya' iliyopigwa na kiungo Salum Machaku na kuisawzishia timu yake dakika tano tu mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili. Mechi ikamalizika kwa sarte ya kufungana bao 1-1. Hapa kidogo maswali yakaanza kujitokeza, kiwango kibovu kutoka kwa baadhi ya wachezaji kilifanya wengi kuanza kujiuliza kulikoni.

2
Amis Tambwe, mfungaji bora wa ligi kuu Tanzania Bara, 2013/14 ambaye tsayari amefunga bao moja msimu huu. Tambwe alifunga mabao 19 katika michezo 24 msimu uliopita

UONGOZI, BENCHI LA UFUNDI, WACHEZAJI WAKAA KIKAO NA MATIZO YATAJWA….

3

Katika hali ya kutojiamini, ama kutoheshimu timu pinzani. Uongozi wa Simba ulikaa chini na kufikia mwafaka wa kuhitisha kikao cha siri kati ya utawala, benchi la ufundi na wachezaji. Bila uoga baadhi ya wachezaji walisema kuwa matokeo ya sare mbili mfululizo yaliletwa na ushirikiano mdogo uliopo katika timu. Hawakugusia mambo yaliyopo katika uongozi bali walisema ' wachezaji kwa wachezaji' hawapeani ushirikiano ule wa kimpira wakiwa uwanjani. Ilikuwa no hoja ambayo ndani yake ina mantiki kwa sababu kuna baadhi ya viongozi wameonekana kuwagawa baadhi ya wachezaji na kuwapendelea wengine kwa sababu tu mchezaji Fulani hajasajili na ' mtu/wati fulani'

Baada ya kikao hicho mambo yalikwenda vilevile. Mchezo wa tatu ulikuwa ni dhidi ya Stand United ya Shinyanga ambao nao ulifanyika katika uwanja wa Taifa. Kisiga akitokea benchi kuchukua nafasi ya Said Ndemla aliyeumia alifunga bao lake la pili msimu huu, pia lilikuwa bao la kwaju ' uliokufa'. Katika ligi ambayo mabao kadhaa yamefungwa kwa mipira ya adhabu ndogo, Kisiga angweza kuipa Simba pointi ' tatu za kwanza' msimu huu kama tu safu ya ulinzi isingeendeleza ' tabia yao ya kukubali kuruhusu bao la kuswazishwa'. Mwishoni mwa mchezo Stand walichomoa na kutengeneza sare ya ' Tatu mfululizo katika uwanja wa nyumbani'.

4
Haroun Chanongo naye pia amesimamishwa

Katika mchezo wowote huwa tunasema; ' asiyekubali kushindwa, si mshindani', lakini katika fikra za kishabiki, matokeo ya Simba yalipangwa. Hivyo ndivyo wanavyoamini baadhi ya viongozi. Nahodha, Joseph Owino aliwekwa benchi katika mchezo dhidi ya Stand na nafasi yake kuchezwa na chipukizi, Joram Mvegeke. Sijui kama yalikuwa ni mapendekezo ya Phiri mwenyewe kama mkuu wa benchi la ufundi, au ni muendelezo wa makocha ' dhaifu wa kigeni' ambao wanaendeshwa ' kwa rimoti' na baadhi ya watu wenye kuwashikilia?. Kama tatizo la kwanza ilionekana ni Owino, Simba hawakung'amua chanzo cha tatizo lenyewe.

Je, baada ya Owino kuwekwa benchi, safu ya ulinzi ilifanya kazi nzuri zaidi?. Matokeo yalikuwa ni ' yale yale tu'. Mchezaji pekee ambaye hajakosekana katika safu ya ulinzi ya Simba msimu huu ni Hassan Isihaka. Kiwango chake ni kizuri lakini kama sababu ni hujuma, wengine wote waliofanyiwa mabadiliko hawakuleta afadhali yoyote hadi pale Owino alirudishwa katika mchezo dhidi ya Yanga ambao ni pekee Simba hawakufunga bao wala kuruhusu goli msimu huu.

Kihistoria, Simba ilipaswa kuchukua pointi tatu dhidi ya Polisi Moro kwa sababu huwa hawana uwezo wa kuifunga timu hiyo ya Morogoro ikiwa nyumbani katika miaka ya karibuni. Sare dhidi ya Coastal ni kielelezo cha ugumu wa ligi ya msimu huu, sare ya Stand ni matokeo ya soka tu. Huku suluhu dhidi ya Yanga ilichukuliwa kama ' mwisho wa matatizo'. Hawakujua, kumbe ni mwanzo wa kuelekea kipigo cha kwanza msimu huu.

KUWATIMUA KAMBINI, KIEMBA, KISIGA NA CHANONGO………

Wakati Fulani msimu uliopita ulipokuwa ukielekea mwishoni, niliwahi kuhoji kiwango cha kiungo Haroun Chanongo. Ukweli wakati ule wa mchezo dhidi ya Mbeya City uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 niliamini kuwa, Chanongo ni mchezaji mwenye ' tabia ya kupanda na kushuka kwa kiwango chake'. Lakini kuanzia msimu huu, mchezaji huyo amekuwa juu, lakini ametimuliwa kambini kwa sababu za kudaiwa kuchangia matokeo mabaya ya timu. Kivipi?

Okwi alifunga bao la kuongoza kwa timu yake na kuifanya iwe mbele kwa bao 1-0 katika uwanja ambao wameishinda, Tanzania Prisons mara mbili tu katika kipindi cha miaka 14 sasa. Zikiwa zimesalia tano mchezo kumalizika Prisons waliswazisha. Simba imepata pointi ya kwanza katika uwanja wa ugenini msimu huu baada ya kufungana bao 1-1 na Prisons lakini hilo limeambatana na kusimamishwa kwa baadhi ya wachezaji. Chanongo, Kiemba na Kisiga. Lakini katika hali ya kimpira tuhuma hizo si za kweli zaidi ya ' chuki binafsi alizonazo' mwenyekiti wa kamati ya usajili kwa wachezaji hao ambao hakuwasajili yeye. Majuzi alisikia mwenyekiti huyo wa kamati ya usajili akisema kuwa kila anapopangwa Kiemba timu yao haishindi. Je, huu ndiyo weledi wa kiuongozi. Ule mgawanyiko ambao wachezaji waliusema katika kikao unaletwa na viongozi kama hawa ambao wanasema tu wachojisikia.

Nathubutu kusema kuwa baada ya sare tano mfululizo, Simba itapigwa na Mtibwa Sugar wikiendi ijayo na baada ya hapo atakayefuata ni kocha Patrick Phiri. Lakini Simba SC inaharibiwa na hao jamaa zao wenyewe, ' Watu wakubwa'. Wakati wa uongozi wa Mh. Aden Rage nilikuwa nikipenda kutumia sentesi ya ' Mtu mkubwa ni Mwanafunzi', hutamani vitu vingi zaidi. Labda Phiri apange wachezaji wote waliosajiliwa na ' Mbwana Mkubwa' ndipo Simba itashinda!!. Nyakati za furaha zimepotea klabuni huku ndani ya uwanja matokeo yakiwa ' hovyo'.

5

Felix Sunzu ( kushoto) marehemu, Patrick Mafisango ( katikati), na Emmanuel Okwi wakishangilia moja ya ushindi wa Simba msimu wa 2011/12 ambao Simba ilitwaa ubingwa wa mwisho.

Msiwape lawama ' wale-Simba Ukawa' ambao hawajulikani wanaishi wapi, ' adui wa kwanza wa Simba ni Pesa', Si Kiemba, Kisiga wala Chanongo. Niliwahi kuandika ' Phiri atafukuzwa kazi Simba SC…..', Phiri yupo katika ' shinikizo la chinichini' hivi sasa. Hakuna, Simba ukawa ila kuna watu ndani ya Simba yenyewe wanataka Simba ifungwe sasa na si kutoa sare, unajua ni kwa nini? Mtu mkubwa ni Mwanafunzi tu.
0714 08 43 08



Comments